Saturday, 31 December 2011

SALAM ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA

SALAM ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,

TAREHE 31 DESEMBA, 2011

Ndugu Wananchi;

Leo tunauaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka 2012. Naungana nanyi Watanzania wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na bahati ya kuiona siku ya leo. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakujaaliwa kuwa nasi kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki. Tuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema na sisi tuendelee kumuomba Mola wetu atujaalie rehema na neema tele katika mwaka ujao.

Mapitio ya Mwaka 2011 na Matarajio kwa Mwaka 2012

Miaka 50 ya Uhuru

Ndugu wananchi;

Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa aina yake na wa kihistoria kwa nchi yetu na wenye mchanganyiko wa mambo. Kulikuwa na matukio ya furaha na majonzi na ulikuwa mwaka tuliopata mafanikio mengi na changamoto mbalimbali. Tumeweza kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa heshima stahiki kama nilivyoelekeza katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011. Tumezitumia vizuri sherehe hizo kufanya tathmini ya maendeleo tuliyoyapata tangu Uhuru mpaka hapa tulipo sasa pamoja na kutambua changamoto zilizo mbele yetu.

Hakika tumepata mafanikio makubwa sana katika miaka 50 hii ya Uhuru wetu kuliko yale yaliyopatikana katika miaka 77 ya ukoloni wa Wajerumani (miaka 34) na Waingereza (miaka 43). Pamoja na mafanikio hayo tuliyoyapata bado nchi yetu ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani hivyo bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya mbele yetu. Katika tathmini iliyofanywa na kila Wizara na Idara za Serikali, mambo yanayostahili kufanyika miaka ijayo pamoja na mikakati ya kufikia malengo hayo, yameainishwa vizuri.

Mpango wa Maendeleo

Ndugu Wananchi;

Bahati nzuri, mambo yote yaliyoainishwa kufanywa yanakuwa sehemu ya mambo ya kutekelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 mpaka 2015/2016. Kama mtakavyokumbuka miongoni mwa matukio muhimu katika mwaka 2011 ni kukamilika kwa kazi ya kufanya tathmini ya kuhuisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na kutengenezwa kwa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutekeleza Dira hiyo. Tumejipanga vizuri kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika Bajeti ijayo. Pia nimeunda Kikundi Kazi kinachoongozwa na Prof. Benno Ndulu cha kushauri juu ya vipaumbele na kufuatilia utekelezaji wa Mpango huo.

Ndugu Wananchi;

Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Watanzania wenzangu wote kwa jinsi tulivyosherehekea miaka 50 ya kuzaliwa kwa taifa huru la Tanganyika ambalo sasa ni Tanzania Bara. Tumeikumbuka na kuitukuza ipasavyo siku hii maalum na adhimu kwa nchi yetu. Nawapongeza sana wale wote waliofanya kazi kubwa ya maandalizi ya sherehe zile pamoja na wananchi walioshiriki. Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu katika ngazi yake na dhamana yake atafanya tathmini ya jinsi mambo yalivyokuwa katika maeneo yake ili kujua mafunzo gani amepata. Lengo ni kutambua maeneo ya udhaifu kwa nia ya kurekebisha kasoro zilizopo na yale waliyofanya vizuri kwa nia ya kuimarisha zaidi.

Mchakato wa Katiba

Ndugu Wananchi;

Tukio lingine la kihistoria lililotokea mwaka huu tunaoumaliza leo ni kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba mpya ya nchi yetu. Kama mnavyokumbuka, katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011, niliahidi kwamba tutaanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa lengo la kuihuisha, ili hatimaye tuwe na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne. Azma yetu ni kuwa tusherehekee miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tukiwa na Katiba mpya itakayotumika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.

Kama mnavyofahamu nyote, katika Bunge la Aprili, 2011, Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (2011). Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge liliupitisha Mswada huo na mimi nikatia saini na kuwa Sheria tarehe 29 Novemba, 2011. Sheria hiyo sasa ndiyo inayotoa mwongozo wa namna mchakato wa kupata Katiba mpya utakavyoendeshwa.

