USULI .
Mhesimiwa Rais , nakupa pole kwa majukumu mengi na mazito ya kuendesha nchi yetu yenye matatizo mengi na kila mahali hatuonekani kufanikiwa ila matatizo na umasikini kwa watanzania vinaonekana kuongezeka kwa kasi kubwa, huku uzalishaji ukipungua kwa kasi kubwa na wakati huo huo wawekezaji ama wakiamua kuondoa mitaji yao au wale wengine ambao hii ni nchi yao hawana pa kukimbilia wakiwa wanafilisika kutokana na matatizo ya nishati ya umeme na hata mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo na mashine mbalimbali za uzalishaji.
Pamoja na hayo yote naomba leo uchukue muda wako kidogo japo uweze kusoma maoni yangu kwani naamini kuwa yanaweza yakawa ni mchango katika kusaidia katika kukuza uchumi wetu kama yatachukuliwa maanani na kufanyiwa kazi, Pamoja na ukweli kuwa ninajua unavyo vyombo vingi sana na watu wengi sana ambao wanakushauri kwenye mambo mbalimbali si vibaya ukasoma maoni yangu pia .
Mheshimiwa Rais , kwa ruhusa yako naomba leo niweze kuchukua muda huu kukueleza kwa kina juu ya matatizo yaliyopo kwenye biashara ya uwindaji wa Kitalii na haswa kutokana na wasaidizi wako ambao umewateua kutokutaka kupokea ushauri ama kupuuzia ushauri ambao wamekuwa wakipewa na watu mbalimbali na hata ushauri uliotolewa na wabunge wakati wakijadili bajeti ya wizara ya Maliasili na utalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Rais nimeamua kufanya hivyo kwa kutumia njia hii kwani naamini kabisa kuwa wasaidizi wako na haswa waziri na watendaji wa wizara hiyo wamekuwa hawakuelezi ukweli juu ya biashara hii ya uwindaji wa kitalii au hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na biashara hii na ndio maana wanashindwa kukushauri vizuri kuhusiana na jambo hili .
Hii ni kutokana na ukweli kuwa Matumizi ya raslimali ya wanyamapori hayajapewa thamani na hivyo sekta hii inachangia kidogo sana kitaifa kuliko ilivyotegemewa. Licha ya kuwepo uwezo wa kuzidisha mapato kutokana na wanyamapori kupitia misingi ya ushindani wa kiuchumi, hili halifanyiki. Hii inatoa fursa kwa ufisadi. Kawaida iliyopo katika usimamizi wa wanyamapori kwa sasa hairuhusu kukuza manufaa ya uchumi kitaifa kutokana na raslimali ya wanyamapori.
Historia ya uwindaji wa kitalii Tanzania.
Mheshimiwa Rais utakumbuka kuwa biashara hii ilikuwa inafanyika hapa nchini tangu miaka ya 1960 tena kwa kutumia sheria ya mkoloni iliyotungwa 1958. Mnamo mwaka 1973 hadi 1978 biashara hii ilifungwa kutokana na tangazo la serikali namba 210 lililochapwa mwaka 1973.
Kutokana na biashara hii kufungwa kwa kipindi hicho tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanyama walipungua kwa kasi kubwa sana na haswa wa jamii ya Tembo,Vifaru ,Simba na wengineo kutokana na ujangili uliofanywa kwa kipindi hiki ambacho serikali ilikuwa imezuia biashara kuendelea kufanyika kihalali .
Mwaka 1978 serikali iliamua kuruhusu biashara hii kuendelea kufanyika na iliwekwa chini ya ukiritimba wa shirika la serikali la TAWICO ambalo lilipewa haki ya kufanya biashara hii na ndilo lilikuwa na jukumu la kugawa vitalu pamoja na kuendesha biashara hii.
Mnamo mwaka 1984 ukiritimba wa TAWICO katika kuendesha biashara hii uliondolewa na ndipo makampuni nane yakiwemo ya kigeni yalipewa vibali rasmi na vitalu kwa ajili ya kuendesha biashara hii hapa nchini .Naeleza yote haya ili uweze kunielewa kwani tangu wakati huo makampuni haya yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, huku yakiendelea kuwekeza mitaji yao kwenye sekta hii muhimu kwa uchumi wetu , pia sheria zetu tumekuwa tukiziboresha kulingana na mahitaji ya wakati, na sasa tunatumia sheria namba 5 iliyotungwa mwaka 2009 na kutiliwa saini na wewe mwenyewe tarehe 12 Machi 2009.
