Thursday, 27 January 2011

TAARIFA KWA UMMA

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU HAIHUSIKI NA MIGOMO YA HIVI KARIBUNI KATIKA VYUO VYA ELIMU YA JUU

1.0 UTANGULIZI

Katika kipindi cha hivi karibuni pamekuwepo migomo ya wanafunzi katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu inayotokana na madai mbalimbali. Katika hali isiyo ya kawaida migomo yote hiyo imekuwa ikihusishwa moja kwa moja na Bodi, kitu ambacho siyo sahihi hata kidogo.

Matukio hayo yanahusisha wanafunzi wa vyuo vinane vilivyotajwa hapa chini. Wanafunzi wa vyuo vyote vilivyotajwa hawana sababu za msingi za kuinyooshea Bodi kidole kwa kuwa matatizo yao ni kati yao na vyuo wanakosoma, kama ilivyoelezwa hapa chini.

Bodi inachukua nafasi hii kutoa taarifa ya msisitizo ili wanafunzi hao na vyuo husika na Umma kwa ujumla waelewe hali halisi ya matukio yaliyojitokeza, tukianzia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) ambacho mmoja wa Viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wamekitoa kama mfano wakati akitoa tamko la kukurupuka hivi karibuni dhidi ya Bodi, hata bila ya kufanya uchunguzi wa sababu za ndani za migomo ya wanafunzi vyuoni.

2.0 CHUO KIKUU KISHIRIKI CHA ELIMU MKWAWA (MUCE)

Ijumaa, Januari 14, 2011 wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) waligoma wakiwa na madai kadhaa dhidi ya Uongozi wa Chuo chao lakini pia wakidai kutolipwa mikopo kwa ajili ya chakula na malazi kwa robo mwaka ya pili.

Kuhusu mikopo ya Chakula na Malazi ni kwamba, awali, Wanafunzi hao walilipwa kupitia Chuoni fedha za robo mwaka ya kwanza (siku 60) kabla ya tarehe 6 Novemba, 2010 chuo chao kilipofunguliwa. Mara baada ya wanafunzi hao kuripoti chuoni walitakiwa kujisajili na baada ya hapo Chuo kilitakiwa kuwasilisha Bodi, orodha inayoonyesha namba zao za usajili (Registration Numbers) na namba za Akaunti zao za Benki katika muda wa siku 30 ili Bodi iweze kuandaa na kufanya malipo ya robo ya Pili, kupitia akaunti zao. Lakini badala ya kufanya hivyo, katika muda uliopangwa, Chuo chao kilileta majina ya wanafunzi waliosajiliwa na wanaostahili kukopeshwa tarehe 28 Desemba, 2010, yaani uchelewevu wa zaidi ya wiki tatu!

Pamoja na kuchelewa huko, Bodi ilishughulikia haraka malipo hayo na tarehe 7 Januari, 2011, malipo ya jumla ya sh. 241,800,000.00 kwa ajili ya Wanafunzi wapatao 806 yalifanyika na kupitishwa kwenye akaunti za Wanafunzi hao katika benki. Aidha, Bodi ingependa ieleweke kwamba malipo hayo ya robo mwaka ya Pili yalitakiwa yawe yamelipwa kwao mnamo tarehe 6 Januari 2011 (yaani baada ya siku 60 kupita tokea tarehe kufungua Chuo). Hivyo, kulikuwa na uchelewesho wa kama siku moja tu, ambao kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na Uongozi wa Chuo na siyo Bodi.

Wakati mgomo wa wanafunzi hao ukitokea tarehe 14 Januari, 2011 mikopo yao ilikuwa imekwishalipwa kupitia Benki tangu Januari 7, 2011. Hivyo, madai kuwa malipo haya yalifanyika baada ya wanafunzi kugoma si ya kweli na ni uzushi mtupu.

3.0 CHUO KIKUU KISHIRIKI CHA ELIMU DAR ES SALAAM (DUCE)

Jumanne Januari 18, 2011 wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es salaam (DUCE) nao waligoma wakidai malipo ya mikopo kwa ajili ya chakula na malazi kwa robo mwaka ya pili.

