Mkurugenzi wa Clouds Ruge Mutahaba akiongea
Ruge Mutahaba, Shigongo, Juma Mbizo na Abdallah Mrisho wakiwa meza kuu
Toka shoto ni Mbasha, Profesa J, AY, Innocent Galinoma, na mratibu Juma Mbizo
AY, Mrisho Mpoto na Profesa J
AY, Mrisho Mpoto, Profesa J na Innocent Galinoma
Mzee Yusuf na Sauda Mwilima wa Star TVAY, Mrisho Mpoto na Profesa J
AY, Mrisho Mpoto, Profesa J na Innocent Galinoma
Bwana na Bibi Mbasha
Mratibu Juma Mbizo akitoa neno
Innocent Galinoma akiwa katulia
Mzee Yusuf
Kampuni ya Global Publishers ikishirikiana na Clouds Media Group inapenda kuufahamisha umma wa watanzania kuwa wameandaa tamasha la wazi na la bure lililopewa jina la “TAMASHA LA UZALENDO: TANZANIA KWANZA, SISI SOTE NI NDUGU”.
Tamasha hili Kubwa, linatarajiwa kufanyika Jumamosi ya tarehe 26 Machi, 2011 katika viwanja vya Biafra, Kinondoni Dar es Salaam kuanzia, saa 5:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni.
Madhumuni ya tamasha hili ni kuwakumbusha watanzania umuhimu wa kuishi pamoja kwa upendo na amani bila kujali tofauti zao. Vilevile kuwahamasisha kuipenda nchi yao na kupendana kama binadamu na kuweka uzalendo mbele kwa maslahi ya taifa. Tamasha hili linakadiriwa kujumuisha watu kati ya 20,000 hadi 25,000 wa rika tofauti na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa makampuni na taasisi mbalimbali wanaoheshimika na jamii, ambao siyo wanasiasa.
Tamasha linatarajiwa kuvuta watu wengi kutokana na maudhui yake pamoja na kauli mbiu yake ya kuhimiza na kuhamasisha mapinduzi ya kifikra kwa kuwajenga watanzania wawe na uzalendo na moyo wa kupenda nchi yao. Kwa kufanya hivyo, wataweza kuongeza upendo miongoni mwao na hii itasaidia kulinda amani na utulivu tulio nao na tunaojivunia.
Kwa kipindi kirefu sasa, nchi ya Tanzania imekuwa katika vita ya maneno kati ya wanasiasa wanaokinzana na hivyo kwa namna fulani kuathiri watanzania wengi kutokana na misimamo na matamshi yanayowakatisha tamaa wananchi wengi. Tamasha hili litakuwa ni fursa ya kipekee ya kurejesha matumaini kwa kufufua chachu ya kutaka kuwa wazalendo, wenye uchu wa kulinda nchi yetu na kuonesha mapenzi kwa kila kitu kinachohusisha Utanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na vyama.
Ujumbe wa tamasha hili ni muhimu sana kwa kila mtanzania atakayefika pamoja na wale watakaosikia habari zake. Ili ujumbe uweze kufika kwa ufasaaha, kunatarajiwa kuwepo wanaharakati watakaozungumza siku hiyo, wakiwemo Eric Shigongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Joseph Kusaga, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group na wengineo.
Tamasha hili linatarajiwa kusindikizwa na burudani mbalimbali kutoka kwa bendi na vikundi mbalimbali vya sanaa. Kati ya burudani hizo ni muziki wa dansi kutoka kwa bendi za African Stars, Msondo Music Band, DDC Mlimani Park, TOT Band na Stone Mayiyasika. Vile vile kutakuwa na muziki wa taarabu ambapo bendi za Jahazi Modern Taarab na Super Shine Modern taarab zitatumbuiza.
Vijana wakiwa ndiyo kundi kubwa linalowakilisha idadi ya Watanzania wengi, burudani ya bongo flava itakuwepo huku wasanii wengi wakionesha nia ya kushiriki. Miongoni mwa wasanii hao ni pamoja na Profesa Jay, AY, H. Baba, H-Mbizo, wasanii kutoka Zizzou Entertainment, mwimbaji wa injili, Flora Mbasha na wengineo wengi.
Mbali ya wasanii hao, atakuwepo pia mwanamuziki mkongwe wa Reggae, Innocent Galinoma, Mtanzania aishiye nchini Marekani, ambaye amejipatia umaarufu kutokana na nyimbo zake za kizalendo kama vile “Sote ni ndugu” na “Kilimanjaro”.
Juhudi za makusudi zimefanywa na kamati ya maandalizi kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama wa watu na mali zao unakuwa wa kutosha. Vyombo husika vya ulinzi na usalama vimeshapewa taarifa na vinajipanga kuhakikisha tukio hili linakuwa la kihistoria. Vilevile kutakuwa na maninja watakaoongeza nguvu kusaidiana na polisi ili kuhakikisha usalama wa kutosha.
Kamati ya maandalizi ya tamasha inapenda kutoa hamasa kwa watanzania wote kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kula kiapo cha uzalendo. Wananchi watakaohudhuria, si tu watapata fursa ya kupokea changamoto ya kuwa wazalendo na kuishi kwa amani na upendo, bali pia wataburudika na burudani zilizotajwa hapo awali. Vilevile huduma mbalimbali muhimu, kama vinywaji, vyakula, vitatolewa kwa gharama nafuu.
Asanteni,
Mungu awabariki na aibariki Tanzania.
Global Publishers & General Enterprises Ltd
.Clouds Media Group
Juma Mbizo,
Mratibu wa Tamasha.
No comments:
Post a Comment