Mheshimiwa Rais, Biashara hii tangu kurejeshwa mwaka 1984 imekuwa ikifanywa kwa ushirikiano/ubia kati ya makampuni mbalimbali ya watanzania na yale ya wageni kwa lugha ya leo tunawaita wawekezaji . Ila Sheria namba 5 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu wa kuwa na Makampuni yanayomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100, kama ni kuingia ubia na makampuni ya nje basi lazima watanzania wamiliki kuanzia asilimia 25 ya hisa na kuendelea.
Mheshimiwa Rais, sheria hii uliisoma na kuitia saini wewe mwenyewe na hivyo sioni kama nitakuwa sahihi nikitaka kukuelewesha kuhusiana na vifungu mbalimbali vilivyopo kwenye sheria hii kwani unaifahamu na ndio maana ukaitia saini.
Mheshimiwa rais, sheria hii katika kifungu cha 39 (3) (b) kinasema kuwa waziri atatunga kanuni kuhusiana na Makampuni ya Kigeni na yataweza kumilikishwa asilimia 15 ya vitalu vyote vitakavyogawanywa, ila hakuna mahali popote kwenye sheria hii imewekwa tafsiri ya neno kampuni ya kigeni maana yake nini au kuwa kampuni itatambulikaje kuwa hii ni ya kigeni !Je? kampuni za ubia nazo ni za kigeni, kwani masharti ya kampuni kuweza kupatiwa kitalu ni pamoja na kuwa kampuni iwe imesajiliwa Tanzania.
Mheshimiwa Rais nasema haya yote japo naamini kuwa wewe unayafahamu na uliamua kuisaini sheria yenye vifungu hivyo ambavyo vinazungumza kinyumenyume, kwa lugha ya huku mtaani kwetu vifungu kama hivyo huwa tunaita ni vya Kichina! Ila kwa wale watani zako wa kisiasa huwa nawasikia wakisema kuwa vimechakachuliwa!
Mheshimiwa rais, Naomba uniruhusu nimalizie kipengele hiki kwani nitakuwa na vipengele vingi kwa kutumia maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye leo ni Mbunge wa Pangani Mhe.Salehe Pamba, ambaye wakati sheria hii ilipokuwa inapitishwa alikuwa katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii alipoulizwa swali na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi chapisho la tarehe 09 Agusti 2011 kuhusiana na vifungu tajwa hapo juu alisema ifuatavyo:
“Swali: Unasemaje kuhusu kupunguzwa kwa kampuni za kigeni katika utalii wa uwindaji ambazo zimekuwa zinafanyabiashara kwa muda mrefu. Je hii itaathiri mapato ya nchi?
Jibu: Hapa pana tatizo kubwa. Kwanza hatuambiwi kuhusu ufanyajikazi wa makampuni ya uwindaji wa kitalii pamoja na mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vitalu vya uwindaji wa kitalii.
Idara ya Wanyamapori imefanya mapato kuwa siri kwa miaka kumi iliyopita. Kabla, mapato yalikuwa yakitangazwa kwenye vyombo vya habari. Takwimu za hali ya uchumi 2010 inaonyesha uwindaji wa kitalii uliingizia serikali mapato ya dola za Kimarekani 18.4 milioni 2009 na dola za Kimarekani 14.4 milioni mwaka 2010. Pato lilishuka kwa asilimia 21.7.
Kuna sababu mbalimbali zilisosababisha pato kushuka ikiwa ni pamoja na ujangili, ardhi kuchukuliwa kwa kilimo na ukataji wa magogo sehemu zilizotengwa kwa wanyamapori.
Hata hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitangaza mapato ya uwindaji wa kitalii ya miaka mitatu iliyopita na ambapo makampuni ya kigeni yalilipa kodi Sh8 bilioni wakati makampuni ya wazawa yalilipa mapato ya Sh500milioni”. Chanzo tovuti ya mwananchi tarehe 06/09/2011 saa 22:50
Jibu: Hapa pana tatizo kubwa. Kwanza hatuambiwi kuhusu ufanyajikazi wa makampuni ya uwindaji wa kitalii pamoja na mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vitalu vya uwindaji wa kitalii.
