Thursday, 18 August 2011

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE. MCHUNGAJI PETER MSIGWA, (MB) WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA 2011/2012.


 Mbunge wa iringa Mjini-Chadema Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa
---

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani,nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi yetu kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) na (7) toleo la 2007.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumsifu, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye nguvu na hekima tele kwa kunipa afya njema na kuendelea kunipigania kwenye kila jambo. Kama alivyomuwezesha Daudi kuibuka mshindi dhidi ya Goliath, jitu kubwa na lenye nguvu nyingi, ndivyo alivyoniwezesha mimi kushinda uchaguzi na kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Kwa makusudi yake maalum, ambayo sina budi kuyatekeleza nikifuata uongozi wake, namshukuru kwa kunifanya sehemu ya Bunge hili la Kumi, ambalo binafsi naamini ni Bunge la Kimapinduzi. 

Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa, namshukuru mke wangu mpenzi, Mama Kisa Msigwa, watoto wetu Jimmy, Peter Junior, Semione, Karren na mapacha wetu, Jacqueline na Jocelyn, kwa upendo na sala zao kwangu. Na huko waliko nawaomba wakumbuke kuwa; The value of our dignity in this World will never be determined by what we have accumulated, but rather for what we have contributed. Thamani ya utu wetu hapa duniani haitatokana na kile tunachokichuma katika jamii, bali itatokana na kile tunachojitolea kwa jamii. Naisihi familia yangu iendelee kuniunga mkono wakati wote ninapokuwa mbali, nikishughulikia kero na matatizo ya wananchi wa Iringa Mjini. 

Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Iringa Mjini kwa kunielewa, kuniamini na hatimaye kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mbunge wao. Wazee wa Iringa Mjini, Vijana wa Iringa Mjini na akina Mama wa Iringa Mjini, kwa hiyari yao wenyewe waliamua kuchagua uadilifu dhidi ya ufisadi, umakini dhidi ya usanii, na walichagua haki dhidi ya dhuluma. Nawasifu, nawapongeza na ninawashukuru kwa ujasiri na ushujaa wao mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni zetu na hasa wakati wa kulinda kura zao. Nawapenda, na Mungu awabariki sana. Sitawaangusha.

Mheshimiwa Spika, shukrani na pongezi zangu za dhati pia nazielekeza kwaviongozi wakuu wa CHADEMA, kwa kukiongoza vema chama chetu na kuwa tumaini pekee na la uhakika la Watanzania wengi. Mwanafalsafa mmoja maarufu wa karne ya 16, katika moja ya maandiko yake aliwahi kusema, `Weak leaders inspire their followers to have confidence in them. But Great leaders inspire citizens to have confidence in themselves

Viongozi dhaifu huhamasisha kuaminiwa na wafuasi wao, lakini Viongozi makini huhamasisha wananchi wajiamini’,mwisho wa kunukuu.Leo Watanzania wamejitambua zaidi, wamejiamini zaidi na wamekuwa na ujasiri zaidi, hata kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano na maandamano ya kudai haki na maendeleo yao, kwa sababu wameguswa na harakati za kizalendo za CHADEMA, chini ya uongozi makini wa Kamanda Mkuu, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe na Katibu Mkuu wetu Mhe. Dk. Willbrod Peter Slaa. Nawapongeza sana, CHADEMA mwendo mdundo, hakuna kulala mpaka kieleweke.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Maliasili na Utalii inalenga kuwa na “Maliasili na Malikale zilizohifadhiwa vizuri, kusimamiwa na kutumika kiendelevu na kuwa na utalii unaowajibika”. Kwa dira hii na utajiri mkubwa wa maliasili na vivutio vya utalii tulivyo navyo, Wizara hii, ilipaswa kuwa mtaji mkubwa wa kuharakisha maendeleo ya nchi hii. Ilipaswa kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali katika kugharamia na kusukuma miradi mingi ya maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, kinyume chake, Watanzania wengi, ndani ya nchi hii, yenye utajiri mkubwa wa misitu na mbuga nyingi za wanyama, milima na mabonde ya kuvutia, pamoja na vivutio vingi vya utalii, wameendelea kuwa maskini hata baada ya miaka 50 ya uhuru wetu. Wizara ya Malisili na Utalii, iliyopaswa kuwa mtaji na chachu ya maendeleo yao, imekuwa ndiyo moja ya wizara dhaifu kabisa kwa ubadhirifu na upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali na maliasili zetu wakiwemo Wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, Rais wa zamani wa Marekani, Theodere Roosevelt, aliwahi kusema, “si kweli kwamba tumeachiwa maliasili tulizonazo na mababu na mabibi zetu…. Ukweli ni kwamba tumeazimishwa maliasili hizi na watoto wetu na vizazi vijavyo”, mwisho wa kunukuu.
Ni kwa bahati mbaya kuwa Viongozi wa Serikali hii wamekuwa wakiishi kama vile wana haki ya kutumia maliasili hizi kadri watakavyo na kwa nguvu zao zote. Kizazi chetu hiki ni waangalizi tu wa mali hizi ambazo ni za watoto wetu na vizazi vijavyo. Kama waangalizi tuna wajibu wa kudai uwajibikaji katika matumizi ya maliasili zilizopo.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani kwa niaba ya Watanzania, inachukua wajibu huu kudai uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za nchi hii; Kwani, kila mwaka, maliasili zetu zimekuwa zikifujwa kwa makusudi na viongozi na watumishi wa Serikali kwa kisingizio cha udhaifu wa kimfumo. Upembuzi wetu kuhusu ripoti na nyaraka za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, umeonyesha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010 pekee, Wizara hii ilifanya ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Kanuni za Fedha, wa jumla ya shilingi bilioni 9.2 na kusababisha taifa lipate hasara ya moja kwa moja ya zaidi ya shilingi bilioni 1. 