Kama ilivyotakiwa kwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Uongozi wa DUCE nao ulitakiwa uwe umewasilisha Bodi, orodha ya wanafunzi waliosajiliwa na namba za akaunti zao za benki kabla ya tarehe 6 Desemba, 2010 ili Bodi nayo iweze kuandaa malipo ya robo mwaka ya pili kwa wakati.

Lakini, orodha ya wanafunzi waliosajiliwa na wanaostahili mikopo iliwasilishwa na Chuo chao tarehe 6 Januari, 2011, yaani uchelewesho wa mwezi mzima. Pamoja na uchelewesho huo, Bodi iliandaa malipo hayo na tarehe 11 Januari, 2011, malipo ya jumla ya shilingi 337,800,000.00 yalifanyika kupitia hundi nambari 961240 kwenda kwenye akaunti ya Chuo chao kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 1,126. Tofauti na ilivyokuwa kwa MUCE, malipo hayo ya DUCE ilibidi yapitie kwenye akaunti ya chuo kwa sababu Chuo hicho kilileta orodha ambayo haionyeshi Namba za Akaunti za wanafunzi. Hivyo, uchelewesho wa mikopo ya wanafunzi hao ulisababishwa na Chuo chao na siyo Bodi ya Mikopo.

Wakati Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) wanatangaza kugoma tarehe 18 Januari, 2011, Bodi ya Mikopo ilikuwa imekwishafanya malipo ya mikopo hiyo kupitia Chuoni tangu Januari 11, 2011. Hivyo, siyo kweli kwamba walilipwa baada ya kugoma.

4.0 CHUO CHA UHASIBU ARUSHA (IAA)

Mnamo Ijumaa, Desemba 10, 2010, wanafunzi wapatao 26 wa chuo hicho walifika kwenye Ofisi Bodi wakiwa na masuala yafuatayo;

4.1 Wanafunzi wanaoendelea na masomo kutopewa mikopo.

Uchunguzi uliofanywa juu ya madai hayo ulibaini kuwa wanafunzi husika matokeo yao ya mitihani yalikuwa hayajawasilishwa kwenye Bodi kama utaratibu unavyotaka.

Msimamo wa Bodi ni kwamba kama sheria Na. 9 ya Bodi inavyotamka, Bodi haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao Bodi haijapokea matokeo yao ya mitihani ya mwaka wa masomo uliopita. Hivyo, wanafunzi husika walishauriwa kufuatilia na chuo chao ili chuo kilete kwanza matokeo hayo Bodi na hivyo mchakato wa upangaji mikopo uendelee. Walifanya hivyo na baadaye Bodi iliachia malipo ya mikopo yao.

4.2 Majina ya baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoonekana kwenye orodha ya wanafunzi wanaopata mikopo.

Uchunguzi uliofanywa juu ya madai hayo ulibaini kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa hawakujaza fomu na wale waliokuwa wamejaza fomu, fomu hizo zilikosa baadhi ya taarifa muhimu na hivyo kushindwa kufanyiwa kazi. Hapo awali, mwezi Agosti, 2010 Bodi ilitangaza kupitia vyombo vya habari majina ya waombaji wote ambao fomu zao zilikuwa na kasoro na kuwataka warekebishe katika kipindi cha wiki tatu. Hadi hivi sasa waombaji 760 wa vyuo vyote hawajafanya marekebisho hayo. Badala yake, wanataka Bodi iwape tu mikopo bila kurekebisha mapungufu muhimu katika maombi yao, kitu ambacho hakiwezekani.

Msimamo wa Bodi ni kwamba fomu zenye hitilafu hazitafanyiwa kazi hadi hapo taarifa zitakapokamilishwa na wanafunzi husika ambao orodha yao iko katika tovuti ya Bodi kuanzia Agosti, 2010.

4.3 Baadhi ya wanafunzi kutopata mikopo licha ya kuwa wana sifa stahili.

Uchunguzi wa madai haya ulionyesha kuwa Wanafunzi hawa ni wale wenye udahili kwenye zaidi ya chuo kimoja na wengine mikopo yao ilishalipwa kupitia vyuo walivyopangiwa na Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU).