Idara ya Wanyamapori imefanya mapato kuwa siri kwa miaka kumi iliyopita. Kabla, mapato yalikuwa yakitangazwa kwenye vyombo vya habari. Takwimu za hali ya uchumi 2010 inaonyesha uwindaji wa kitalii uliingizia serikali mapato ya dola za Kimarekani 18.4 milioni 2009 na dola za Kimarekani 14.4 milioni mwaka 2010. Pato lilishuka kwa asilimia 21.7.
Kuna sababu mbalimbali zilisosababisha pato kushuka ikiwa ni pamoja na ujangili, ardhi kuchukuliwa kwa kilimo na ukataji wa magogo sehemu zilizotengwa kwa wanyamapori.
Hata hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitangaza mapato ya uwindaji wa kitalii ya miaka mitatu iliyopita na ambapo makampuni ya kigeni yalilipa kodi Sh8 bilioni wakati makampuni ya wazawa yalilipa mapato ya Sh500milioni”. Chanzo tovuti ya mwananchi tarehe 06/09/2011 saa 22:50
Mheshimiwa rais , huyu ndio alikuwa Mtendaji Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii ambaye naamini kuwa alikushauri na aliishauri serikali kuanzia kwenye kuandaa mswada na katika kuhakikisha kuwa sheria hiyo inapitishwa na Bunge pamoja na vifungu hivyo na leo baada ya kuwa Mbunge anakugeuka na kusema kuwa sheria hiyo na haswa vifungu hivyo vina matatizo makubwa ! Hiki ni kati ya vitu ambavyo vimenisukuma kukuandikia barua hii ya wazi nikiamini kuwa kama hukupata fursa ya kusoma maneno yake hayo basi hata wewe utagundua kuwa kuna tatizo mahali kwenye sheria hiyo na vifungu vyake kwani hata muaandaaji leo anaikana sheria yake mwenyewe, sijajua nini kitatokea kama Bunge likiulizwa leo juu ya sheria hiyo maoni yao yatakuwa nini, naamini hata wewe unawaza hivyo hivyo! Wakati ukiwaza hayo naomba kuingia kifungu kinachofuata.
TANGAZO MAALUM: KUKARIBISHA MAOMBI YA VITALU VYA UWINDAJI WA KITALII.
Mheshimiwa rais tangazo hili lilitolewa kwenye vyombo mbalimbali vya habari mnamo tarehe 10 Februari 2011 na waziri Ezekiel Maige na lilitengenezwa chini ya Kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori, Sura ya 283 (Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2010) na huku ndiko kwenye mambo mengine yanayopaswa kuangaliwa, kutokana na tangazo hili nataka kuamini kuwa Mhe.Salehe Pamba alipotoa maoni yake alikwisha kulisoma na aliona tatizo ambalo leo nataka na wewe uweze kuliona ili ulitafutie ufumbuzi pamoja na ukweli kuwa nitakushauri juu ya nini mawazo yangu katika suala hili.
Tangazo lililowekwa kwenye tovuti ya wizara ya maliasili na utalii lilianza kwa kusomeka kama ifuatavyo, naomba kunukuu “Wizara ya Maliasili na Utalii inakaribisha maombi kutoka kwa kampuni zenye sifa zinazohitaji kugaiwa vitalu kwa ajili ya kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2013 hadi Machi, 2018. Jumla ya vitalu 156 vimetengwa kwa ajili ya ugawaji kwenye mapori ya akiba (Game Reserves), mapori tengefu (Game Controlled Areas) na maeneo ya wazi yenye wanyamapori (Open Areas). Vitalu hivyo vimepangwa katika makundi matano kulingana na ubora (Kiambatisho). Kampuni ya uwindaji wa kitalii inaweza kugawiwa hadi vitalu vitano (5) ambavyo vitakuwa katika makundi mchanganyiko ya ubora”.
Mheshimiwa Rais, tatizo la kwanza kabisa limeanza na jinsi tangazo lenyewe lilivyoaanza yaani linaelekeza kuwa ni makampuni mangapi yanahitajika kwa ajili ya kuweza kupatiwa vitalu kwani kwa kusema kuwa kila kampuni inaweza kupatiwa vitalu visivyozidi vitano maana yake ni kuwa kila mmoja anapaswa kuchakarika kuanzisha kampuni hata kama hana uwezo na ujuzi wa biashara hii kwani sasa yanahitajika makampuni 31.2 kwani kuna vitalu 156 vilivyotengwa kwa ajili ya kugawiwa ! ukichunguza utaweza kuona kuwa miongoni mwa kampuni zilizoomba utakuta zilizosajiliwa baada ya tangazo hili na huenda nyingine zimeundwa na wagawaji wenyewe wa vitalu hivyo ,nitaendelea kuchunguza kwa upande wangu ila naamini wewe unaweza kuitisha faili na kuuona ukweli kwa urahisi zaidi yangu.