Mheshimiwa Spika, katika sehemu ya ubadhirifu huo mkubwa ambao nimeufafanua kwa kirefu sana kwenye Kiambatanisho Na 1cha hotuba hii, Wizara hii kinyume kabisa na Sheria ya Misitu (CAP 323) na Kanuni za misitu za mwaka 2007, ilipunguza tozo ya mrabaha wa mazao ya misitu tena bila kibali cha mamlaka husika ya misitu na kusababisha taifa lipate hasara ya shilingi milioni 874.8;

Wizara hii ililipaposho ya samani kwa watumishi ambao hawakustahiliwanaoishi kwenye nyumba zao binafsi, kinyume na Waraka waUtumishi, na kusababisha taifa lipate hasara ya shilingi milioni 119.3; Na Wizara hii, ililipa mishahara ya watumishi ambao ni wastaafu, waliokufa na walioachaajira, na kusababisha taifa lipoteze kiasi cha takribani shilingi milioni 10.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani viongozi na watendaji wakuu wa wizara hii tuliowapa dhamana ya kuhifadhi na kusimamia fedha na maliasili zetu, wavunje sheria na kanuni, na kusababisha nchi yetu ipate hasara kubwa kiasi hicho, halafu waachwe bila kuwajibishwa. Kwa mfano Wizi huu wa fedha za wananchi, uliopachikwa jina la “mishahara hewa” umekuwa ni mchezo unaofanywa karibu kila mwaka. 

Mheshimiwa Spika, haiwezekani tukaendelea hivi, ni lazima Bunge la kumi lichukue hatua kali zaidi za kuisimamia Serikali kuliko ilivyofanyika huko nyuma, vinginevyo fedha nyingi za taifa hili zitaendelea kufujwa kila mwaka, Watanzania wataendelea kuteseka kwa umaskini kila mwaka, na Serikali itaendelea kulalamika haina pesa kila mwaka, ilhali pesa za maendeleo zipo nyingi, lakini zinaingia kwenye mifuko ya mafisadi. Mtalamu mmoja wa sayansi ya jamii, aliwahi kusema, kwamba; “Uwendawazimu ni kufanya jambo lilelile kwa njia ile ile huku ukitegemea matokeo yawe tofauti”, Watanzania hatutaki kuwa wendawazimu hata kidogo. Ni lazima tuchukue hatua tofauti katika Bunge hili la kumi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwaukiukwaji huu washeria na kanuni za fedha, umekuwa ukifanyika ndani ya wizara hii, na taasisi nyingine za serikali kwa muda mrefu, hata kusababisha nchi yetu ipate hasara kubwa karibu kila mwaka; Kwa kuwa wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wamekuwa wakishauri na kupendekeza hatua mbalimbali kuchukuliwa, lakini bado ufujaji mkubwa wa fedha unaendelea;

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka viongozi na watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii, waliohusika katika kukiuka sheria na kanuni za usimamizi wa fedha za umma na kulisababishia taifa hasara, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kushitakiwa haraka iwezekanavyo, kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi, na kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Vinginevyo Serikali isipochukua hatua, hakutakuwa na njia nyingine sahihi na ya kizalendo, ya kuwanusuru Watanzania na umaskini wao, zaidi ya kutumia nguvu ya umma kushinikiza hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika. 

SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI

Vitalu vya Uwindaji

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo uelewa mdogo kuhusu nini hasa kinafanyika kwenye sekta nzima ya uwindaji wa kitalii, ikiwemo uwekezaji unaofanywa, sheria pamoja na taratibu mbalimbali zinazotawala sekta hiyo. Matokeo ya uelewa huu mdogo ni Watanzania wengi kutobaini fursa na changamoto zilizopo na kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara ambayo pengine si ya lazima sana kujitokeza. Kambi rasmi ya Upinzani, tunamtaka Mhe Waziri wakati wa majumuisho yake alieleze kwa kina Bunge hili, kile kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kifungu 38 (3) – (e), imempa madaraka makubwa Waziri mwenye dhamana katika mchakato mzima wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ikiwemo kuteua wajumbe watano wa kuingia kwenye Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji.Hata hivyo, wakati wa uteuzi wa wajumbe hao, Waziri analazimika kwa mujibu wa sheria kuzingatia vigezo vifuatavyo; jinsia, ujuzi na uzoefu katika masuala ya utawala, na uhifadhi wa mazingira unaohusiana na uwezeshaji wa kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wajumbe walioteuliwa na Mhe.Waziri Ezekiel Maige, kuingia kwenye kamati hiyo, ni pamoja na Bwana Benno Malisa (ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Bwana Daniel Nsanzungwako (ambaye pia ni kada wa CCM). Kambi rasmi ya Upinzani imeshitushwa sana na uteuzi wa wajumbe hawa kuingia kwenye kamati hiyo ya kumshauri Waziri. Watu hawa hawana vigezo vinavyotakiwa, ikiwemo ujuzi na uzoefu kwenye masuala ya utawala, na uhifadhi wa mazingira unaohusiana na uwezeshaji wa kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, mmoja wa wataalam wa masuala ya uongozi, Bwana John Maxwel, aliwahi kusema, “When leaders are incompetent they become destruction to the team, they waste people’s energy, they prevent people from keeping the main thing, the main thing”, mwisho wa kunukuu. Haifai watu wasio na vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, wakapewa nafasi nyeti kama hiyo. Mathalan, Bwana Benno Malisa, anafahamika kitaaluma kuwa ana elimu ya sheria, lakini hata sheria yenyewe hana uzoefu nayo na wala hana uzoefu wowote katika masuala ya utalii na mazingira zaidi ya kujihusisha tu na shughuli za vijana wa CCM.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Waziri amekiuka Sheria ya Wanyamapori na vigezo vyake katika uteuzi huo. Kambi rasmi ya Upinzani inalitaka Bunge hili tukufu kupitia kamati yake husika, ichunguze sababu za Mhe. Waziri wa Maliasili kukiuka sheria katika uteuzi huo ili kujua alifanya hivyo kwa maslahi ya nani. Na kwa kuwa uteuzi huo haukuwa wa wazi, haukufuata misingi ya utawala bora na ulikiuka vigezo vya kisheria, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka Kamati hiyo iliyoundwa na Waziri ivunjwe yote mara moja na kuundwa kamati nyingine.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Wanyamapori kifungu cha 39 (3) –(b), inatamka kuwa asilimia ya kampuni za kigeni zinazopewa vitalu vya uwindaji isizidi asilimia 15 ya idadi ya makampuni yote ya uwindaji. Kambi rasmi ya Upinzani imebaini kuwa kifungu hiki kinapingana na sheria yenyewe. Kwa sheria hii, hakuna kampuni inayomilikiwa na raia wa kigeni kwa asilimia mia moja. Ni lazima kampuni ya utalii imilikiwe angalau kwa asilimia 25 na Watanzania. Waziri atahakikishaje kwamba kampuni ambazo raia wa kigeni wanamiliki hisa nyingi (majority shareholding) hazitapewa vitalu vya uwindaji zaidi ya asilimia 15% ya vitalu? 