Msimamo wa Bodi ni kwamba haiwezi kutoa mkopo kwa mwanafunzi mwenye udahili katika zaidi ya chuo kimoja. Hivyo, wanafunzi wenye tatizo hilo walishauriwa kuwasiliana na Vyuo vyao na TCU ili Bodi iarifiwe ni Chuo gain wanaruhusiwa kujiunga nacho. Aidha kwa wale ambao mikopo yao imeshapelekwa kwenye Vyuo walivyopangiwa na TCU, itabidi wasubiri hadi hapo fedha hizo zitakaporejeshwa Bodi na hivyo waweze kutumiwa huko walikohamia kwani Bodi haiwezi kulipa mikopo miwili kwa mwanafunzi huyo huyo (multiple loans).

5.0 CHUO CHA USIMAMIZI WA FEDHA (IFM)

Alhamisi, Desemba 16, 2010, Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wapatao 200 waliandamana hadi ofisi za Bodi wakiwa na dai lifuatalo:

5.1 Dai kuwa Bodi iwalipie ongezeko la ada.

Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kiliongeza ada kuanzia mwaka wa masomo 2008/2009 lakini viwango hivyo vipya vya ada havitambuliwi na Bodi kutokana na maelekezo ya Serikali yaliyotolewa mwaka wa masomo 2007/2008 yaliyoilekeza Bodi kuendelea kutoa mikopo kwa viwango vya ada vilivyotozwa katika mwaka wa masomo 2007/2008.

Msimamo wa Bodi ni kwamba, Bodi itaendelelea kutumia viwango vya ada vya mwaka wa masomo 2007/2008 kwa mwaka wa masomo 2010/2011 kwa waombaji wapya na wanafunzi wanaoendela na masomo hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo. Aidha, Mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2010/2011 uliotolewa na Bodi ambao ulitangazwa kupitia vyombo vya habari mwezi Machi, 2010 na ambao unapatikana kwenye tovuti ya Bodi www.heslb.go.tz, ulieleza bayana juu ya msimamo huu kabla ya Bodi kuanza kutoa fomu za kuomba mikopo kwa mwaka 2010/2011.

Hivyo, si sahihi kuilaumu Bodi katika mgomo huo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwani Bodi inatekeleza maelekezo iliyopewa na Serikali ambayo yanalenga kuzuia upandishaji holela wa ada katika Vyuo vya Elimu ya Juu.

6.0 CHUO KIKUU CHA KIISLAM CHA MOROGORO (MUM)

Alhamisi, Desemba 16, 2010 Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro wapatao 180 nao waliandamana hadi Bodi ya Mikopo wakiwa na madai yafuatayo:

6.1 Bodi iwalipie ongezeko la ada.

Chuo kikuu cha Kiislam cha Morogoro kimeongeza kima cha ada katika mwaka wa masomo 2010/2011 na kuwataka wanafunzi wanaonufaika na mikopo wadai ongezeko hilo kutoka Bodi. Dai hili ni kama lile la IFM.

Msimamo wa Bodi ni kwamba itaendelelea kutumia viwango vya ada vya mwaka wa masomo 2008/2009 kwa mwaka wa masomo 2010/2011 kwa waombaji wapya na wanafunzi wanaoendela na masomo hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo.

Hivyo, kwa mgomo huo nao, si sahihi kuitupia lawama Bodi ya Mikopo kwani Bodi inatekeleza maelekezo ya Serikali.

6.2 Wanafunzi waliohama kutoka vyuo vingine kutopewa mikopo.

Wanafunzi hawa waligundulika kuwa ni wale wenye udahili kwenye zaidi ya chuo kimoja kutokana na kuomba nafasi za masomo nje ya “Central Admission System” unaoratibiwa na TCU. Wanafunzi wenye udahili kwenye zaidi ya chuo kimoja ni wale ambao hawakufuata utaratibu huo na hivyo kuomba udahili moja kwa moja kwenye vyuo hivyo, bila kupitia TCU.

Msimamo wa Bodi ni kwamba haitatoa mkopo kwa mwanafunzi yeyote ambaye ana udahili kwenye zaidi ya chuo kimoja. Aidha, Mwanafunzi ambaye atakopeshwa ni yule aliyepitishwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE) kupitia Centralised Admission System (CAS). Hivyo, wanafunzi husika wanashauriwa wawasiliane na Vyuo vyao pamoja na TCU na siyo kuisababishia Bodi lawama ambazo hazina msingi wowote.