Mheshimiwa Rais, tangazo hili haliangalii tena uwezo wa kampuni katika kuwekeza na kutenda kazi ila ni kuwa waziri ameona ni busara kuwa vitalu sasa vigawanywe kwa makampuni kutokana na idadi na sio ufanisi wa makampuni hayo na hapa kumbuka maneno ya Mhe.Salehe Pamba hapo juu alipozungumzia kodi na taarifa ya TRA ya miaka mitatu ukidadavua utajua waziri anataka kutupeleka wapi.
Mheshimiwa Rais, ukija kwenye kipengele cha sifa na utaratibu wa kuomba kitalu cha uwindaji kilichoweka na waziri Kulingana na matakwa ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283, ugawaji wa vitalu utafanyika baada ya waombaji wenye sifa kutuma maombi na kukubalika. Mwombaji wa vitalu anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
(a) Kuwa na kampuni iliyosajiliwa na Msajili wa Kampuni Tanzania kwa ajili ya uwindaji wa wanyamapori;
(b) Uzoefu wa angalau mmoja wa wakurugenzi usipungue miaka mitano katika fani ya biashara na uhifadhi wa wanyamapori nchini; na
(c) kwa kampuni za ubia kati ya Mtanzania na wageni, hisa za Mtanzania zisipungue asilimia 25 (ishirini na tano) ya hisa zote zilizolipiwa (Subscribed shares).
Mheshimiwa Rais, baada ya sifa hizi ambazo kila kampuni inapaswa kuwa nazo, wakati wa kufanya tathimini ya ni nani apewe kitalu na nani anyimwe kitalu waziri ameweka masharti mengine na kuyagawa makampuni haya kati ya yale yanayomilikiwa na Watanzania na yale ya wageni ! la kusikitisha zaidi hapa ni kuwa hata wale Watanzania ambao wameona kuwa hawana mitaji ya kutosha na kuamua kuwa na ubia na wageni na wao wamewekwa kwenye kundi la makampuni ya kigeni hii maana yake nini ?
Utakumbuka kuwa sheria yetu imesema wazi kuwa makampuni ya kigeni yataweza kupata asilimia 15 tuu ya vitalu vyote na hii maana yake ni kuwa ni vitalu 19 tuu vimetengwa kwa ajili ya makampuni ya kigeni na hapa maana yake ni kuwa hata wale watanzania walionunua hisa kwenye makapuni haya nao wanakuwa ni wageni na wananyimwa haki ya kumiliki vitalu , je ni kweli kuwa ukinunua hisa kwenye kampuni ya kigeni ya uwindaji wa kitalii unapoteza haki ya kuwa Mtanzania? Na kama ndivyo hivyo naomba utoe tamko mapema ili wale Watanzania ambao wamenunua hisa huko kwenye makampuni hayo na bado wanataka kuendelea kuwa Watanzania basi wauze hisa zao mara moja ili wasijepokonywa haki nyingine zaidi!
Mheshimiwa Rais na kuthibitisha hili ni kuwa kwa wale Watanzania ambao wameamua kushirikina na wageni (Watanzania daraja la pili) ili kuweza kuongeza mtaji wamepewa masharti magumu sana ukilinganisha na wale Watanzania ambao wanamiliki makampuni wao binafsi ambao nimegundua leo kuwa kumbe ndio daraja la kwanza! Kuna maana gani ya wewe kuendelea na safari za kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuongeza mitaji na huwa unaambatana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Kitanzania , huku mawaziri wako wakiwabagua Watanzania wanaoshirikiana na wageni hawa? Tuamini kuwa unawapiga changa la macho kama huku mtaani wanavyosema! Mimi sitaki kuamini hivyo na ndio maana nimekuandikia barua hii ya wazi ili na wale wanaosema hivyo huku mtaani wajue kuwa nimekueleza na utawaumbua kwani utatoa majibu ya kuonyesha vinginevyo.