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Wanyamapori kifungu cha 12 (e) kinatamka kwamba Waziri anaweza kufuta ugawaji wa kitalu cha uwindaji endapo aliyepewa atakikodisha. Lakini kifungu cha 39 (4) cha Sheria hiyo hiyo ya Wanyamapori kinampa mamlaka Waziri kuandaa Kanuni zitakazoruhusu uhamishaji wa vitalu vya uwindaji kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hapa Kambi ya Upinzani inahoji kuna maana gani ya kuzuia kukodisha kitalu cha uwindaji na wakati huo huo iwepo na sheria ya kuhamisha? Na je Kanuni hizo zimeshapitishwa?

Mheshimiwa Spika, kuna uhakika gani kwamba Kanuni hizo hazitatumika kuruhusu wajanja wachache kuomba na kupewa vitalu kwa lengo la kuviuza kwa bei ya juu mara baada ya kupewa kwa kisingizio cha uzalendo? Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba muombaji yeyote atakayepewa kitalu cha uwindaji asiruhusiwe kuhamisha umiliki wake mpaka baada ya kumalizika kwa miaka miwili, tangu kupewa kitalu hicho. Na endapo atakuwa ameshindwa kukiendeleza kitalu au kufanya biashara basi kitalu hicho kitangazwe kuwa wazi na uwekwe utaratibu wa mtu yeyote kukiomba upya.

Mheshimiwa Spika, pia Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua kwanini Kanuni za ugawaji wa vitalu vya uwindaji imekuwa ni siri ya Wizara husika. Si kwa wananchi tu, bali hata Bunge hili pamoja na kamati yake ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, halizijui kanuni hizo. Usiri huu unatoa mwanya wa vitalu hivyo kugawiwa kwa upendeleo na pengine rushwa kupenyezwa. 

Mheshimiwa Spika, kifungu namba 15 (a) kuhusu “Mgawanyo wa mapato yatokanayo na utalii wa picha katika maeneo yaliyo nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba, kinatamka kuwa asilimia 20 ya mapato italipwa kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, asilimia 15 kwa Halmashauri za wilaya, na asilimia 65 zitarudishwa katika Serikali za Vijiji ambazo uwekezaji unafanyika. 

Mheshimiwa Spika, pamoja na vifungu hivyo vizuri, tumebaini kuwa mgawanyo wa mapato hayo umekuwa haufanyiki kama inavyotakiwa. Na matokeo yake mapato ya utalii wa picha kwa kijiji cha Robanda Wilaya ya Serengeti yameripotiwa kushuka kutoka milioni 300, mwaka 2008/2009 hadi kufikia milioni 200 mwaka 2009/2010. 

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na upotevu huu mkubwa wa mapato ya wananchi, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa vijiji vilivyo tenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji vipewe uwezo wa kuendelea kukusanya mapato ya Vitanda (Bed fee) na yale yanayohusu matumizi ya ardhi (concession fee) kwa kuingia mikataba na kukusanya mapato hayo moja kwa moja kutoka kwa wawekezaji wake.

Ujangili

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Septemba, mwaka 1961,Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliuhakikishia ulimwengu kwamba Serikali ya Tanganyika (ambayo sasa ni Tanzania) itahakikisha wanyamapori hawataangamia kama ambavyo Serikali itahakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wataishi. Leo miaka takribani 50 tangu Baba wa Taifa atangaze dhamira hiyo njema, tunashuhudia wanyama pori wetu wengi tena wenye thamani kubwa kiuchumi wakiuwawa na majangili kila kukicha.

Mheshimiwa Spika, taarifa za mwezi Oktoba 2010 hadi Machi, 2011, zinaonyesha kuwa Tembo 55 waliuwawa na majangili kwenye mbuga mbalimbali kama, Katavi (tembo 7), Kilimanjaro (3), Lake Manyara (4), Mikumi (4), Mkomazi (1), Ruaha (4), Serengeti (17), Tarangire (10) na Udzungwa(1). Hii ni hali ya hatari sana na hasa ikizingatiwa kuwa wanyama hao wengi, wameuwawa ndani ya kipindi cha miezi sita tu, na kwa mantiki hiyo hali hii ikiiachwa, kwa mwaka wanaweza kuuwawa jumla ya Tembo 110 na kwa miaka 5 Tembo550 watakufa .

Mheshimiwa Spika, hii inaonyesha kuwa upo uwezekano mkubwa wa kupoteza maliasili yote ya Wanyamapori mikononi mwetu kabla hatujairithisha kwa vizazi vijavyo. Hii ni kwa sababu tu watendaji waliopewa dhamana ya kuhifadhi maliasili zetu, wamekuwa wabinafsi na hawawajibiki ipasavyo, huku Serikali iliyopewa jukumu la kuwawajibisha, ikiwaacha bila kuwachukulia hatua madhubuti. 

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, inahoji, je huku ndiko kuthubutu, kuweza, na kusonga mbele kunakohamasishwa? Tunaitaka Serikali ijieleze imechukua hatua gani madhubuti mpaka sasa, kukabiliana na wimbi hili la ujangili?

Wizi wa Wanyamapori

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu na za kisheria aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, kwa uzembe na/au kwa kufanikisha wizi wa wanyamapori hai 130, wakiwemo Twiga, uliofanyika Novemba 26 mwaka jana (2010). 

