Tuesday 8 February 2011

HOTUBA YA MHESHIMIWA PROFESA MAKAME MBARAWA (MB), WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWENYE SHEREHE ZA UFUNGUZI JENGO LA MAKAO MAKUU YA TCRA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kufungua rasmi jengo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) katika barabara ya Sam Nujoma jijini Dare s Salaam leo asubuhi.Kushoto ni Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa na kulia ni Mkurugenzi mkuu wa TCRA Prof.John Nkoma

Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu;
Mheshimiwa Jaji Mstaafu Buxton David Chipeta, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA
Wajumbe wa Bodi ya TCRA;
Wageni Waalikwa;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana.

MHESHIMIWA RAIS;
Kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii ya pekee kukushukuru wewe Mheshimiwa Rais kwa kukubali mwaliko wetu wa kuja kuzindua Jengo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania - Mawasiliano Towers.

MHESHIMIWA RAIS;
Sisi viongozi wa Wizara pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) tumefarijika sana kwa uamuzi wako wa kujumuika nasi siku ya leo, pamoja na kuwa na majukumu mengi ya kitaifa lakini umeweza kupata fursa ya kufika hapa. Tunakushukuru na karibu sana.

MHESHIMIWA RAIS;
Kwa kuzingatia program yetu hapa leo, jukumu langu kubwa ni kukukaribisha Mheshimiwa Rais kutuzindulia jengo la Mawasiliano Towers ambalo limejengwa kwa fedha zetu sisi wenyewe. Hata hivyo, kabla ya kukukaribisha Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo, naomba nizungumze kwa ufupi masuala machache yanayohusu sekta ya mawasiliano.

MHESHIMIWA RAIS;
Kwa kipindi kifupi nilichokaa katika Wizara hii baada ya kuniteua mwezi Novemba 2010, nimepata fursa ya kufahamu masuala kadhaa kuhusu sekta ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto mbalimbali za sekta ya mawasiliano.

MHESHIMIWA RAIS;
Chini ya uongozi wako, umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inachangia vyema zaidi katika kuleta maendeleo hapa nchini. Hii inajidhihirisha katika kuipatia sekta ya mawasiliano kipaumbele katika sera, mikakati na sheria mbalimbali za sekta. Sera za Mawasiliano, Sera ya Teknohama, Sera ya Posta, Sheria ya mawasiliano ya Kielekroniki na Posta na Kanuni zake ambazo zitakamilishwa hivi karibuni ni baadhi tu ya Sera na sheria muhimu ambazo umehakikisha kuwa zinapata nafasi stahiki katika utekelezaji wake ili sekta ya mawasiliano iweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa letu.

Sera, Sheria na Kanuni hizi zimekuwa chachu ya maendeleo ya sekta na uchumi kwa ujumla kwa kuwa zimeweza kuweka mazingira mazuri ambayo yataiwezesha sekta kusonga mbele. Matokeo yake makampuni za ndani na za nje yameweza kuwekeza katika sekta ya mawasiliano na TEKNOHAMA hapa nchini. Umekuwa ukifanya hivyo kwa kusudi la kuhakikisha kuwa nchi yetu haibaki nyuma katika suala zima la teknolojia ya habari na mawasiliano duniani.

MHESHIMIWA RAIS;
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 iliweka bayana mikakati ya maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini na kutamka bayana kuwa itafanya jitihada za makusudi katika kuboresha sekta ya mawasiliano ili kila raia wa nchi hii aweze kupata mawasiliano yaliyo bora na kwa bei nafuu.
Hakika katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Nne unayoiongoza, sekta ya mawasiliano imekuwa ikikua kwa kasi na kuongeza pato la taifa, ajira na kurahisisha maisha ya watanzania katika shughuli zao za kila siku.
Itakumbukwa Mheshimiwa Rais, wakati wa ziara zako mbali mbali ndani na nje ya nchi umekuwa ukiwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta mbali mbali ikiwa ni pamoja na sekta ya mawasiliano. Tuna kila sababu za kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa umuhimu uliouweka katika kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini katika kipindi chote cha uongozi wako tangu uingie madarakani.

MHESHIMIWA RAIS;
Kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika kusimamia sekta hii, imewezesha kupatikana kwa maendeleo makubwa katika sekta na utendaji bora unaoweza kuigwa na wengine. Usimamizi mzuri wa sekta ya mawasiliano nchini umewezesha wawekezaji kuwa na imani ya kuwekeza hapa nchini na ndiyo maana tumekuwa nchi pekee na ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na makampuni mengi ya mawasiliano baada ya kufungua milango ya uwekezaji wa sekta ya mawasiliano.
Mara kadhaa taasisi na nchi marafiki zimekuwa zikiomba wataalamu wao kuja kujifunza kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania namna ya kusimamia sekta ya mawasiliano kwa ufanisi zaidi. Hata katika nyanja za kimataifa, Mamlaka ya Mwasiliano Tanzania ni Mamlaka inayoheshimika na kuaminika sana. Tanzania, kupitia Mamlaka hii, imekuwa mmoja wa wajumbe wanne kutoka bara la Afrika, wa Baraza la Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano ya Simu (International Telecommunication Union) kuanzia mwaka 2006 hadi 2010. Aidha, kutokana na utendaji mzuri wa Mamlaka hii, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilichaguliwa kuwa ni Mamlaka bora ya usimamizi (best regulator) wa masuala ya mawasiliano barani Afrika kwa mwaka 2009 na taasisi ya African Telecom People ya Ufaransa.

Ni dhahiri kwamba utendaji mzuri wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania umetokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na sera, sheria na kanuni za nchi yetu ambazo wewe Mheshimiwa Rais ndiye msimamizi mkuu. Wawekezaji katika sekta na watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano wanapata uhakika (confidence) katika kuwekeza na pia katika kutumia huduma za mawasiliano.

MHESHIMIWA RAIS;
Palipo na mafanikio, hapakosi changamoto. Ninaamini kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano tutaendelea kushirikiana kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo ili sekta ya mawasiliano iweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi yetu.

MHESHIMIWA RAIS;
Ujenzi wa jengo hili na kukamilika kwake kunaonyesha jinsi TCRA ilivyoweza kulenga mbali. Pamoja na kukidhi mahitaji yao ya kiofisi, jengo hili limekuwa kivutio katika mandhari ya jiji letu na pia linachangia katika pato la taifa letu ikiwa ni pamoja kuongeza ajira na wawekezaji kupata sehemu ya kuweka ofisi zao na hata kufanyia vikao na mikutano mbali mbali.

MHESHIMIWA RAIS;
Kama nilivyoahidi nia yangu siyo kutoa hotuba ndefu, hivyo baada ya kusema haya machache, kwa heshima na taadhima naomba sasa nikukaribishe utoe nasaha zako zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na hadhara hii.

KARIBU MHESHIMIWA RAIS

No comments:

Post a Comment