Mheshimiwa Rais, masharti yenyewe ni kuwa kwa wale Watanzania walioshirikiana na wageni wanapaswa kuwa na magari mapya yasiyopungua matano na yawe 4WD, wale Watanzania wengine kwa kuwa hawakushirikisha wageni basi wanapaswa kuwa na magari mawili na ambayo sio mapya kwani tangazo linasema kuwa yawe angalau yameingizwa na kusajiliwa nchini kwa kipindi kisichozidi miaka 3 iliyopita ,hata kama yatakuwa yamenunuliwa kule tunakotoa magari yetu Dubai! Kuhusiana na mahema Watanzania ambao wamenunua hisa kwenye makampuni ya kigeni wanapaswa kuwa nayo 12 wakati wale ambao wanauwezo mkubwa wa kuendesha makampuni peke yao bila msaada wa mgeni wanapaswa kuwa nayo 6, kwa upande wa majokofu na freezers Watanzania watakaoshirikina na wageni majokofu matano na “freezers” tano, huku Watanzania wanaomiliki kampuni peke yao ni angalau majokofu 2 na freezers 2.
Mheshimiwa Rais, nimeshindwa kupata mantiki ya kuwa kwa yale makampuni yanayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 ,wao endapo inatokea kwamba mwombaji hana vifaa vilivyotajwa hapo juu, atawajibika kuonyesha dhamana ya benki yenye kiasi kisichopungua Dola za Marekani 300,000.00 ndani ya miezi mitatu (3) baada ya kufanyiwa ukaguzi (Due diligence) na kupitishwa kugawiwa kitalu ili kuhakikisha kwamba vifaa hivyo vinaweza kununuliwa. Na kwa yale makampuni yanayomilikiwa na Watanzania kwa ubia na wageni wao watapaswa Pale inapotokea kwamba mwombaji hana vifaa vilivyotajwa hapo juu, atawajibika kuonyesha dhamana ya benki yenye kiasi kisichopungua Dola za Marekani 1,000,000.00 ndani ya miezi mitatu (3) baada ya kufanyiwa ukaguzi (Due diligence) na kupitishwa kugawiwa kitalu ili kuhakikisha kwamba vifaa hivyo vinaweza kununuliwa. Hoja yangu hapa ni kuwa je? Dola laki tatu zinatosha kununua magari 2, majokofu 2, freezer 2, jenereta 2, mahema 6,bunduki za kuwindia, na vinginevyo kweli ? ama hapa kuna mkakati wa kuikosesha serikali mapato kwa kutumia kivuli cha uzawa!
Mheshimiwa Rais,masharti haya yanaonyesha kuwa tunamtegemea mtanzania kuwa na vifaa duni na hivyo uzalishaji wake utakuwa duni na hata bidhaa zitakuwa duni na hivyo kutokupata soko lenye viwango vinavyotakikana na kulikosesha taifa fedha za kigeni.Hivi huku ndio kumjenga mtanzania au ni kumfanya ashindwe kushindana na wawekezaji wa kigeni? Kwanini tusiwahamasishe watanzania kuingia ubia ili waweze kupata mitaji ya uhakika na hatimaye kuweza kushindana kwenye soko kikamilifu? Magari mawili haya yatakuwa ni kwa ajili ya ulinzi wa kuzuia majangili ama ni kwa ajili ya kufanya shughuli za uwindaji?
Mheshimiwa rais, hivi kama nikipewa kitalu na kuamua kutafuta wageni ambao nitaingia nao ubia ili waweze kuendesha biashara yangu ninakosa haki za kuendelea kuwa mtanzania? Jambo hili linafikirisha sana Mhe.rais. hivi waziri anajua kuwa Tanzania tunao wawindaji wataalamu (Professional hunters) wanaokadiriwa kuwa 45 tuu na ambao wana uzoefu? Hawa wengine watatoka wapi kama hatutaki kushirikiana na wageni?
Mengine yanayohitajika.
Mheshimiwa Rais , biashara hii inahitaji mitaji mikubwa, ujuzi pamoja na vifaa mbalimbali kama vile bunduki za kisasa zenye kipenyo cha kuanzia 200mm-500mm na haswa kwa uwindaji wa wanyama wakubwa kama Nyati na Tembo ,ndege kwa ajili ya kufanya doria kwenye vitalu ili kuhakikisha kuwa majangili hayawezi kuingia na kuua wanyama ambao hawapaswi kuuwawa kama vile wanyama majike ama hata ambao umri wa kuweza kuvunwa kisheria haujafika .