Mheshimiwa Spika, moja ya majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, yaliyoainishwa katika ukurasa wa tatu wa randama ya Wizara husika iliyotolewa hivi karibuni, ni “...Kulinda raslimali za maliasili (ikiwemo Wanyamapori walioibwa) na malikale dhidi ya matumizi haramu na kuhakikisha utoaji bora wa huduma za utalii”Kwa hiyo, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka viongozi na watumishi hawa wa umma wawajibishwe kwa sababu ya kuzembea wajibu wao au/na kufanikisha wizi huo.

Pia Serikali iwawajibishe wakuu na watendaji wote wa vyombo vya usalama waliopewa dhamana ya moja kwa moja ya kulinda maliasili zetu. Na tunaitaka Serikali ilieleze Bunge hili wanyama wetu hao wako wapi mpaka sasa?

Mheshimiwa Spika, badala ya kuchukuliwa hatua, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii, mapema mwaka huu alihamishwa na kuelezwa kuwa amepelekwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kupangiwa kazi maalum. Pia, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakati wizi huo unafanyika, badala ya kuchukuliwa hatua, Februari mwaka huu alipewa likizo mpaka atakapostaafu kwa mujibu wa sheria.
Kwa namna yoyote ile maamuzi ya kuhamishwa kwa viongozi hao, yanatoa picha mbaya kuwa Serikali yetu inaendeleza utamaduni wa kulindana badala ya kuwajibishana.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani wanyamapori hai 130 wakiwemo Twiga, wanyama wakubwa kabisa, waibwe, wasafirishwe kutoka mbugani hadi uwanja wa ndege wa KIA, wapakiwe kwenye Ndege ya Qatar, na hatimaye watoroshwe nje ya nchi, halafu viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Idara zake wasijue – haiwezekani. Watanzania sio wajinga hadi waibiwe hivyo, tutawaongoza kudai utajiri wao ikiwa hatua dhidi ya watuhumiwa hawa wakubwa hazitachukuliwa. 

Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa kwa taifa. Tunalitaka Bunge lako tukufu lihakikishe watuhumiwa hawa wakubwa na wengine wote wanaohusika wanawajibishwa haraka iwezekanavyo. Ni lazima tujenge taifa la viongozi wanaowajibika na wanaowajibishwa pindi wanapofanya uhalifu na pindi uhalifu unapofanyika chini ya na ndani ya mamlaka yao. Vinginevyo, Watanzania wataendelea kuwa maskini daima, kwani maliasili na kodi zao zitaendelea kuibwa na kufujwa kila mwaka

SEKTA NDOGO YA UTALII

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya Wizara hii, iliyotolewa hivi karibuni, mchango wa Sekta ya Utalii katika Pato la Taifa umekadiriwa kuwa ni asilimia 17.2. Serikali imeeleza kuwa mchango huu umetokana na shughuli za utalii katika sekta ndogo za Wanyamapori, Hoteli, Usafirishaji, Mambo ya Kale, Mawasiliano, Biashara, Michezo na kwamba unachangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani hairidhishwi na kiwango hiki cha ukuaji wa Sekta ya Utalii wala mchango wake katika Pato la Taifa, kwani mapato mengi ya utalii yanapotea kila mwaka kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa na miundombinu duni ya usafiri, kutosimamiwa kikamilifu kwa sheria za utalii hapa nchini, ufisadi na zaidi ni kutokuwepo kwa mikakati na mipango madhubuti ya kuboresha sekta hii kwa ujumla wake. 

Mheshimiwa Spika, tafiti zinaonesha kuwa nchi zenye Shirika la ndege la umma, asilimia 70 ya mapato yanayotokana na utalii hubakia ndani ya nchi husika, ilhali kwa nchi ambazo hazina National Carriers, ni asilimia 30 tu ya mapato yanayotokana na Utalii ndiyo hubakia katika nchi hizo. Ndio maana nchi kama Kenya inapata watalii zaidi na mapato ya Utalii hubakia nchini humo kwa kiwango kikubwa. Wakati Serikali hii ikijivunia takwimu zake za ukuaji wa sekta ya utalii, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa nitheluthi moja tu ya mapato yanayotokana na Utalii ndiyo hubakia nchini, kwa sababu Shirika letu la Ndege limekufa.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza maradufumapato yatokanayo na utalii na hivyo kuchochea ukuaji mkubwa na wa haraka wa uchumi, Kambi rasmi ya Upinzani tunaendelea kusisitiza ushauri wetu wa kuitaka Serikali ishirikiane na mashirika ya Umma yenye kuendesha shughuli za uhifadhi, katika kumiliki Shirika la Ndege, kuanzia katika mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu huu tunaoupendekeza, sehemu ya mtaji ishikwe na Serikali na itakapofika Shirika kuanza kupata faida wananchi wauziwe sehemu ya hisa za Shirika. Uwekezaji kutoka nje sio mwarobaini wa matatizo yetu yote. Tunaweza kutumia mitaji ya ndani kimkakati ili kuimarisha Shirika la Ndege. Jambo la msingi ni serikali kusafisha vitabu vya Shirika kwa kuchukua madeni yote na kuingiza uwekezaji kutoka mashirika ya umma ya ndani ya nchi.

Aidha, Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzaniinaitaka Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, iharakishe upanuzi na uboreshaji wa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa kuufanya kuwa wa kisasa na wa kimataifa zaidi, ili kukabiliana na changamoto ya ushindani wa kitalii, baina yetu na Kenya, ambayo taarifa zisizo rasmi zinasema imeamua kujenga uwanja wa ndege mpakani eneo la TAVETA, takribani kilometa 7 tu kutoka uwanja wetu wa KIA.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mikoa ya nyanda za juu kusini na magharibi iko nyuma kwa muda mrefu katika maendeleo ya sekta ya utalii, Kambi rasmi ya Upinzani, pamoja na mambo mengine, tunaishauri Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi, kwa pamoja waharakishe ujenzi wa barabara zinazounganisha maeneo yenye vivutio vya utalii kwenye mikoa hiyo, hususan barabara ya kutoka Iringa Mjini mpaka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwa kiwango cha lami na kuboresha uwanja wa ndege wa Nduli.