Ndugu Wananchi;

Sheria hiyo imeainisha utaratibu wa uundwaji wa Tume ya Kukusanya Maoni ya wananchi wote na jinsi itakavyofanya kazi yake. Aidha, inaelezea namna ya kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba lenye uwakilishi mpana zaidi kuliko Bunge la sasa la Jamhuri ya Muungano. Kazi ya Bunge hilo itakuwa ni kupokea na kujadili Rasimu ya Katiba itakayotayarishwa na Tume ya Katiba. Baada ya Bunge kujadili Rasimu hiyo na kufanya uamuzi wake, Rasimu ya Katiba itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kura ya maoni. Sheria, pia, inaelekeza namna kura ya maoni ya wananchi itakavyoendeshwa na hatimaye kupata Katiba mpya.

Ndugu Wananchi;

Sote tunafahamu maoni mbalimbali na mjadala mkali uliokuwepo baada ya mimi kueleza dhamira yangu ya kuanzisha mchakato wa kufanya mabadiliko ya Katiba yetu wakati Muswada ulipokuwa Bungeni na hata baada ya kupitishwa na kusainiwa kuwa Sheria. Kwa kutambua wajibu wa kusikiliza maoni ya wadau, sikusita kukubali maombi ya kukutana na viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR na Shirikisho la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali. Tulikuwa na mazungumzo mazuri na viongozi wa CHADEMA, CUF na tulielewana juu ya namna ya kushughulikia hatua zinazofuata katika mchakato huu. Nitakutana na viongozi wa NCCR mapema mwezi Januari, 2012.

Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu wote kuwa niko tayari kukutana na kuzungumza na wadau wowote na kupokea mawazo mema ya kuboresha mchakato wetu huu muhimu. Dhamira yangu na ya wenzangu Serikalini ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na mchakato mzuri ili hatimaye tupate Katiba iliyo nzuri; Katiba ambayo italilea taifa letu kwa miaka 50 ijayo likiwa na amani, utulivu, demokrasia na maendeleo makubwa zaidi.

Ndugu Wananchi;

Ni matarajio yangu kuwa ndani ya robo ya kwanza ya mwaka ujao uundaji wa Tume ya Katiba utakuwa umekamilika. Katika robo ya pili au ya tatu ya mwaka 2012, Tume hiyo itaanza kazi yake ya kukusanya maoni. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu wote mjiandae kushiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yenu kwenye Tume ya Katiba. Aidha, niwaombe, ndugu zangu, tujiepushe na vitendo vya kuzuia watu kutoa maoni yao kwa uhuru hasa wale wenye maoni tofauti na yetu. Kutoa maoni katika Tume hiyo ni haki ya kila mwananchi.

Iwe ni mwiko kwa mtu yoyote au kikundi chochote kumzuia mtu au watu wowote kutumia haki yao hiyo. Iwe ni mwiko pia kwa mtu, watu au taasisi yoyote kujaribu kuhodhi mijadala hiyo. Ni vyema tukajua kuwa tunatengeneza Katiba ya watu wote na kwa maslahi yetu sote. Hatutengenezi Katiba ya watu fulani wateule au kikundi fulani cha kisiasa au kijamii kwa maslahi yao. Tuwaache watu watoe maoni yao kwa uhuru ili tupate Katiba ya watu wote.

Hali ya Usalama Nchini

Uharamia Baharini

Ndugu Wananchi;

Hali ya usalama wa nchi yetu katika mwaka 2011 ilikuwa ya kuridhisha na Tanzania iliendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu. Kwa jumla, mipaka yetu yote ilikuwa salama isipokuwa ule wa majini kwa upande wa Bahari Kuu ya Hindi ambako kumekuwepo na matukio ya uharamia. Katika mwaka huu tunaoumaliza leo, kumekuwepo na majaribio tisa ya kuteka meli ndani ya mipaka yetu katika Bahari Kuu hiyo. Bahati nzuri hakuna hata moja lililofanikiwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi letu la Wanamaji. Maharamia saba wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani ambako kesi zao zinaendelea.

Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya ya kupambana na maharamia katika Bahari Kuu ya Hindi. Kutokana na juhudi zao hizo matukio ya kujaribu utekaji meli yamepungua mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana ambapo kulikuwa na matukio 30.

Ndugu Wananchi;

Natambua kuwepo kwa mahitaji kadhaa kwa Jeshi letu na wanajeshi wetu ili kuimarisha ulinzi katika mipaka yetu ya majini katika Bahari Kuu ya Hindi na katika maziwa yetu makuu ya Nyasa, Tanganyika na Victoria. Tumekwishaanza kuchukua hatua muafaka kwa ajili hiyo na tutaendelea nazo kwa kasi zaidi katika mwaka 2012 na kuendelea.

Uhalifu

Ndugu Wananchi;

Juhudi za kupambana na kudhibiti uhalifu nchini ziliendelea na mafanikio yameendelea kupatikana. Taarifa za Jeshi la Polisi za kati ya Januari na Novemba, 2011 zinaonesha kuwa matukio ya makosa makubwa ya jinai yamepungua ukilinganisha na hali ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka 2010. Makosa hayo yamepungua kutoka 86,150 hadi 69,678 na punguzo kubwa zaidi limetokana na kupungua sana kwa makosa ya wizi, pamoja na yale ya kubaka, kunajisi, kutupa watoto, unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma nyumba, na dawa za kulevya.

Ndugu Wananchi;

Mafanikio haya ya kutia moyo ni uthibitisho wa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Tutaendeleza juhudi za kuliwezesha Jeshi hilo kwa zana, vifaa, mafunzo, maslahi na mazingira ya kazi na ya kuishi katika mwaka 2012 na miaka ijayo ili ufanisi mkubwa zaidi upatikane katika kupambana na uhalifu nchini.

Ajali za Barabarani

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa ajali za barabarani, matukio yamepungua kutoka 22,440 mwaka 2010 hadi 22,000 mwaka 2011. Hata hivyo, ajali zilizosababisha watu kupoteza maisha ziliongezeka mwaka huu kuliko mwaka wa jana. Mwaka jana ajali hizo zilikuwa 2,833 ukilinganisha na 3,012 mwaka 2011 na watu waliopoteza maisha walikuwa 3,332 ukilinganisha na 3,707 mwaka 2011.

Ongezeko la ajali barabarani linasababishwa na ongezeko kubwa la vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki. Katika miaka sita iliyopita, magari 514,136 na pikipiki 1,206,679 zimeinginzwa nchini. Sababu nyingine ni madereva kutokuwa makini katika uendeshaji ama kwa sababu ya ujuzi mdogo au uzembe na ulevi. Mimi naamini kuwa tatizo hili litapungua sana kama madereva wataacha uzembe, ulevi na kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Aidha, nirudie kuwataka ndugu zetu wa Polisi wanaosimamia sheria ya usalama barabarani, kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo na wale wote wanaotumia barabara, yaani vyombo vya usafiri na watu.
Ajali ya Mabomu, Meli na Mafuriko

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka 2011 licha ya ajali barabarani, kulitokea ajali ya kulipuka mabomu katika kambi ya Jeshi Gongolamboto, ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander huko Zanzibar na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam. Matukio hayo yamesababisha ndugu zetu wengi kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa na mali nyingi kupotea.

Milipuko ya Mabomu

Katika ajali ya Gongolamboto watu 25 walifariki dunia na 512 walijeruhiwa na nyumba 1,791 ziliharibiwa kwa viwango mbalimbali. Nimearifiwa kuwa shilingi 817,740,849 zimelipwa kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa nyumba zao zilizoharibiwa. Bahati mbaya kwa wale ambao nyumba zao ziliharibiwa sana na kulazimika kujengwa upya kazi hiyo imechelewa sana kuanza kwa sababu za urasimu wa kupata viwanja.

Nimemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ahakikishe kuwa wahusika katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Manispaa ya Ilala wanaacha urasimu na kuharakisha upatikanaji wa viwanja ili kazi ya ujenzi ianze. Aidha, nimewaomba viongozi wa Wizara ya Ulinzi, JWTZ na hasa JKT kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi itakapoanza inakamilika mapema iwezekanavyo.

MV Spice Islander

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa ajali ya MV Spice Islander iliyotokea Septemba 10, 2011 ndugu zetu 619 waliokolewa na maiti 203 zilipatikana. Mali iliyokuwa ndani ya meli hiyo haikuweza kuokolewa hivyo haikuweza kujulikana kama wapo watu wengine waliokuwa wamezama na meli hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein aliunda Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo. Tume hiyo imekamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake Serikalini. Hivi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaitafakari taarifa hiyo kwa lengo la kuchukua hatua muafaka. Subira yavuta heri.


Mafuriko ya Dar es Salaam

Ndugu Wananchi;

Kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia usiku wa kuamkia tarehe 20 mpaka tarehe 23 Desemba, 2011, Bonde la Mto Msimbazi na maeneo ya jiji yalikumbwa na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya jiji la Dar es Salaam. Kutokana na mafuriko hayo ndugu zetu 40 wamepoteza maisha na nyumba na mali nyingi zimeharibiwa. Pia, watu wapatao 5,029 wamekosa makazi na kupatiwa hifadhi na jamaa zao au katika maeneo yaliyotengwa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam. Aidha, Serikali imekuwa ikiwahudumia waathirika hao kwa malazi, chakula na huduma ya afya. Vile vile, watu na mashirika mbalimbali yamekuwa yanatoa misaada ya kibinadamu kuwasaidia ndugu zetu hao.

Ndugu Wananchi;

Tarehe 21 Desemba, 2011, niliwatembelea baadhi ya waathirika na kuona athari za mafuriko katika jiji la Dar es Salaam. Pia nilipata nafasi ya kupokea taarifa ya maafa hayo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa. Nilielezwa shughuli za uokoaji, huduma zinazotolewa kwa walioathirika katika makazi ya muda na mipango ya baadaye kuhusu watu walioathirika na ujenzi wa makazi katika Bonde la mto Msimbazi na mabonde mengine katika jiji la Dar es Salaam.

Niliwapa pole waathirika na kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam walivyoongoza juhudi za kuokoa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na janga hili na jinsi wanavyowahudumia. Niliafiki uamuzi wa Mkoa kwamba ndugu zetu waliojenga na kuishi katika Bonde la Mto Msimbazi wahame. Aidha, nilikubaliana na uamuzi wao kuwa wale wote waliojenga katika njia za asili za kupita maji na kuyalazimisha maji kutafuta njia nyingine na kusababisha madhara pasipostahili nao pia wabomoe. Maji yaachwe yapite kwenye njia zake za kawaida ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.

Ndugu Wananchi;

Ni matumaini yangu kuwa ndugu zetu wa Jangwani na kwingineko hawatakaidi tena amri halali ya mkoa kama walivyofanya miaka ya nyuma. Baada ya mafuriko ya mwaka 1998, ambapo baadhi ya watu waliokolewa kwa helikopta kama safari hii, watu waliamriwa kuhama na kugawiwa viwanja vya kujenga makazi mbadala. Lakini, walikaidi amri na kudiriki kwenda Mahakamani kuzuia utekelezaji wa amri hiyo. Bahati nzuri walishindwa.

Wahenga wamesema “asiyesikia la mkuu huvunjika guu”. Mafuriko yametokea tena mwaka huu, tena mabaya zaidi. Safari hii helikopta hazikutosha bali boti na vijana hodari wa kuogelea walitumika kuokoa maisha ya watu. Pamoja na juhudi hizo safari hii ndugu zetu 40 wamepoteza maisha na mali nyingi zaidi zimepotea na kuharibiwa.

