Friday 25 March 2011

Serikali yaomba baraka za Mchungaji Loliondo

Foleni ya leo Loliondo

KIKAO cha kutafuta njia bora ya kuwawezesha wananchi kupata tiba ya magonjwa sugu huko Loliondo kilichoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na viongozi wa mikoa sita wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Isdore Shirima na mwenzake wa Mara, Enos Mfuru kimeahirishwa katika kile kinachoaminika kuwa ni hadi pale maazimio yake yatakapopata baraka za Mchungaji Ambilikile Mwasapile.

Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kuahirisha kikao hicho saa 3:35 usiku kuwa bado kuna mambo ya kujadiliwa kabla ya kutoa tamko rasmi.
“Kikao kimeahirishwa tumepeana majukumu, kesho Mkuu wa Mkoa wa Arusha atakuwa Loliondo kuongea na Mchungaji Ambilikile Mwasapile na kujionea hali ilivyo kwa sasa na wengine wamepewa majukumu mengine, hivyo kesho (leo) tutakuwa na la kuwaambia baada ya RC kurudi," alisema.


Kwa siku nzima viongozi hao walikuwa katika Ukumbi wa Ofisi namba 40 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, wakijadili hali ilivyo huko Loliondo hasa baada ya mvua kuanza kunyesha na kusababisha msongamano mkubwa magari.


Mbali ya viongozi hao, mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Manyara na Shinyanga, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na vingozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati.


Habari zilizopatikana baada ya kikao hizo zinasema Serikali inakusudia kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mahema ya kutosha ambayo yatakodishwa kwa wananchi wanaokwenda huko.


Pia Serikali imerejea ahadi iliyoitoa wiki kadhaa zilizopita ya kuandaa utaratibu wa kuwasaidia wagonjwa waliozidiwa kupata huduma haraka kwa kutumia gari la kubebea wagonjwa (ambulance) ambalo kwa sasa limeshindwa kufanya hivyo kutokana na baadhi ya watu kudai gari hilo linatumika kuwabeba vigogo badala ya wagonjwa wenye hali mbaya.

Taasisi yajitokeza kujenga vyoo, mahema

Taasisi ya kimataifa ya masula ya mazingira ya Solar Oven Society Africa, imetangaza mpango wa kuokoa maisha ya watu na uharibifu wa mazingira katika barabara iendayo Kijiji cha Samunge kwa kutoa vyoo na gari la kubeba wagonjwa.


Akizungumza na Mwananchi jana, Mwakilishi wa Taasisi hiyo hapa nchini, Profesa Solomon Mwenda alisema wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa kuna tatizo la huduma muhimu kwa wagonjwa na uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo hilo ambalo pia ni mapito ya wanyamapori.

“Tumekwenda Samunge na tumeona hali ni mbaya sana na ni hatari kwa afya za watu. Tumekuta bado watu wanajisaidia porini, bado chupa tupu na uchafu mwingi unatupwa barabarani hovyo,” alisema Profesa Mwenda.

Alisema kazi ya vyoo itaanza Jumanne ijayo na kwamba kila baada ya kilometa moja kutakuwa na choo cha muda.

Pia watatoa gari la kubeba wagonjwa, mifuko ya kutunza taka, mahema na maofisa wa mazingira.
Mpaka sasa hakuna hata choo kimoja kilichokamilika kujengwa wakati Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imekuwa ikivuna kiasi cha Sh 6.4.milioni kwa siku katika Kijiji cha Samunge.

Tayari halmashauri hiyo imetia kibindoni kiasi cha Sh 140.8 milioni kwa mwezi mmoja lakini hivi sasa kuna taarifa ya mgonjwa mmoja kuhara damu, kwa mujibu wa ripoti kutoka zahanati ya kijiji jicho.


Pato hilo linatokana na tozo la ushuru wa kila siku kwa magari yanayokwenda kwa Mchungaji Mwaisapile kwa ajili ya kupata tiba.