Biashara hii inahitaji wataalamu wafuatao kwa ajili ya kuweza kuifanikisha kama vile wawindaji wajuzi (Proffessional Hunters),wawindaji wenye ujuzi wa kuweza kutambua umri wa mnyama na haswa wanapokuwa wanyama kama simba ambao anapaswa kuwindwa akiwa amezeeka yaani mwenye miaka saba na kuendelea,Nyati anapaswa awe na pembe zenye urefu wa futi 40 na kuendelea na ili kuweza kutambua hilo kunahitajika vifaa maalum kama vile darubini na vinginevyo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Kunahitajika pia vifaa kwa ajili ya kuweza kutambua idadi ya wanyama waliopo kwenye kitalu husika na hivi ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mwenye kitalu anaweza kutambua idadi ya wanyama waliopo na wakati wa kuweza kuvuna wanyama hao.
Mheshimiwa rais , pia kunahitajika uwekezaji maalumu wa kujenga njia za ndege (air strips) ili kuhakikisha kuwa ndege zinaweza kutua kwenye kitalu husika kwa ajili ya ama kufanya doria au hata kubeba mazao yatokanayo na wanyama husika.Ni hakika kuwa vifaa vyote hivyo vinahitaji uwekezaji mkubwa na mitaji mikubwa .Hapa bado sijazungumzia yale maeneo yenye vitalu ambavyo lazima mweye kitalu awe na boti kwa ajili ya usafiri kwani huko kumezungukwa na mamba na hakuna barabara! Sijui hili kama Maige analifahamu na kama ndio mbona hakuliweka kama mojawapo ya kigezo cha mtu kuwa nacho?
Mheshimiwa Rais,naomba kukukumbusha ya kuwa historia hapa duniani inaonyesha kuwa mataifa yafuatayo ndiyo yenye historia ya kufanya uwindaji wa kitalii nayo ni Marekani,Urusi,Uingereza, Uhispania , Uitaliano na Afrika ya Kusini. Hivyo kutokana na mataifa haya kuwa kwenye biashara hii kwa muda mrefu kumeyafanya mataifa haya kuwa na ujuzi katika kuendesha biashara hii kuliko mataifa mengine yaliyosalia.
Naomba nisikuchoshe na maelezo marefu na haswa kwenye kipengele hiki cha nini kinahitajika ili mtu aweze kuwekeza kwenye biashara hii ya uwindaji wa kitalii na naomba sasa nihamie kwenye kipengele kingine .
Muda uliowekwa wa kumiliki kitalu.
Mheshimiwa rais hapa napo kuna kizungumkuti kikubwa kwani muda wa kumilikishwa kitalu ni miaka 5 tuu, sasa kama mwekezaji anaambiwa kuwa atamiliki kitalu hicho kwa kipindi cha miaka 5 na utaalamu unaonyesha kuwa Simba ili aweze kuvunwa anapaswa kufikisha umri wa miaka 7 hadi nane, kuna mwekezaji atakuwa tayari kuhakikisha kuwa anawalinda wanyama hawa kweli ama kila mmoja atawinda kutokana na kukimbizana na muda? Nani atakuwa tayari kuwekeza fedha na mtaji kwenye kitalu wakati anajua kuwa vitagawanywa na yeye atakuwa hajarejesha fedha yake ! Nani atakubali tena kujenga njia za ndege kwa fedha yake wakati anajua baada ya muda njia hizo kutakuwa hakuna hata ndege za kupita humo? hili nalo linafikirisha Mheshimiwa!
Hali ilivyo kwenye sekta hii .
Mheshimiwa Rais kutokana na utafiti ambao nimeweza kuufanya ni kuwa maeneo yenye vitalu yana matatizo yafuatayo ;
- Hakuna mpango wa matumizi ya ardhi (Wildlife Management Plan) wa jinsi ya kutunza maeneo hayo na hivyo hilo limepelekea kila mwenye kitalu kuwa na mpango mkakati wake kwenye kitalu anachokimiliki.Pamoja na ukweli kuwa sheria inamtaka mkurugenzi mkuu wa Wanyamapori kutengeneza mpango huu lakini mpaka leo mpango husika haujatengenezwa.