7.0 CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM)

Ijumaa, Desemba 10, 2010, Wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi za Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waligoma wakiwa na madai kadhaa dhidi ya Uongozi wa Chuo chao. Aidha, wanafunzi hao pia walikuwa wanadai kwamba Chuo chao kiweke mafunzo kwa vitendo katika mtaala wake na hivyo kuiwezesha Bodi ya Mikopo kuwapa mikopo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Mikopo kwa kipengele cha Mafunzo kwa Vitendo hutolewa tu kwa Wanafunzi wanaosomea kozi ambazo mitaala yake imepangwa kuwawezesha Wanafunzi kwenda kwenye mafunzo hayo nje ya chuo. Wanafunzi wanaochukua masomo ya Sayansi za Jamii UDOM, mitaala yao haikupangwa kuwawezesha kufanya mafunzo kwa vitendo. Hivyo, wanafunzi hao walikuwa wanashinikiza uingizwaji wa mafunzo kwa Vitendo katika mitaala ya masomo ya sayansi ya jamii, lengo likiwa ni kuweza kupata mikopo baada ya hapo.

Msimamo wa Bodi ni kwamba mikopo ya mafunzo kwa vitendo itatolewa kwa programu ambazo vyuo vimezibainisha katika mitaala kwamba zinahitaji mafunzo kwa vitendo na siyo vinginevyo. Aidha, mikopo ya mafunzo kwa vitendo itatolewa tu baada ya Bodi kupata taarifa na orodha kutoka vyuoni ikiainisha wanafunzi wanaotakiwa kwenye mafunzo hayo, muda na mahali wanakokwenda.

Hivyo, migomo iliyotokea UDOM haina uhusiano wowote na Bodi ya Mikopo, tofauti kabisa na Vyombo vya habari vilivyoripoti.

8.0 CHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA KAMPALA (KIU)

Alhamisi, Desemba 23, 2010 baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) waliandamana na kwenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na baadaye kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu wakidai kutaka kujua “status” ya chuo chao na kama wao nao wanakopesheka kama ilivyo kwa vyuo vingine vinavyotambulika hapa nchini.

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala kimepata ithibati kutoka Kamisheni ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kuratibu utoaji wa Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili kwa mfumo wa masafa (Open and Distant Learning and Part time Basis).

Vigezo na taratibu za utoaji mikopo zinasisitiza kuwa mikopo itatolewa kwa mwombaji ambaye amedahiliwa kusoma Stashahada au Shahada “on full time basis”.

Msimamo wa Bodi ni kwamba, kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya utoaji mikopo, wanafunzi wanaosoma kwa mfumo wa ‘ODL’ hawana sifa za kukopeshwa. Chuo hicho kinatakiwa kipeleke suala lake TCU na siyo Bodi. Hivyo siyo sahihi kuihusisha Bodi na mgomo wa wanafunzi wa Chuo hicho kwani TCU ndiyo inayohusika na kutoa ithibati kwa vyuo vya elimu ya juu nchini na siyo Bodi ya Mikopo.

9.0 CHUO KIKUU CHA ARDHI (ARU)

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi waliandamana Ijumaa Desemba 24, 2010 katika maeneo ya chuo chao wakiwa na madai kumi, tisa kati ya hayo yakiwa dhidi ya Uongozi wa Chuo, baadhi yake ni uhaba wa malazi, kubadilishwa kwa mihula na uhaba wa vifaa vya kujifunzia. Aidha, wanafunzi hao walikuwa wanakilaumu Chuo kwa kutowasilisha kwa wakati, majina ya wanafunzi wa chuo hicho walioko mwaka 2, 3 na 4 wanaopaswa kwenda katika mafunzo kwa vitendo.

Lakini taarifa za wanafunzi wanaostahili kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo ziliwasilishwa kwenye Bodi tarehe 23 Desemba, 2010 baada ya Uongozi wa Chuo kusikia fununu za mgomo wa wanafunzi. Hivyo, Bodi ya Mikopo haipaswi kulaumiwa katika mgomo huo bali chuo ndicho kilaumiwe.