Ndugu Wananchi;

Nimewataka viongozi wa Serikali na Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam washikilie msimamo wao huo huo. Watu watakaokaidi wasiachwe kuendelea kuishi mabondeni. Tukikubali wabaki, sote, yaani watu wenyewe na Serikali, hatutaeleweka. Tena tutachekwa na kulaumiwa vibaya siku za usoni mafuriko mengine yatakapotokea na watu kukutwa katika hali kama hii na Serikali kujikuta inarudia tena kufanya kazi ya kuokoa watu.

Bahati nzuri maeneo ya kuhamia yametambuliwa na viwanja vimeshaanza kugawiwa. Kila mwenye nyumba atapewa na naomba hata wapangaji wapewe iwapo viwanja vitasalia. Hivyo, narudia kuwataka ndugu zetu kuhama kwa hiari yao na wale watakaokaidi wahamishwe bila ya ajizi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Uchumi na Maendeleo

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa uchumi, mwaka 2011 ulikuwa na changamoto nyingi. Kulikuwa na mchanganyiko wa ukame, uhaba mkubwa wa umeme, upungufu wa chakula kwenye baadhi ya maeneo nchini, kupanda kwa bei za mafuta na vyakula, kushuka kwa thamani ya shilingi, mfumuko wa bei kupanda na sasa mvua nyingi na athari zake. Pamoja na changamoto hizo tunatarajia uchumi wetu utakua kwa asilimia 7 ingawaje wenzetu wa IMF wanakadiria kuwa utakua kwa asilimia 6.3. Hata kwa kiwango hicho bado nchi yetu inabakia kuwa miongoni mwa nchi 20 duniani zinazoongoza kwa ukuaji wa uchumi. Ni dhahiri basi kuwa kama athari hizo zisingekuwepo hali ya uchumi wetu ingekuwa bora zaidi.

Ndugu Wananchi;

Tulianza mwaka 2011 kukiwa na ukame mkali uliokumba maeneo mengi nchini. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 nililizungumzia suala la uhaba wa mvua na ukame na kutaka tuombe mvua za masika ziwe nzuri. Mvua hazikuwa nyingi na mtawanyiko wake haukuwa mzuri. Maeneo mengi mvua zilikuwa chini ya wastani. Kwa sababu hiyo watu 423,530 katika Halmashauri 36 za mikoa 13 walikumbwa na upungufu wa chakula na kuilazimisha Serikali kutoa msaada wa chakula.

Aidha, kwa sababu ya upungufu huo, bei za vyakula zilipanda sana hasa mijini. Ili kukabiliana na hali hiyo niliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuanza utaratibu wa kuuza mahindi kwa wafanyabiashara wa mijini ili kusaidia kupunguza bei ya chakula. Agizo langu hilo sasa ni sehemu ya sera ya Taasisi hiyo itakayotekelezwa kila mwaka wakati chakula kutoka mashambani kitakapopungua katika masoko ya mijini.

Ndugu Wananchi;

Ukame huo pia ukasababisha kupungua sana kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme na hivyo kuliingiza taifa katika tatizo kubwa la upungufu wa umeme. Ili kukabiliana na tatizo hilo TANESCO imelazimika kuingia mikataba na makampuni ya kuzalisha umeme kwa malipo. Kwa vile gesi inayozalishwa hivi sasa kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kufulia umeme iliyopo Ubungo haitoshelezi mahitaji ya taifa, makampuni hayo yamelazimika kutumia mitambo inayotumia mafuta.

Mitambo hiyo imepatikana na tayari inazalisha umeme. Ndiyo maana mgao sasa haupo. Lakini, kwa sababu ya kutumia mafuta, umeme huu ni ghali na umekuwa mzigo mkubwa wa gharama kwa TANESCO. Kutokana na sababu hizo, TANESCO wamepeleka maombi EWURA ya kutaka kuongeza bei ya umeme.