Pia Mheshimiwa Spika, wakati umefika sasa kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na ile ya magharibi, kusogezewa chuo cha utalii ili kiweze kuzalisha wataalam wa kutumikia sekta hiyo moja kwa moja kwenye mikoa hiyo, kama ilivyo kwa mikoa ya kanda ya kaskazini. 

SHIRIKA LA HIFADHI YA TAIFA (TANAPA)

Viwango vya Malipo ya Concession Fees



Mheshimiwa Spika, kumekuwepo upotevu mkubwa wa Mapato ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kupitia viwango vidogo vya concession fees zinazolipwa na wamiliki wa hoteli za kitalii zilizopo hifadhini. Mapato ya concession fees yamekuwa ni kidogo sana kulinganisha na yale yanayotokana na upigaji mahema (camping) ambapo mtu mmoja hulipa takribani dola 50 za Kimarekani kwa siku, wakati concession fees ni wastani wa dola 8 mpaka dola 10 za kimarekani kwa mtu mmoja kwa siku. 



Mheshimiwa Spika, hali hii ilisababisha TANAPA kupoteza mapato ya shilingi bilioni 19 kwa mwaka wa fedha 2008/2009 na kuambulia mapato ya shilingi bilioni 2.4 tu. Na hasara hii ilitokana na hatua ya Waziri aliyepita kwenda kinyume na mapendekezo ya TANAPA ambayo ilitaka viwango vya concession fees vitozwe kwa kuzingatia fixed rate kwa hoteli zote ili kudhibiti upotevu wa mapato. Na hapa Kambi ya Upinzani inahoji, je Serikali hii ilichukua hatua gani dhidi ya Waziri aliyepita wa kwa kuisababisha nchi hasara kubwa kiasi hicho?



Mheshimiwa Spika, kutokana na hasara hiyo iliyosababishwa na Waziri aliyepita, Kamati ya Bunge hili ya Hesabu za Mashirika ya Umma, iliagiza viwango vya concession fees vilivyokuwa vimependekezwa na TANAPA virejeshwe na kwa hiyo concession fees ikaagizwa kuwa dola 40 za kimarekani kutoka dola 10 za kimarekani kwa mtu kwa siku. Hata hivyo, uamuzi huo ulipingwa vikali na makampuni yanayofanya kazi za watalii na hata kupelekea kuweka zuio mahakamani ambalo liliamuliwa tarehe 09/08/2011, kuwa makampuni hayo yanapaswa kwanza kutangaza kwenye magazeti kuhusu kusudio la pingamizi lao ndani ya siku 30 tangu siku ya uamuzi huo.



Mheshimiwa Spika, baada ya agizo hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ezekiel Maige aliandika barua yenye kumb. AB 315/484/01 ya tarehe 02/08/2011 ambapo aliondoa agizo la awali la kuwataka waendesha biashara wa utalii kulipa wakati wanapokuwa wanaingia na badala yake makampuni haya yaandikiwe invoice. 



Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inahoji, je uamuzi huo wa Mheshimiwa Waziri Maige wa kutaka mahoteli ya kitalii yaandikiwe invoice badala ya kulipa concession fees moja kwa moja, aliutoa kwa maslahi ya nani, ikiwa hata kesi ya msingi ya pingamizi hilo bado haijatolewa hukumu?



Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inataka Mhe. Waziri wakati wa majumuisho yake ajieleze kwa uwazi wote, ni kwanini amefanya hivyo. Na pia tunaitaka Serikali mara moja ianze kutoza concession fees kwa mahoteli hayo ya kitalii kwa kiwango cha dola 40 za Kimarekani kwa mtu mmoja kwa siku. 



Mheshimiwa Spika, madai kuwa punguzo la viwango vya concession fees lina nia njema ya kuhamasisha upatikanaji wa Watalii wengi kama nchini nyingine, hayana msingi, kwani duniani kote mbuga ya Serengeti, Ngorongoro, na Mlima wa Kilimanjaro, havipatikani popote isipokuwa nchini Tanzania tu. 



Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani imepata taarifa za uhakika na za kushtusha kuhusu matumizi makubwa ya fedha za umma yanayofanywa na TANAPA, kulinganisha na kile inachoingiza. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2008/2009 gharama za uendeshaji za TANAPA zilikuwa shilingi bilioni 66.0 wakati shirika lilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 70.4.Na katika kipindi hicho TANAPA ilitumia shilingi bilioni 3 tu kwa ajili ya kusaidia jamii. Mwenendo mzima wa mapato ya TANAPA umo katika Kiambatanisha Na. 2 cha hotuba hii.


Mheshimiwa Spika, kwa hali hii,ni dhahiri kuwa mapato mengi ya TANAPA yanaishia kwenye kugharamia zaidi utawala wake kuliko kuingia Serikalini na kusaidia jamii. Kwa hiyo, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha inadhibiti matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya fedha za umma yanayofanywa TANAPA. 



Kashfa ya Jengo la TANAPA

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa Serikali imeliamuru shirika la TANAPA kuhama mara moja kutoka kwenye jengo lao la makao makuu ya hifadhi za taifa liitwalo Mwalimu J.K Nyerere Conservation Centre ambalo ni mali ya TANAPA. Hatua hiyo imekuja kutokana na Mahakama ya Afrika kumwomba Mhe. Rais Kikwete awapatie jengo hilo, licha ya kuwa lilijengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za TANAPA.



Mheshimiwa Spika, ni vema ikakumbukwa kuwa huko nyuma, TANAPA walijenga jengo lao la kitega uchumi (commercial wing) mkabala na makao makuu, ambalo Mahakama hiyo ya Afrika walipangishwa, lakini leo taarifa tulizonazo ni kwamba wamepewa jengo hilo kwa nguvu na Rais, na TANAPA wametakiwa kutafuta sehemu nyingine ya kupanga kwa ajili ya ofisi.



Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani imesikitishwa sana na taarifa hizi, na zinaonyesha kuwa Serikali yetu ipo tayari kuyapokonya mashirika yetu vitega uchumi vyake, kwa sababu tu ya kuzibeba taasisi za nje. Kuna msemo wa Kiingereza usemao“if you dont know where you are going, then any road will take you there”, “kama hujui unakokwenda, basi unaweza kuchukuliwa na njia yoyote”. Taarifa za Serikali kutaka kuipokonya TANAPA jengo lake, inadhihirisha kuwa Serikali yetu haijui inakokwenda, kwani jengo hilo halikujengwa kwa ajili ya mahakama ya Afrika, bali lilijengwa kwa ajili ya TANAPA kwa malengo ya TANAPA. 



Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inataka uamuzi huo usitishwe mara moja, na TANAPA waendelee kubaki na jengo lao.

Kashfa ya Ukwepaji Kodi

Mheshimiwa Spika, TANAPA inamgogoro katika Hifadhi ya Arusha unaohusisha eneo la Mashamba namba 40 na 41 ambayo ni mali ya Shirika hilo. Katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 996 kuna mali mbalimbali yakiwemo majengo ya hoteli ijulikanayo kama Momella Wildlife Lodge inayoendeshwa na kampuni ya Lions Safari International (LSI).


Mheshimiwa Spika, TANAPA ilinunua eneo hilo pamoja na mali zote zilizokuwemo mnamo mwaka 1988 kutoka Serikalini na hivyo kumfanya mwendeshaji wa hoteli hiyo kuwa mpangaji wa Shirika, na kwa hiyo Mwekezaji alipaswa kulipia pango hilo. Hata hivyo, hoteli hiyo haijawahi kulipia pango, ambapo hadi kufikia tarehe 31 Desemba 1998 ilipaswa kulipa jumla ya shilingi bilioni 1.4, na baada ya hapo kuanzia tarehe 01 Januari 1999ilipaswa kuanza kulipakiasi cha shilingi milioni 149.3 kwa mwaka, lakini kodi zote hizo hazikulipwa.


Mheshimiwa Spika, piahoteli ya kitalii ya Bilila iliyopo Serengeti tangu kuanzishwa kwake, imekuwa hailipi tozo za malazi tangu ilipojengwa mpaka sasa kutokana na Serikali kuisamehe kulipa tozo hizo.Na kwa kipindi cha miezi sita iliyopita hata baada ya kumaliza muda wa msamaha iliokuwa imepewa (yaani grace period), bado imeendelea kutolipa tozo hizi ambazo hoteli nyingine zinalipa.


Mheshimiwa Spika, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema, kuwa, Serikali isiyoweza kukusanya kodi ni Serikali iliyonunuliwa na wenye mali, ni Serikali iliyowekwa mfukoni na wenye mali”. Hatua ya Wawekezaji wote hawa kutolipa kodi kwa kipindi chote hicho, inatoa picha mbaya kuwa Wawekezaji hawa bila shaka wana nguvu kubwa inayoifanya Serikali ilainike na kushindwa kukusanya kodi kutoka kwao. Kambi rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri wakati wa majumuisho yake alieleze Bunge hili ni kwanini kwa kipindi chote hicho, Wawekezaji hao wa hoteli wamekaidi kulipa kodi wakati Serikali ipo.


Mkataba wa “Group Endowment Scheme Assuarance”

Mheshimiwa Spika, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania linao mfuko maalum wa kuwasaidia wafanyakazi wake wanapostaafu au kufariki kabla ya kustaafu, ambao unasimamiwa na African Life Assurance (T) Ltd. Mfuko huo unajulikana kama Group Endowement Assurance Scheme (GEAS). Uamuzi wa kuanzisha Mfuko huo ulitolewa tarehe 17-Agosti-2007 na madhumuni yake ni kutoa nyongeza kwa mafao yatolewayo na NSSF/PPF ambayo ni madogo.


Mheshimiwa Spika, Mfuko huu ulikuwa unatoa mafao ya mishahara ya miezi 24 kwa mfanyakazi aliyestaafu kazi kwa umri wa miaka 55 (kwa hiari) au miaka 60 (kwa lazima) na pia akifariki akiwa kazini. Utaratibu huu uliendelea hivyo hadi tarehe 30 June 2010, lakini kuanzia Julai 2010, mafao hayo yalipitiwa upya na kuboreshwa kwa kuwalipa malipo ya mishahara ya miezi 48. Katika kupitia upya, mkataba huo uligawanywa na kuwa mikataba miwili inayojitegemea, ambayo ni (i) Group Endowement Fund - GEF (mfuko kwa ajili ya wastaafu) na (ii) Group Life Assurance Policy - GLA (ambayo ni bima kwa ajili ya vifo).


Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, inashauri kuwa Shirika liachane na huduma ya “Group Life Assurance” ambayo ni Bima kwani wamekuwa wakilipa kiwango cha “premium” ambacho ni kikubwa kwa mwaka lakini idadi ya vifo vya watumishi ni ndogo na pia jumla ya kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kinalipwa kwa warithi wa watumishi waliofariki kwa mwaka kama mafao ni kidogo sana.

Uchimbaji Madini katika Hifadhi

Mheshimiwa Spika, Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini, tayari imeshaanza mchakato wa kuchimba madini ya Uranium ndani ya eneo la hifadhi ya taifa ya Selous kwa kuishirikisha UNESCO, kinyume cha Sheria na bila kulishirikisha Bunge. Hi si tu dharau kwa Bunge, bali pia ni dharau kwa Watanzania wote waliotutuma kuwawakilisha. Tunaitaka Serikali iwaombe radhi Watanzania na kurudi kwanza Bungeni kuomba ridhaa, ili sote tujiridhishe kama kweli kuna maslahi ya taifa kwa uchimbaji huo kuingilia hifadhi.


Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro

Mheshimiwa Spika, pamoja na matatizo mengine mengi, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, inakabiliwa na tatizo la kuwa na Mwenyekiti wa Bodi anayevuka mipaka ya majukumu yake. Tuna ushahidi kuwa, Mhe. Pius Msekwa (Makamu Mwenyekiti wa CCM), ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, amegeuka kuwa Mwenyekiti Mtendaji anayefanya kazi ya kutoa offer kwa Wafanyabiashara wenye mahitaji ya kujenga hoteli za kitalii, huku akiwaelekeza maeneo hayo, kazi ambazo si zake. 