Ijumaa, Januari 21, 2010, wanafunzi wa Chuo hicho waliandamana pia wakiwa na madai ya wanafunzi wapatao 226 wa mwaka wa kwanza kutopewa mikopo yao ya chakula na malazi kwa robo ya pili. Ufuatiliaji wa suala hilo, ulionyesha kuwa majina ya wanafunzi hao 226 wa Skuli ya Sayansi ya Mazingira na Teknolojia (School of Environmental Science and Technology) hayakuwasilishwa na chuo kwenye Bodi. Chuo kiliwasilisha majina hayo tarehe 21 Januari, 2011 siku wanafunzi walipoandamana.

Msimamo wa Bodi ni kwamba mikopo ya mafunzo kwa vitendo itatolewa kwa programu ambazo vyuo vimezibainisha katika mitaala kwamba zinahitaji mafunzo kwa vitendo na siyo vinginevyo.

Aidha, mikopo ya mafunzo kwa vitendo itatolewa tu baada ya Bodi kupata taarifa na orodha kutoka vyuoni ikiainisha Wanafunzi wanaotakiwa kwenye mafunzo hayo, muda na mahali wanakokwenda angalau mwezi mmoja kabla ya tarehe ya kuanza kwa mafunzo hayo.

Mikopo katika robo ya pili, kwa ajili ya chakula na malazi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, inatolewa mara baada ya vyuo kuwasilisha orodha za wanafunzi waliosajiliwa vyuoni. Mikopo haitatolewa pasipokuwa na orodha hiyo.

HITIMISHO

Taasisi nyingi za elimu ya juu ambazo wanafunzi wake wanakopeshwa na Bodi zimekuwa zikichelewa kuleta taarifa muhimu zikiwemo orodha ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosajiliwa, matokeo ya mitihani na orodha za majina ya wanafunzi wanaokwenda katika mafunzo kwa vitendo. Matokeo ya kucheleweshwa kwa taarifa hizo yameibua malalamiko miongoni mwa Wanafunzi na hivyo kuelekeza shutuma kwenye Bodi bila sababu za msingi.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuwakumbusha wadau wake hususan Vyuo vya Elimu ya Juu na Wanafunzi kuzingatia na kutekeleza taratibu za utoaji mikopo kuepusha malalamiko na kuwezesha kazi hiyo kufanyika kwa ufanisi. Taarifa hii inasisitiza juu ya umuhimu wa kuelewa taratibu za utoaji mikopo kabla ya kushutumu na kutoa malalamiko yasiyokuwa na msingi wowote kwa Bodi ya Mikopo.

Aidha, Bodi inaviomba Vyombo vya Habari na Wadau wengine kuwasiliana mara kwa mara na Menejimenti ya Bodi ili kupata taarifa sahihi zinazohusu mwenendo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi, badala ya kukurupuka na kuchochea Umma uwe na chuki zisizokuwa na msingi, dhidi ya Bodi, kama Mhariri wa “The Sunday Guardian” alivyokurupuka, katika toleo la Jumapili tarehe 23 Januari, 2011. Bila shaka baada ya maelezo ya kina ya sababu za migomo hiyo, Mhariri huyo atagundua kwamba anapaswa kuwa makini zaidi katika uandishi wake wa habari.

Aidha, Bodi inaomba isigeuzwe kuwa Jimbo la Uchaguzi ambapo kila anayetaka kusikilizwa na Wanafunzi wa Elimu ya Juu, basi anatumia mgongo wa Bodi ya Mikopo kwa kutoa shutuma ambazo hajazifanyia uchunguzi wa aina yoyote.

Pia, Bodi inapenda kusisitiza kwamba hata kama ikivunjwa, kama Mhariri wa “The Sunday Guardian” na Kiongozi mmoja wa UVCCM walivyokurupuka kusema, hata chombo kitakachoundwa badala ya Bodi nacho kitabidi kivunjwe hapo baadaye, endapo changamoto zilizotajwa hapo juu na nyingine nyingi zinazosababishwa na Wadau wengine na siyo Bodi ya Mikopo, hazitapata ufumbuzi.

IMETOLEWA NA:

MKURUGENZI MTENDAJI

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA

No comments:

Post a Comment