- Wakati wa uwekaji mipaka ya vitalu vigezo vimekuwa havizingatiwi katika kuweka mipaka baina ya kitalu kimoja na kingine kama vile kuzingatia kuwa upatikanaji wa maji badala yake mipaka imekuwa inawekwa tuu kama mtu anayegawa eneo la ardhi bila kujali kuwa kunahitajika utaalamu mahususi kuhusiana na tabia za wanyama.
- Mazingira ya kuishi wanyama kama vile Simba , kwa mfano kitaalamu ni kuwa simba mmoja dume huwa anaishi na kuweka mipaka kwenye eneo la kilomita za mraba 10 na hivyo kitalu chenye eneo la kilomita za mraba 1000 kina uwezo wa kuwa na Madume 20 tuu ya simba . Hii maana yake ni kuwa muwindaji anapaswa kuwa na eneo kubwa ili aweze kuwa na wanyama wa kutosha na hiki ndio kitamfanya mwekezaji kuwa na uhakika wa fedha ambazo anawekeza.
- Miundombinu ya kuweza kufikia maeneo ya uwindaji , na hii inatokana na ukweli kuwa barabara zetu bado zina hali mbaya na hivyo mara nyingine kuwalazimu wawekezaji hawa kuamua kutengeneza barabara kwenye vitalu vyao ili waweze kuwinda wanyama.
- Tunapoteza fedha nyingi sana kwa kutokujua ama kwa makusudi kwani wakati package ya safari ikiwa inawekwa kwa mafungu matatu yaani siku 7,siku 14 na siku 21 na hii ni kulingana na aina ya wanyama ambao muwindaji anahitaji , serikali imekuwa ikikusanya dola 800 kwa siku wakati makampuni haya yamekuwa yakitoza kati ya ($5,000-10,000) kwa kila safari ya uwindaji, hii maana yake ni kuwa kwa safari ya siku kumi na nne serikali inapata dola 11,200, wakati makampuni haya yanapata kati ya $70,000- 140,000) na fedha hizi zinabakia nje ya nchi kwani zinalipwa huko huko. Mheshimiwa hili lipo kwenye tovuti za makampuni haya na ukitizama utashangaa! Naomba hili nalo ulifikirie kwani linatufanya sote tuonekane kama wendawazimu!
Ushauri wangu kwako .
- Simamisha ugawaji wa vitalu hadi hapo sheria hii itakapofanyiwa marekebisho, na hili lifanyike kwenye Bunge la mwezi Novemba kwa kuhakikisha kuwa vipengele vyote vinavyokinzana na vile vyenye ubaguzi vinaondolewa ,kwa njia hii hatutakuwa tumepoteza chochote kwani tunagawa leseni kwa ajili ya uwindaji kuanzia mwaka 2013-2018 , hivyo hatutachelewa.
- Mwelekeze waziri Maige arekebishe kanuni na kuhakikisha kuwa badala ya watanzania kuwa wanamiliki asilimia 25 tuu ya hisa basi wawe wanamiliki asilimia hamsini (50% ) kwenye makampuni yenye ubia. Hii itahakikisha kuwa watanzania wanakuwa na umiliki zaidi.
- Utengenezwe mpango wa matumizi ya ardhi kwenye vitalu hivi na kila mwenye kitalu awajibike kuutekeleza na huu ufanywe kabla ya vitalu hivi kuanza kufanya kazi na atakayeshindwa kuufuata anyanganywe leseni mara moja.
- Uteuzi wa wajumbe wa kuingia kwenye kamati ya ugawaji vitalu ufanywe kwa kutumia mchakato wa wazi na sifa mahususi ziainishwe na pia wanaojihusisha na biashara hii wawe walau na mjumbe mmoja kwani wataweza kutoa ushauri wa uhalisia wa shughuli yenyewe.
- Sheria irekebishwe na kuongeza viwango vya malipo kutoka dola 800 kwa siku hadi kuwa dola 2000 kwa siku na viwango hivi viwe vinarekebishwa kila mwaka.