Mheshimiwa Spika, huu ni mgongano mkubwa sana wa kimaslahi, na wenye madhara makubwa sana kwa hifadhi hii. Haiwezekani Mwenyekiti wa Bodi ya Ngorongoro, ambaye moja ya majukumu yake ni kukagua hali halisi ya hifadhi hiyo, ajiingize pia katika shughuli za utendaji tena zilizo nyeti kama hizo. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya Mwenyekiti huyu wa bodi mara moja kwa kukiuka mipaka ya majukumu yake. Na tunaahidi kuwa tupo tayari kuipa Serikali ushirikiano kuhusiana na tuhuma hizi.



Upanuzi wa Hifadhi na fidia kwa wananchi 

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina Hifadhi za Taifa, Mapori Tengefu na Mapori ya Akiba takribani 100. Nyingi ya hifadhi hizo zimeanzishwa kwa baada ya kuwahamisha wananchi waliokuwa wakiishi maeneo hayo kabla ya kufanywa hifadhi, mara nyingi bila malipo yoyote kwa wananchi hao. Aidha, Serikali imekuwa ikilalamikiwa kupanua maeneo haya kwa kumega ardhi za vijiji kwa visingizio vya kuepusha uharibifu wa mazingira – tena bila kuwalipa wahanga hawa.


Mheshimiwa Spika, mathalan, ili kupisha mipango ya kupanua ukubwa wa Hifadhi ya Taifa Ruaha kutoka kilomita za mraba 10,300 hadi 20,226, Serikali iliwafukuza wafugaji wa Mbarali mkoani Mbeya (Walsh, 2007:11).Pia, baada ya upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Manyara, uliotangazwa na Gazeti la Serikali No. 105 la Mei 2009, wakai wa Kijiji cha Moyo Mayoka Wilayani Babati, waliachwa wakilalamikia kuonewa na Serikali kwa hatua ya kulifanya Ziwa Manyara lote kuwa ndani ya hifadhi hivyo kuwakosesha maelefu ya wavuvi wa samaki katika ziwa hilo chanzo kikuu cha kipato.


Mheshimiwa Spika, pamoja na kuweka mazingira mazuri katika hifadhi hizini vema ikazingatiwa hatma ya yote ni kuwe na ustawi wa jamii. “We cannot preserve nature, at the expense of human life”. Hatuwezi kuhifadhi mazingira, kwa gharama ya kupoteza uhai wa mwanadamu”. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwafidie wananchi wote waliopoteza ardhi, mifugo yao, na vyanzo vyao vya mapato kwa visingizio vya utunzaji mazingira. Na tunaitaka Serikali ije utaratibu mbadala wa kuhakikisha inawianisha haja ya usalama wa maliasili na haja ya usalama wa binadamu kwa pamoja. 



Usimamizi wa Sheria na Taratibu za Utalii

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 58 kifungu kidogo cha (1) na (2), cha Sheria ya Utalii ya mwaka 2007, kwa ujumla wake vinaelekeza kwamba shughuli za uwakala wa kusafirisha watalii na kuongoza watalii mlimani zifanywe na Watanzania tu. Pia, kifungu cha 3 cha Sheria ya TANAPA ya mwaka 2003, kinaielekeza TANAPA kushughulika tu na Wakala wa Utalii aliyeandikishwa na mwenye leseni (za TALA) na ambaye ni mwanachama wa chama kinachoshughulika na masuala ya utalii. 



Mheshimiwa Spika, pamoja na vifungu hivi vizuri vilivyopitishwa na Bunge hili kwa busara ya kumjali Mtanzania mzawa, Kambi rasmi ya Upinzani imebaini kuwa bado Watanzania wengi hawafaidiki vya kutosha, kwa sababu sheria hizisimamiwi vizuri. Mathalan, kinyume kabisa na kifungu hicho, kampuni nyingi za kigeni zinafunguliwa hapa nchini kwa mbinu ya ubia kati ya wageni na wazawa wakati wenye kampuni hizo wanakuwa ni wageni, na hivyo wageni wanapata mwanya wa kufanya biashara ya mlimani na faida kubwa inabaki nje badala ya kubaki kwa Watanzania wazawa.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji, je serikali imechukua hatua gani kuhakikisha Sheria ya Utalii ya mwaka 2007 inasimamiwa kwa manufaa ya Watanzania wazawa, ikiwa kampuni za wageni zilizokuwa zikifanya uwakala wa safari za mlimani bado zinaendelea kufanya kazi hiyo, licha ya sheria kutaka ifanywe na wazawa pekee? Na je, serikali imechukua hatua gani dhidi ya kampuni za kigeni zinazotumia mbinu ya kuingia ubia na wazawa kufanya biashara ya utalii ya kupeleka watalii mlimani, ikiwa faida kubwa iliyopaswa kuwa ya Wazawa (kwa busara ya sheria) inaishia kwa wageni?


SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi yatokanayo na biashara ya uvunaji magogo, kwa sababu ya kuwepo udhaifu katika usimamizi wa sheria zilizopo. Maelekezo yanayotolewa yamekuwa hayazingatiwi. Mathalan, katika msitu wa Sao Hill uliopo wilayani Mufindi mkoani Iringa, kampuni ya Mufindi Paper Mills tangu mwaka 2007, imekuwa ikiuziwa mita moja ya ujazo wa miti kwa shilingi 10,000 – ilhali beiiliyoelekezwa na Serikali ni shilingi 29,000 kwa mita moja ya ujazo wa miti.



Mheshimiwa Spika, wakati hali ikiwa hivyo, gharama za kutunza mita moja ya ujazo wa miti kwa miaka 25 ni shilingi 18,000. Na wakati huo huo Wawekezaji wengine wakiwamo wananchi wanauziwa mita moja ya ujazo wa miti kwa shilingi 29,000/ na si shilingi 10,000, kama inavyouziwa kampuni hiyo. Kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 kampuni hiyo ilikuwa ikiuziwa kwa bei sawa na kampuni nyingine, lakini ilipofika mwaka 2007, kampuni hiyo ilianza kuuziwa shilingi 10,000 kwa mita moja ya ujazo wa miti.



Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, Kambi rasmi ya Upinzani imebaini kuwa Serikali imeshapoteza mapato ya takribani shilingi bilioni 22 hadi sasa. Wawekezaji wa ndani wanazidi kupoteza imani kwa Serikali kutokana na kutokuwepo kwa usawa katika uwekezaji kwenye msitu wa Sao Hill, jambo linaloashiria uwepo wa harufu ya rushwa.



Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kuona Bajeti za Wizara mbalimbali, kama Wizara ya Uchukuzi zikipitishwa, huku zikiwa na fedha kidogo za maendeleo, wakati fedha nyingi zinapotea bure. Kambi rasmi ya Upinzani inalitaka Bunge hili kupitia Kamati zake za kifedha, ichunguze sababu za kampuni ya Mufindi Paper Mills kupewa fursa ya kuvuna hekta 300,000 kila mwaka katika msitu wa Sao Hill kwa bei ya shilingi 10,000, ambayo ni chini ya bei inayotakiwa.



Mheshimiwa Spika, pia badala ya kuanzisha Mamlaka ya Misitu Tanzania, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa sheria ya misitu Na 14, ya mwaka 2002, isimamiwe kikamilifu kwa kuwa inakidhi mahitaji ya uhifadhi endelevu kwa manufaa ya taifa.



Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, John Maxwell “Kila kitu kinasimama au kuanguka kutegemeana na kiongozi aliyepo”. Taifa letu lipo katika umaskini wa kutisha katikati ya msitu mkubwa wa raslimali. Taifa letu linaanguka kwa sababu ya uongozi uliopo. Bunge la Kumi ndilo tumaini pekee la kunusuru taifa hili. Bunge la Kumi lina hiyari ya kusuka au kunyoa, kwa pamoja tutimize wajibu wetu kuiwajibisha Serikali.



Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, nawashukuru wote walioniwezesha kuwasilisha maoni haya. Mimi ni jumla ya yale yote niliyofunzwa kutoka kwa wale walionifundisha, Wakubwa kwa Wadogo. Nawashukuru Marehemu wazazi wangu, Baba yangu Mchungaji Simon Msigwa na Mama Atu Nsyenge, kwa malezi, hekima na busara walizoniachia.



Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

Mchungaji Peter Simon Msigwa (Mb).
                                       Waziri kivuli wizara ya maliasili na utalii.


17/08/2011
Kiambatanisho Na 1. Uchambuzi wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010, kwa hesabu za Wizara ya Maliasili na Utalii, umebaini kufanyika kwa ufisadi na ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za usimamizi wa fedha za umma wa jumla ya shilingi bilioni 9.2, kama ifuatavyo;Wizara ilifanya upendeleo kwa kutoa kiwango cha chini cha mrabaha wa mazao ya misitu kuliko kiwango cha sheria ya misitu (CAP 323) na Kanuni za misitu za mwaka 2007, bila kibali cha mamlaka husika.Hivyo, ilisababisha nchi yetu kupoteza kiasi cha shilingi milioni 874,853,564. 
Wizara ililipaposho ya samani kwa watumishi ambao hawakustahiliwanaoishi kwenye nyumba zao binafsi kinyume na waraka waUtumishi namba C/AC/134/213/01/G/69 wa tarehe30 Januari 2006na hivyo ilisababisha nchi yetu ipoteze kiasi chashilingimilioni 119,373, 094.66Wizara ililipa mishahara ya watumishi ambao ni wastaafu, waliokufa na walioachaajira, na kusababisha nchi yetu ipoteze kiasi cha shilingi milioni 10,052,511.80.Wizara ililipa malipo yenye nyaraka pungufu ya jumla ya shilingi milioni 165,448,602.00.Wizara ilikutwa na madeni yasiyotarajiwa na ambayo chanzo chake hakikuonyeshwa ya jumla ya shilingi bilioni1,608,732,000.Wizara ilikutwa na madai ambayo hayajashughulikiwa ya kiasi cha shilingi milioni 663,541,372.75,
  ikijumuisha madai ya wazabuni na watumishi wake.Wizara ilizidisha matumizi yake kwa jumla ya shilingi milioni 65,601,951.09.Wizara haikuweza kuonyesha viambatanisho vya madai ya kiasi cha shilingi milioni 207,246,498 na hivyo kusababisha kutothibitishwa kwa uhalali wa madai hayo.Wizara haikuwasilisha nyaraka za mapokezi ya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 1,667,139,734.64 na hivyo kukwamisha ukaguzi. 
Shamba la miti Sao Hill lililo chini ya wizara hii, lilitoa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 53,815,000 kwa Idara na Taasisi nyingine bila ruhusa ya Mlipaji Mkuu.Wizara ilikutwa na tofauti ya shilingi milioni 755, 874,245.67 kati ya kiasi kilichoko kwenye taarifa ya maduhuli na kwenye daftari la kukusanya maduhuli.Wizara kinyume na taratibu za kihasibu ilishindwa kubainisha vyanzo vya makusanyo ya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 2,920,879,363.60. 
Wizara ilishindwa kutoa maelezo na uthibitisho kuhusu tofauti ya makusanyo ya mrabaha wa mazao ya misitu ya shilingi milioni 242,735,027.Wizara haikuonyesha misaada ya fedha kutoka nje ya nchiiliyopokelewa kwa mwaka kwenye Mfuko wa Mambo yaKale.Wizara haikuonyesha mali zote zilizopo katika vituo vya urithi wa utamaduni na mambo ya kale ya kihistoria, ambavyo viko chini yake. 
 Kiambatanisho Na 2.Mapato ya TANAPA kwa miaka 10.












YEARTOTAL REVENUECONCESSION FEES

TSHSTSHS
2000/200116,440,966,421.00348,772,051.00
2001/200217,812,588,831.00383,669,145.00
2002/200323,175,280,370.00392,792,993.00
2003/200425,648,039,359.00706,374,182.00
2004/200533,222,383,950.00949,946,313.00
2005/200644,762,528,972.001,210,526,243.00
2006/200769,059,501,937.001,769,511,217.00
2007/200871,879,146,099.001,527,935,437.00
2008/200970,370,064,590.002,477,791,186.00

No comments:

Post a Comment