Monday 21 March 2011

LIBENEKE LA KATIBA MPYA

Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda

Vuguvugu la kudai katiba mpya linazidi kupamba moto sasa Tanzania, kila Sehemu watu wanadai katiba mpya, tayari chama cha wananchi CUF kimefanya maandamano yaliyoongozwa na kaimu katibu mkuu Julius Mtatiro lengo kuu la maandamano hayo ni kuitaka serikali kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuandika katiba mpya ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania, wakati huohuo chama cha wafanyakazi Tanzania maarufu kama TUCTA kupitia kwa katibu mkuu wake Nicholas Mgaya tayari kimeshatangaza kuwa swala la mabadiliko la katiba ni la lazima na kwa upande wa CHADEMA tayari na wao wameshatangaza kupitia kaimu katibu mkuu wake John Mnyika kuwa ni lazima serikali ikubali kubadili katiba pia hali ipo hivyohivyo kwa viongozi wa dini nchini ambao kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakisema kwa msisitizo kuwa katiba tuliyonayo imepitwa na wakati ni muhimu kwa serikali kuridhia mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.

Siku kadhaa nyuma wakati vuguvugu hili linaendelea kushika kasi waziri mkuu Mizengo Pinda alifanya mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika kile kilichoonekana ni kama kujibu madai hayo ya katiba mpya. Katika majibu yake waziri mkuu alidai kuwa atamshauri rais Kikwete aunde jopo la wataalamu kwa ajili ya kazi hiyo ya kuipitia katiba iliyopo na kisha kuandika rasimu ya katiba mpya na kweli haukupita muda rais Kikwete akaweka bayana azma yake hiyo ya kuunda jopo la wataalamu.

Uchambuzi wangu wa leo umejikita katika kuyachambua majibu ya waziri mkuu na kisha kueleza ulazima wa katiba mpya na jinsi ya kuipata katiba hiyo kwa misingi ya hoja ili hata ikibidi kujibiwa nijibiwe kwa misingi ya hoja hivyohivyo.

Kwanza waziri mkuu anapaswa kutambua kuwa katiba tuliyonayo sasa haikidhi mahitaji ya sasa, naomba nieleweke kuwa katiba tuliyonayo sasa licha ya kufanyiwa mabadiliko mengi bado ina mikanganyiko mingi tu na ni ukweli ulio wazi kuwa katiba hii ya sasa ilifaa kwa kipindi kile cha chama kimoja sio sasa ambapo tunataka kujenga taifa la watanzania wote ambapo hatutakuwa na chama tawala tena bali chama kinachoongoza na hatutakuwa na vyama vya upinzani bali vyama mbadala.

Pili waziri mkuu inbidi ajue kuwa wanaodai katiba mpya sio vyama vya upinzani bali ni watanzania wote wakiwemo wana CCM wenzake hivyo kwa misingi ya kidemokrasia kama tunavyojinadi kuwa tunajenga taifa la kidemokrasia ni lazima sauti hii isikilizwe kwa umakini mkubwa.

Tatu waziri mkuu ni lazima akiri udhaifu wa katiba iliyopo na aonyeshe waziwazi kuwa haitufai tena kwasababu kwanza ikumbukwe kuwa hii tunayoiita katiba ya kudumu ya mwaka 1977 iliandikwa na tume ya Thabit Kombo ambayo pia ndio iliandika katiba ya Chama cha CCM, kwa hali ya kawaida tu tayari kumbe katiba hii haikuandikwa na watanzania bali wanazuoni wa chama tawala CCM.

Nne waziri mkuu inabidi ajue kuwa hata tunayoyaita maboresho kwenye katiba hii yana walakini kwasababu mengi yameongozwa na matukio na sio mitazamo , maboresho hayo aidha ni matokeo ya mnyukano na misigano ya kisiasa au kijamii ambayo yalipeleka hoja bungeni ya kufanya mabadiliko ya katiba na ni mara chache sana mabadiliko haya yametokana na watanzania kuchukua tahadhari kwa kufahamu kwao jambo Fulani lililopo kwenye katiba au lisilokuwepo kwenye katiba.

Tano ni logic ya kawaida kuwa hata tukifanya maboresho ni kazi bure ikizingatiwa kuwa tayari mwaka 1991 tume ya Jaji Francis Nyalali ilishatoa mapendekezo mbalimbali kuhusu katiba lakini kwasababu tume hiyo haikuwa na meno kwa maana iliteuliwa na rais haitokana na Bunge basi serikali ilchagua mapendekezo iliyofurahishwa nayo na mengine yakaachwa bila kutekelezwa.

Hivyo nitoe wito kwa Mizengo Pinda ajue kuwa watanzania sio mashabiki wala wafata mkumbo bali ni waelewa na wamedhamiria na kweli wanahitaji katiba mpya na kama wanahitaji katiba mpya basi kwa mantiki ya kawaida tu maana yake iliyopo sasa haikidhi mahitaji kwa hivyo kuna ulazima wa dhati.

Hivi waziri mkuu yeye haoni umuhimu wa kuliacha Bunge liteue tume huru itakayoandaa mapendekezo ya jinsi gani kila mtanzania atashiriki katika katiba mpya? ikizingatiwa kuwa sasa watanzania wana uelewa mkubwa wa mambo ya kiraia na kisiasa pia utawala tofauti na kipindi cha nyuma. Haoni kwamba kuunda jopo la wataalamu ni kuwanyima haki watanzania kushiriki tukio hili muhimu? Haoni kuwa mwisho wa siku kuna hatari Ya mapendekezo hayo ya jopo la wataalamu au tume ya kuteuliwa ya rais yakatupwa kapuni kama yale ya mwaka 1991?

Au tuseme kuwa Mizengo Pinda haoni mikanganyiko iliyopo kwenye katiba yetu inayohitaji sio ufumbuzi tu bali ufumbuzi wa wazi utakaoshirikisha wananchi wote sio jopo la wataalamu pekee?

Yeye haoni kuwa sisi tunaushangaza ulimwengu kwa kushindwa kuuweka Muungano wetu sawa ukaeleweka ni wa mfumo upi? Kwa maana hali ilivyo sasa ni kama serikali ya Tanganyika haipo tena bali kuna serikali mbili yaani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, yeye haoni kuwa tumekosea hesabu kwani tangu lini moja na moja ikazaa moja na nusu na sio mbili kamili? Kwanini tusiwe na serikali mbili zenye meno kuliko kuwa na serikali moja huku nyingine ikiwa ni nusu serikali kwa kuzidiwa nguvu na nyingine?

Ina maana Mizengo Pinda haoni athari za kizungumkuti cha itikadi tulionao? Huku katiba yetu ikidai sisi ni wajamaa na watanzania wakiimba ujamaa ilihali tumekumbatia ubepari. Ina maana waziri mkuu haoni kuwa kama taifa tunahitaji kujipambaua kupitia katiba kuwa sisi ni wajamaa au wabepari?

Ikumbukwe kuwa historia inaonyesha kuwa Mwalimu Nyerere mwenyewe amewahi kuongelea udhaifu wa katiba yetu akidai kuwa katiba hiyo inampa mamlaka makubwa rais kiasi kwamba akiamua kutumia madaraka hayo kwa ukamilifu atakuwa ni mtawala wa kimla au rais dikteta, ina maana yeye waziri mkuu Mizengo Pinda haoni umuhimu wa kuanza kumpunguzia madaraka rais kwa kuliacha bunge litunge tume huru ya kusimamia na kuandaa mapendekezo ya kitaalamu jinsi ya kuendesha mchakato wa kuandika katiba mpya badala ya kumwacha rais huyohuyo kuunda jopo la wanaoitwa wataalamu ambalo mwisho wa siku kuna hatari jopo hilo likafanya kazi kwa misingi ya kujipendekeza na kujijengea taswira njema kwa rais na sio kwa nia njema kwa manufaa ya taifa zima.

Hii tisa kumi ni hii tume yetu ya uchaguzi ambayo naweza kusema kuwa kutokana na tume hii kutokuwa huru basi ni moja ya sababu kubwa ya vurugu kila inapofika wakati wa uchaguzi , Mizengo Pinda anapaswa afahamu kuwa ni lazima watanzania wote washiriki kuandaa katiba mpya tena katika hali ya uwazi na sio jopo la wataalamu wa kuteuliwa ili kuondoa utata kama huu wa tume ya uchaguzi ambayo kuna baadhi wameanza kudiriki kuiita tume ya uchafuzi kutokana na tuhuma nyingi zinazoikabili tume hiyo hasa zinazohusiana na kile kinachoitwa tabia ya kuchakachua kura ili kukibeba chama tawala.

Mwishowe nitoe ushauri kwa mheshimiwa waziri mkuu Mizengo Pinda kuwa yeye kama mtendaji mkuu wa serikali inabidi aliunge mkono wazo hili kwani ni la kizalendo la utaifa na linalenga kukuza demokrasia ya nchi yetu kwa maana swala hili la katiba mpya limetokanana watanzania kwa ridhaa yao wenyewe wamekusudia kulifanya tena kwa nguvu, juhudi na maarifa yao wenyewe wanataka kuona nchi yao ikipata katiba mpya nzuri ambayo imetokana na watu wote hili si jambo la kubeza hata kidogo ni jambo la kujivunia kuwa watanzania sasa wamedhamiria kwa dhati kuwa nakatiba inayokidhi mahitji yao ya sasa.

Hivyo basi Mizengo Pinda anapaswa kuwa kinara katika hili ili kuweka misingi imara ya taifa hili na kamwe historia haitamtupa atakumbukwa milele na wana wa taifa hili kuliko hiki anachotaka kukuifanya cha kumshauri rais kuunda jopo la wataalamu ambalo mwisho wa siku tutarudi kulekule tulikotoka ambapo kuna hatari ya kuwa na katiba yenye maboresho zaidi yahamsini kweli hata nguo ikiwekwa viraka hamsini itavalika tena? Nani ana ujasiri wa kuvaa nguo yenye viraka hamsini? Bila shaka hakuna vivyo hivyo si jambo jema kuwa na katiba yenye maboresho mengi hebu wa Tanzania tuzinduke muhali wa haya yote ni kuwa na katiba mpya inayotokana na watanzania wote linalowezekana leo tusingoje kesho tuanze sasa tuanze leo bila kusita………..Alluta continua


Nova Kambota Mwanaharakati,
0717-709618 au 0766-730256
novakambota@gmail.com
Pia usikose kunitembelea www.novatzdream.blogspot.com
Mbeya Tanzania East Africa
21 March 2011

No comments:

Post a Comment