Ndugu Wananchi;

Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwamba tunaumaliza mwaka huu na kuuanza mwaka 2012 kukiwa na mvua nzuri karibu nchi nzima. Dua zetu mwaka huu ni kuomba mvua za kiasi kwani sehemu nyingine mvua zimezidi kipimo. Zimesababisha mafuriko, vifo vya watu, mali pamoja na miundombinu ya babara kuharibika. Katika baadhi ya maeneo mazao mashambani hasa mahindi yanaathirika kwa maji kuzidi. Kwa muelekeo huu wa mvua na hasa kama mvua za masika nazo zitakuwa nzuri mwaka 2012 kutakuwa na chakula kingi nchini karibu maeneo yote.

Ndugu Wananchi;

Baada ya ukame wa mwaka 2006 na upungufu mkubwa wa umeme wa tangu wakati huo mpaka mwaka 2008, tulitoa ahadi ya kuchukua hatua za makusudi za kupunguza utegemezi mkubwa wa kupita kiasi wa umeme wa nguvu ya maji. Nilisema kuwa tutaanza juhudi za kuendeleza vyanzo vingine vya nishati hasa gesi asilia na makaa ya mawe mpaka tufikie mahali ambapo hata kama maji hayatoshi katika mabwawa ya vituo vya umeme, nchi haitakosa umeme.

Tumeendelea kutekeleza uamuzi ule wa busara. Mpaka sasa Serikali kupitia TANESCO imeshaongeza MW 245 za umeme unatokana na gesi asilia. Nyongeza hiyo ingeweza kuwa kubwa zaidi lakini hakuna gesi ya kutosha kutoka Songo Songo. Bahati mbaya mchakato wa kuongeza gesi umechelewa kwa karibu miaka miwili, lakini mwelekeo sasa mzuri.


Ndugu Wananchi;

Maombi yetu kwa Serikali ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka Songo Songo yamekubaliwa. Utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi 18 na gesi itakayoletwa inaweza kuzalisha mpaka Megawati 3,000 za umeme. Baada ya hapo kasi ya kuongeza umeme itakuwa kubwa zaidi na tatizo la upungufu wa umeme linaweza kuwa historia.

Bahati nzuri wawekezaji wa kuzalisha umeme kutumia gesi hiyo wapo, wanachosubiri ni gesi kufika. Wakati huo huo michakato ya kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe ya Ngaka, Kiwira na Mchuchuma imeanza na ipo katika hatua mbalimbali. Pia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya upepo unaendelea vizuri.

Matatizo ya Bei ya Mafuta

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka 2011 bei ya mafuta iliendelea kuwa tatizo. Tatizo hilo lilikuwa na sura ya ndani na ya nje. Bei ya mafuta katika soko la dunia ilipanda kutoka dola za Marekani 76.1 kwa pipa mwezi Septemba, 2010 hadi dola 100.5 Septemba, 2011 na dola 99.92 jana tarehe 30 Desemba, 2011. Kwa vile mafuta yanagusa takriban nyanja zote za uchumi na maisha ya Watanzania nyongeza ya asilimia 45 ya bei za mafuta imesababisha kupanda kwa gharama ya huduma na bidhaa nyingi hivyo kuongezeka gharama ya maisha kwa watu.

Ndugu Wananchi;

Hapa kwetu makali ya ongezeko la bei ya mafuta duniani yaliongezwa na kushuka thamani ya shilingi na vitendo vya wafanyabiashara ya mafuta. Thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilishuka kutoka wastani wa shilingi 1,500 kwa dola ya Kimarekani mwanzoni mwa Januari, 2011 hadi shilingi 1,815 kwa dola tarehe 27 Oktoba, 2011. Serikali kupitia Benki Kuu ilichukua hatua mbalimbali zilizoweza kupunguza kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi hadi wastani wa shilingi 1,595 kwa dola hivi sasa.

