Monday, 5 March 2012

MWELEKEO WA MVUA ZA MACHI HADI MEI (MASIKA) 2012 NCHINI TANZANIA

Taarifa hii inatoa tathimini ya msimu wa mvua za Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2012, mvua zinazoendelea katika maeneo ya kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na mikoa ya kusini pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei, 2012.
A.        UTANGULIZI
Tathimini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2011 inaonyesha kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za kutosha. Baadhi ya maeneo ya nchi yalipata mvua nyingi na kulikuwa na vipindi vya mvua kubwa kuelekea mwishoni mwa msimu ambazo zilisababisha maafa katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, Mara, Manyara, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza. Hata hivyo, mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri. Maeneo machache yanayopata msimu mmoja wa mvua (mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi pamoja na kusini mwa Morogoro) yalipata kiwango kidogo cha mvua.

Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2012 unaonyesha maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, isipokuwa kwa mkoa wa Shinyanga ambao unatarajiwa kupata mvua za wastani. Mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika maeneo ya kusini mwa Iringa, Ruvuma na Mtwara ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Mvua hizi zinatarajiwa kuendelea mpaka mwishoni mwa mwezi wa Aprili 2012. Viashiria vilivyopo na vinavyotarajiwa kusababisha mvua hizi ni kuwepo kwa joto chini ya wastani katika maeneo ya tropikali ya bahari ya Atlantiki, sambamba na kuwepo kwa joto juu ya wastani katika maeneo ya kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi. Hali hii inatarajiwa kusababisha upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo kuvuma kuelekea nchini mwetu.

B: TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA 2011
Mvua katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2011, ziliendelea vizuri katika maeneo mengi ya nchi.. Hata hivyo mtawanyiko wake haukuwa wa kuridhisha ambapo baadhi ya maeneo yalipata mvua kubwa kuelekea mwishoni mwa masimu. Vifuatavyo ni viwango vya mvua pamoja na wastani wa muda mrefu katika baadhi ya vituo hivyo:
Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:
Pwani ya Kaskazini: Tanga 244.5 mm (280.8%), Pemba 389.2mm (189.5%), Mlingano 557.9mm (336.7%), Handeni 164.4mm (68.9%), Kizimbani 282.7mm (95.8%), Zanzibar 342.0mm (96.4%), Morogoro 83.8mm (110.1%) na JNIA 469.9mm (94.2%).
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: Moshi 102.4mm (122.8%), Lyamungu 179.2mm (189.2%), Same 66.0mm (65.5%) na KIA 105.5mm (329.7%).
Kanda ya Ziwa Viktoria: Mwanza 247.2mm (113.2%), Bukoba 347.8 mm (128.8%), Musoma 142.8mm (117.8%) na Shinyanga 276.5mm (125.1%).

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Magharibi: Tabora 91.7 mm (63.2%) na Kigoma 202.2mm (101.1%).
Kanda ya Kati: Dodoma 38.2mm (51.8%), Hombolo 60.2mm (154.4%) na Singida 50.6mm (34.7%).
Nyanda za Juu Kusini Magharibi: Iringa 141.3mm (94.1%), Mbeya 92.0mm (36.9%), Tukuyu 312.6 mm (253.7%) na Igeri 163.0mm (250.8%).
Maeneo ya Kusini: Mtwara 81.7mm (70.0%), Kilwa 118.5mm (166.2%) na Songea 81.4mm (169.6%).
Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani, wakati viwango vya kati ya asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.

C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa na athari zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2012 hapa nchini.

Uchambuzi wa hali ya joto katika ukanda wa tropikali ya bahari ya Pasifiki kwa kipindi cha mwezi Februari 2012 unaonyesha hali ya joto lililo chini ya wastani ambalo linaashiria kuwepo kwa La Niña hafifu. Mwelekeo katika kipindi cha Mwezi Machi hadi Mei unaonyesha kuwepo kwa ongezeko kidogo la joto la bahari litakalopelekea kutoweka kwa La Niña na joto la Bahari linatarajiwa kuwa la wastani.

Joto chini ya wastani  katika tropikali ya Bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuendelea katika kipindi chote cha msimu likiambatana na ongezeko kidogo la joto kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi na hivyo kupelekea kuwepo kwa upepo kutoka magharibi kuvuma kuelekea katika maeneo ya nchi yetu , hali ambayo inatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua hususani magharibi mwa nchi.

Tofauti ndogo ya joto kati ya Magharibi na Mashariki mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuwepo kwa kipindi chote cha Mwezi wa Machi, 2012. Hali hii inatarajiwa kusababisha kuvuma kwa upepo kutoka Baharí ya Hindi kuelekea pwani ya Afrika Mashariki.