Mabasi makubwa na malori yanatozwa Sh10,000 kila moja, mabasi madogo yanatozwa Sh5,000 na madogo Sh2,000 huku pikipiki zikitozwa Sh1,000.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka kijijini hapo pamoja na pato hilo ambalo awali lilikuwa likikusanywa na kijiji hicho hali bado ni mbaya na uchafu umekidhiri kila mahali vinyesi, mikojo katika chupa za plastiki ni hali ya kawaida eneo hilo .

Hali inazidi kuwa mbaya kiafya kutokana na mvua ziloanza kunyesha huku misururu mirefu inayofikia umbali wa kilomita 28 na watu waoadiriwa kufikia 150,000 wakiwa wanasubiri kupata tiba. Msururu huo unaanzia katika Kijiji cha Mdito.


Wananchi waliokwama katika msururu huo wamekuwa wakihangaika kupata chakula na vinywaji kiasi kwamba kila abiria wanaopita kutoka Kijiji cha Samunge, wamekuwa wakiombwa maji ya kunywa bila kujali kama yametumiwa na wengine au la
Kijiji cha Mdito chenye kaya zisizozidi 50 hivi sasa kina watu wanaokadiriwa kufikia 200,000 ambao hawana mahitaji muhimu kabisa, huku wengine kama hao wakipata walau huduma kidogo na hao ni wale walio katibu na Kijiji cha Samunge, umbali wa kilometa 10.

Wakati huohuo; mvua zinaendelea kunyesha wilayani Ngorongoro hali ambayo inatishia uharibufu wa barabara.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali alisema kuwa kutokana na mvua hizo, ukarabati wa barabara ambao ulikuwa unafanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umesitishwa kwa muda.

“Ni kweli barabara ni mbaya kutokana na mvua, watu wa Tanroads walikuwa wanatengeneza barabara ila nadhani sasa imekuwa kazi ngumu kwani mvua zimewakuta,” alisema Lali.


Tangu kuanza kwa mvua hizo takriban wiki moja sasa, mamia ya watu na magari wamekwama katikati ya Kijiji cha Selela na Ngaresero kutokana na mito kujaa na maeneo mengi kuharibika.


Lipumba aiponda Serikali

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameishukia Serikali kwa kuruhusu tiba hiyo bila kufanyiwa uchunguzi na mkemia wake mkuu.

Profesa Lipumba ambaye hata hivyo, katika maelezo hayo hakuwakatisha tamaa wananchi kwenda kupata tiba hiyo, alisema kiutaratibu, watu hawazuiliwi kufanya tiba, lakini dawa lazima zipite kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili athibitishe ubora wake kabla ya kuruhusu watu waanze kuitumia.


Profesa Lipumba alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Zakheim, Mbagala Dar es Salaam.


"Katiba yetu haizuii mtu kuendesha shughuli za tiba, lakini taratibu ni kwamba tiba lazima ithibitishwe na maabara za Serikali. Ukiona Serikali inawaruhusu watu kutumia tiba bila kufuata utaratibu huo ujue imekwama," alisema.

Ingawa Lipumba hakutaja moja kwa moja tiba ya Loliondo, tiba iliyoanza kutolewa katika siku za hivi karibuni na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii ni ile inayotolewa na Mchungaji Mwasapile.

Profesa Lipumba aliponda uamuzi wa Waziri Lukuvi kushinikiza tiba hiyo itolewe bila vipimo akisema ni sawa na kuhalalisha mambo yaendee kiholela katika nchi ambayo imejiwekea utaratibu wake kisheria.


"Waziri wa afya alikuwa sahihi sana kutaka dawa hiyo ipimwe kwanza, lakini Lukuvi akapingana naye, hii ni dalili mbaya kwa Serikali," alisema.

Habari hii imeandaliwa na Filbert Rweyemamu,
Moses Mashala, Emanuel Herman, Arusha na Kizitto Noya wa MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment