Wednesday, 23 March 2011

WAZIRI MAIGE AHIMIZA ULINZI WA MALISILI MKOANI RUKWA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Ezekiel Maige

Watu waliovamia maeneo ya hifadhi za Maliasili katika mkoa wa Rukwa wametakiwa kuondoka kutoka kwenye hifadhi hizo ifikapo tarehe 31 Julai 2011 Muda huo umewekwa ili wahusika waweze kuvuna mazao waliyopanda hifadhini.

Hayo yalisemwa Jumatatu na Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Ezekiel Maige alipokuwa anatoa majumuisho kwa viongozi wa mkoa wa Rukwa baada ya kufanya ziara ya siku kumi katika mkoa huo kukagua shughuli za uhifadhi zinazosimamiwa na wizara yake.

Katika ziara hiyo ambayo ilikuwa rasmi ya kutembelea mkoa huo, Waziri Maige aligundua kuwa misitu ya hifadhi na mapori ya akiba yaliyoko mkoani Rukwa yameathiriwa na shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji, na utengenezaji mkaa.

Pamoja na hayo, kwa kuwa kuna vivutio vingi mkoani Rukwa Waziri Maige aliutaka Mkoa wa Rukwa kutengeneza Mpango Mkakati wa Kuendeleza Utalii na kuwa Wizara yake itashiriki katika utekelezaji wake.

Wanyamapori

Katika sekta ya wanyamapori Waziri Maige alibaini kuwa kwa sasa ulinzi wa mapori ya akiba ni hafifu ndiyo maana kuna uvamizi katika maeneo hayo, kama vile mapori ya akiba ya Uwanda na Rukwa-Lukwati. Ili kukabiliana na hali hiyo Waziri aliagiza kuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori afanye utafiti kujua ukubwa wa tatizo hilo ili ijulikane ni mifugo kiasi gani wamo ndani ya mapori, pia ni eneo gani limelimwa mashamba.

Sambamba na hilo Waziri aliutaka uongozi wa mkoa kutafuta eneo jingine kwa ajili ya kuwahamishia watu waliovamia mapori hayo. Aliagiza kuwa elimu kuhusu Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 itolewe kwa wahusika wakati wakisubiri kuhama. Alisisitiza kuwa wahusika wataruhusiawa kuvuna mazao waliyopanda ndiyo maana wamepewa muda hadi tarehe 31 Julai mwaka huu wa kujiandaa kuhama.

Maamuzi mengine aliyotoa Waziri Maige ni kuhusu kuimarisha usimamizi wa Pori la Akiba la Rukwa-Lukwati kwa kuyatenganisha mapori hayo ili kila pori lijitegemee. Hivyo aliagiza kuwa Makao Makuu ya pori hilo yajengwe sehemu nyingine muafaka.

Utekelezaji wa agizo hilo utaleta tija maana watumishi watakuwa karibu zaidi na maeneo yao ya kazi kuliko ilivyo hivi sasa. Waziri pia aliagiza kuwa Meneja wa pori hilo la Rukwa-Lukwaji Bwana Ladislaus Rwelamila ahamishiwe sehemu nyingine ili aje mwingine ambaye ataimarisha shughuli za uhifadhi.

Halikadhalika, Waziri Maige aliagiza kuwa kituo cha Mlele ambacho ni makao Makuu ya Pori hilo yabadilishiwe matumizi ili yatumike kwa shughuli nyingine ya Wizara ambayo itakuwa ya manufaa zaidi. Aliitaka Idara ya Wanyamapori na TANAPA kuhakikisha kuwa agizo hilo linatimizwa ifikapo mwaka 2015.

Waziri Maige pia alilitaka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kufanya utafiti katika mto Katuma ulioko katika hifadhi ya Katavi ili hatua zichukuliwe kuhakikisha kuwa wanyama hususan Viboko wanapata maji ya kutosha mwaka mzima. Akiwa ziarani Waziri Maige alijionea upungufu wa maji katika sehemu wanakokaa wanyama hao.

Halikadhalika, Idara ya Wanyamapori na TANAPA waliagizwa wafanye utafiti wenye nia ya kuipanua Hifadhi ya Katavi kwa kujumuisha Pori la Akiba la Lwafi na Msitu wa Hifadhi wa Nkamba. Taarifa ya utafiti huo iwe tayari ifikapo mwezi Julai 2013 tayari kwa utekelezaji.

Misitu na Nyuki

Kwa upande wa sekta ya Misitu na Nyuki Waziri Maige aliuomba uongozi wa mkoa kuendelea kuwaelimisha wananchi wa mkoa wa Rukwa kuilinda misitu iliyopo mkoani humo. Aidha aliutaka mkoa kukamilisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ili wananchi waweze kujua fika sehemu zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza maliasili na shughuli zingine mbalimbali.

Kwa upande wa ufugaji nyuki Waziri Maige aliahidi kukipatia mizinga mia moja kikundi kiitwacho Miti na Mazingira Kibaoni (MIMAKI) kilichoko kijijini Kibaoni wilayani Mpanda.

Mizinga mingine hamsini watapewa wananakikundi wa kijiji cha Kapozwa kilicho wilayani Sumbawanga baada ya kuelimishwa na mtaalam wa ufugaji nyuki kutoka makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Utalii

Kwa upande wa sekta ya Utalii Waziri Maige alivutiwa na maporomoko ya mto Kalambo yaliyoko katika kijiji cha Kapozwa kilichoko wilayani Sumbawanga. Alisema hicho ni kivutio ambacho kinatakiwa kuendelezwa kama sehemu ya kuendeleza utalii katika mkoa wa Rukwa.

Waziri Maige aliiagiza Idara ya Utalii itoe shilingi milioni ishirini kwa ajili ya kutengenezea ngazi na sehemu mbalimbali muhimu katika maporomoko hayo. Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga nayo itakarabati sehemu ya mwisho ya barabara inayoelekea katika maporomoko hayo

Kwa kuzingatia umuhimu wa Msitu wa Kalambo katika kuhifadhi sehemu hiyo Waziri Maige aliahidi kuwa Wizara yake itatoa vitendea kazi ambavyo vitatumiwa na wataalam wawili ambao ni waajiriwa wa Halmashauri ambao watapangiwa Kalambo kama kituo chao cha kazi.

Malikale

Kwa upande mwingine Waziri Maige aliiagiza Idara ya Mambo ya Kale iliyoko chini ya Wizara yake kuorodhesha maeneo yote ya Malikale yaliyoko mkoani Rukwa ambayo ni vivutio vya utalii. Aliiitaka Idara hiyo kuyafanyia ukarabati maeneo hayo ikiwemo ngome ya Bismark ambayo ilitumika enzi za utawala wa Wajerumani.

George Matiko

MSEMAJI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

23 Machi 2011

Simu: 0784 468047

No comments:

Post a Comment