Mifumo ya migandamizo ya hali ya hewa kwa maeneo yaliyopo kaskazini mwa Tropiki ya Kansa inatarajiwa kuwa hafifu ukilinganisha na maeneo yaliyopo Kusini mwa Tropiki ya Kapirikoni. Hali hii inatarajiwa kusababisha Ukanda wa Mvua kutoka kusini kuelekea  kaskazini kupanda kwa haraka hivyo kupelekea mvua katika msimu wa masika kuisha mapema.

Kutokana na ongezeko dogo la joto linalotarajiwa katika ukanda wa kusini-magharibi mwa Bahari ya Hindi pamoja na viashiria vingine, matukio ya vimbunga kusini-magharibi mwa Bahari ya Hindi yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kusababisha kuongezeka au kupungua kwa mvua katika baadhi ya maeneo nchini kulingana na nguvu ya vimbunga hivyo na maeneo vitakapotokea.

D: MWELEKEO WA MVUA MACHI –MEI 2012
(i)     Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:

Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. katika mikoa ya Kagera, Mara na Kigoma-kaskazini, na kusambaa katika maeneo mengine (Mwanza na Shinyanga) wiki ya pili ya mwezi Machi. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika mikoa hiyo, isipokuwa mkoa wa Shinyanga ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani .

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba): Msimu wa mvua unatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. Mvua za msimu katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua yalipata mvua zisizo za msimu katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2012 zilizosababishwa na kuwepo kwa matukio ya vimbunga hafifu katika Bahari ya Hindi.

(ii)      Mvua za Msimu
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Rukwa ):
Mvua zinazoendelea katika maeneo haya zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya mikoa ya Tabora na Rukwa-mashariki ambayo mvua  zinatarajiwa kuwa za wastani. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2012.

Maeneo ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi)
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani, isipokuwa kaskazini mwa mkoa wa Lindi ambapo zinatarajiwa kuwa za wastani. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2012.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo haya, isipokuwa mkoa wa Singida ambao unatarajiwa kupata mvua za wastani. Msimu wa mvua unaendelea na unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2012.

Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro-kusini):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani, isipokuwa maeneo ya kusini ya mkoa wa Iringa na Morogoro ambapo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Aprili, 2012.

Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu(miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Tofauti katika maeneo madogo madogo na mabadiliko ya muda mfupi yanarajiwa. Vipindi vifupi vya mvua Kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Aidha vipindi virefu vya upungufu wa mvua vinaweza kutokea hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua nchini.

3: USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na unyevu wa udongo wa kutosha isipokuwa maeneo machache ya kusini mwa nchi ambapo upungufu wa unyevunyevu wa udongo unatarajiwa katika mwezi Aprili, 2012. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, unyevunyevu wa udongo kupita kiasi unaweza kuathiri maendeleo ya mazao hususani katika mashamba yaliyopo mabondeni. Katika maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini-mashariki, ukanda wa ziwa Victoria pamoja na magharibi (Kigoma) wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo.

Maeneo ya magharibi (Tabora na Rukwa), maeneo ya kati, nyanda za juu kusini-magharibi pamoja na maeneo ya kusini mwa nchi wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli za kawaida za kilimo. wakati huu mazao yanapoelekea kukomaa. Aidha maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yanaweza kunufaika kwa kuotesha mazao kama vile mihogo, na mazao ya muda mfupi kama vile viazi vitamu na jamii ya mikunde. Mamlaka inawashauri wakulima waendelee kutafuta na kufuata ushauri wa Maafisa Ugani katika maeneo yao.

Maji na Nishati
Vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo mengine yaliyosalia, hayatarajiwi kuwa na ongezeko kubwa la vina vya maji.
Malisho ya mifugo
Hali ya malisho inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi nchini. Wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi. Hata hivyo wafugaji wanashauriwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo katika maeneo yao.
Mamlaka za Miji
Mamlaka za miji katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wstani, zinashauriwa kusafisha mifumo ya maji taka ili kuepusha maji kutuama na kupunguza madhara yatokanayo na mafuriko.
Sekta ya Afya
Maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani, kuna uwezekano wa kutokea milipuko ya magonjwa ya malaria na kipindupindu. Mamlaka husika zinashauriwa kuchukua tahadhari na maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Menejimenti ya Maafa
Taasisi za maafa na wadau husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kutokea. 

Dkt. Agnes L. Kijazi
Mkurugenzi Mkuu

No comments:

Post a Comment