- Rekebisha sheria ili taratibu za Mikataba ya Vitalu vya Uwindaji iwe ni kwa ushindani wa wazi baina ya makampuni na mwenye kuongeza bei aweze kupata kitalu na sio kama utaratibu wa sasa ambao waziri anaamua nani apewe na apewe wapi , Ni kanuni ya msingi ya kiuchumi kwamba ushindani wa wazi uwepo kati ya wanunuzi kwa kununua bidhaa kufuatia maamuzi ya soko kwa bei nzuri na sahihi ya bidhaa. Pia ikumbukwe kuwa katika Sheria ya Manunuzi ya Tanzania inasema raslimali za umma lazima zipatikane kwa mfumo wa uwazi na mfumo wa zabuni. Ajabu, raslimali ya wanyamapori imekuwa tofauti na sheria na hii ni hasara kwa uchumi wa nchi.Utaratibu kama huu uliwasaidia sana Zimbabwe kwani Ada ya pembe ya ndovu nchini Zimbabwe iliongezeka kutoka dola za kimarekani 1,200 (TZS 1.4) mwaka 1984 hadi dola za kimarekani 9,000 (TZS milioni 10.8) mwaka 1999 kama matokeo ya soko shindani na wazi ambalo lilichochea bei kupanda.
- Rekebisha sheria ili Kujenga ubia wa muda mrefu unaochochewa na utendaji kati ya serikali na sekta binafsi ikiwa na ufuatiliaji wa uwazi na tathmini kulingana na vigezo vilivyowekwa na hili litayafanya makampuni kuhifadhi na kulinda maeneo yao kwani watakuwa wana uhakika juu ya uwekezaji wa mitaji yao (security of capital).
- Kuwianisha uwindaji wa kitalii na utalii wa picha. Uwindaji wa kitalii na utalii wa picha ni njia mbili tofauti lakini zote ni muhimu kiuchumi na kifedha kwa kuzalisha maduhuli na uwekezaji dhidi ya wanyamapori. Uwindaji wa kitalii huleta ada kubwa kutoka kwa mgeni; Wakati utalii wa picha ambao hata ni ghali, wenye malazi katika makambi ya hadhi ya juu na hoteli hauwezi kuleta fedha zinazolingana na zile za uwindaji wa kitalii. Hata hivyo, uwindaji unaweza tu kuchukua idadi ndogo ya wateja katika eneo husika kila mwaka kwa sababu wanyama wanaoweza kuwindwa kiutaratibu ni wachache na hivyo kundi moja tu la wateja laweza kuwinda eneo moja kwa wakati moja. Kiyume chake, utalii wa picha unaweza kupokea wateja wengi na zaidi ya maelfu ya watu wanaweza kuona na kupiga picha simba mmoja ndani ya Serengeti, wakati ni mwindaji mmoja anayeweza kupiga simba katika kitalu cha uwindaji ndani ya Selous.
Utalii wa picha una bei ya chini lakini una mauzo makubwa kuliko uwindaji. Tofauti nyingine ni kwamba utalii wa picha huhitaji miundombinu zaidi - kama barabara, makambi, hoteli - wakati uwindaji wa kitalii huweza kufanyika mahala ambapo hakuna miundombinu ya kudumu. Utalii wa picha, kwa sababu huhusisha wageni wengi, huvutia uwekezaji, ajira na mapato kupitia huduma mbalimbali.
Hitimisho.
Naomba kuhitimisha barua yangu kwa kukutakia afya njema na hekima ili uweze kuangalia jambo hili kwa kina kwani linahatari kubwa huko mbeleni kama likiachwa liende linavyoendeshwa .Najua wapo watakaokuambia kuwa Tanzania tuna wanyama wengi kuliko nchi nyingine yeyote Afrika na hivyo lazima wawindaji watakuja tuu hata kama tukiweka masharti ambayo ni magumu sana na hayavutii uwekezaji kwenye sekta hii.
Ila ukweli ni kuwa kuna tishio la mitaji kuweza kuhamishwa kutoka kwetu na kuelekezwa kwenye nchi nyingine kutokana na uwepo wa wanyama na haswa nchi kama vile Ethiopia ambao mtawanyo wa aina za wanyama ni72species,Sudan 76 species,Zambia 39 species na sisi ni 70 species.
Bado kuna washindani wetu wa asili kama Botswana, Namibia, Msumbiji,Afrika ya kusini na wengineo wengi.Tutaweza kushindana tuu kama mazingira yetu yatakuwa bora zaidi na yanavutia mitaji zaidi .
Mheshimiwa rais, kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha na nategemea kupata majibu kutoka kwako.
Abdalah Suleiman,
Mwanza-Tanzania.
E-mail abdalah.suleiman@yahoo.com
No comments:
Post a Comment