Kwa sababu ya shilingi kupungua thamani, waagizaji wa mafuta walilazimika kutumia pesa nyingi za Kitanzania kununua dola ambazo kabla ya hapo walitumia pesa kidogo kuzipata. Hali hiyo ndiyo iliyosababisha athari za kupanda kwa bei za mafuta duniani kuwa kali zaidi hapa nchini.

Sambamba na hilo, mwenendo wa wafanyabiashara hasa wa kukataa kutii maamuzi ya EWURA hasa pale wanapoteremsha bei limekuwa tatizo lingine. Wafanyabiashara hawako tayari kuona watumiaji wa mafuta wakipata nafuu hata kidogo. Kila bei zinaposhuka basi watapinga. Ama wataendelea kuuza kwa bei ya zamani au watasababisha upungufu wa mafuta ili bei iendelee kuwa juu. Lakini EWURA wanapotangaza kupandisha bei, yote hayo hayaonekani.

Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wafanyabiashara ya mafuta kutoa ushirikiano kwa EWURA inapotimiza wajibu wake. Ni ukweli ulio wazi kuwa bei ya mafuta duniani hupanda na kushuka. Kukataa kushusha bei ya mafuta wakati bei ya dunia inaposhuka ni tamaa ya utajiri iliyovuka mipaka ya utu. Nawapongeza EWURA kwa msimamo wao na waendelee kuwawajibisha wanaokaidi. Msirudi nyuma.

Kwa nia ya kutafuta nafuu ya bei ya mafuta, tumeamua kuanzisha uagizaji wa pamoja wa mafuta. Lengo ni kupata nafuu ya bei na ya gharama ya uchukuzi na hivyo kumfanya mtumiaji wa mwisho naye apate nafuu ya bei ya mafuta. Utaratibu huo utaanza rasmi mwezi Januari, 2012. Tungoje tuone utakavyopokelewa na wafanyabiashara. Naamini utasaidia, labda kama utahujumiwa. Naagiza Wizara na Mamlaka husika kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa kama tunavyotarajia.

Kilimo

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa kilimo katika mwaka 2011 juhudi za kuleta mageuzi katika kilimo chetu zinazolenga kuwanufaisha wakulima wadogo zimeendelea kutekelezwa. Ruzuku ya pembejeo iliendelea kutolewa, maafisa ugani waliongezwa vijijini na uboreshaji wa masoko na miundombinu vijijini uliendelea. Juhudi hizo zimeleta matokeo mazuri kwa uzalishaji wa mazao kuongezeka. Bahati mbaya katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa kumekuwa na usumbufu mkubwa wa ununuzi wa mahindi ya wakulima katika msimu huu.

Kiini cha tatizo ni taratibu za kupata fedha za kununulia mahindi kutokamilika mapema. Nimewaagiza viongozi wa NFRA, Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuhakikisha kuwa wakulima ambao mazao yao yako mikononi mwa NFRA wanalipwa mara moja na usumbufu uliokuwepo safari hii haujirudii tena mwakani na miaka ijayo. Lazima taratibu za kupata fedha za kununulia mazao ya wakulima zianze na kukamilika mapema kabla ya msimu wa ununuzi kuanza. Aidha, nimewataka wahakikishe kuwa ucheleweshaji wa upatikanaji wa vocha za pembejeo haujitokezi tena mwakani na miaka ijayo. Kwa sasa njia zitafutwe za kuhakikisha kuwa wakulima hawakosi pembejeo kwa sababu ya vocha kuchelewa.

Ndugu Wanananchi;

Vile vile, nimeelekeza kuwa mwakani uwekwe mfumo mzuri utakaowawezesha wafanyabiashara binafsi kushiriki mapema katika ununuzi wa mazao ya wakulima. Pamoja na kuuza sehemu ya mahindi ya NFRA mijini ili kushusha bei hasa katika kipindi cha upungufu wa mahindi mikononi mwa wakulima, NFRA itafute namna bora ya kuuza mazao yaliyopo katika maghala yake mapema kabla ya msimu mpya wa ununuzi haujaanza. Kufanya hivyo kutatoa nafasi katika maghala ili kutoa nafasi ya kuhifadhi bidhaa za msimu mpya.

Uwekezaji

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka huu tunaoumaliza leo tulitoa kipaumbele cha juu katika kukuza uwekezaji nchini na tunakusudia kuendelea kufanya hivyo mwaka ujao. Tumekuwa tunatangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwashawishi wawekezaji wa ndani na nje kujitokeza kuja kuwekeza. Pia tumekuwa tunachukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuifanya Tanzania kuwa nchi nzuri ya kuwekeza na kufanya biashara.

Tumeainisha maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji ambayo baadhi yake ni viwanda, kilimo, madini, utalii, biashara, nishati, uchukuzi na teknohama. Lengo letu kuu la kuhimiza uwekezaji nchini ni kutaka kuongeza uwezo na kasi ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kuongeza uzalishaji mali, kuboresha huduma na kukuza ajira.

Ndugu Wananchi;

Mara kadhaa unawasikia watu hapa nchini na kwingineko duniani wakiuliza kwa nini nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ni maskini wakati rasilimali zimejaa tele. Moja ya sababu kubwa ni kutokuwepo kwa uwekezaji wa kutosha wa kuzigeuza rasilimali hizo kuwa bidhaa na huduma za kuuza katika soko na kuwapatia mapato wamiliki wake watakayoyatumia kuboresha hali zao za maisha. . Chukua, kwa mfano, mtu mwenye msitu mkubwa na mzuri anayetaka uwe shamba la kuzalisha mazao yatakayomwezesha kupata mapato yatakayosaidia kubadili maisha yake. Haitakuwa hivyo mpaka pale atakapochukua panga na jembe akafyeka na kulima, baadae akachukua mbegu akapanda, akaweka mbolea, akapalilia, akavuna na kupeleka mazao sokoni kuuza akapata pesa, atakapozitumia kujipatia mahitaji yake ya maisha. Kufyeka, kulima, kupanda, kupalilia, kuvuna na kupeleka sokoni ndiyo uwekezaji.

Ndugu Wananchi;

Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana sisi katika Serikali tunahimiza na kuvutia wawekezaji ili nchi itumie fursa zilizopo nchini kujiletea maendeleo, kupunguza umaskini na kukuza ajira.

Inakadiriwa kuwa hapa nchini mwaka 2011, kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi 22,152,320 na kati ya watu hao 2,368,672 au sawa na asilimia 10.7 hawana ajira. Ili watu hao waweze kupata ajira itategemea kwa kiasi gani tunafanikiwa kukuza uwekezaji katika sekta na shughuli mbalimbali. Bila ya hivyo kupatikana kwa ajira itakuwa ndoto.

Ndugu Wananchi;

Katika kuwahamasisha wawekezaji, tunatambua fika umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wananchi wa Tanzania. Wanahitaji upendeleo maalum na wanahitaji kuwezeshwa na tumekuwa tunafanya hivyo. Ndiyo maana kuna maeneo na shughuli zilizotengwa maalum kwa ajili ya wawekezaji wazawa pekee. Aidha, umewekwa ukomo wa kiwango cha chini cha mtaji ambacho wawekezaji wageni lazima wawe nacho ili watambuliwe kuwa wawekezaji. Tusipofanya hivyo uchumi utatawaliwa na wageni.

Lakini hatukuishia hapo tu, tumelitazama suala la uwezeshaji wa wazawa ili waweze nao kushiriki katika fursa zilizopo nchini mwao. Tumechukua hatua za makusudi kufufua Benki ya Rasilimali kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wawekezaji wazawa kwa shughuli za viwanda na biashara. Pia tunakamilisha mipango ya kuanzisha Benki ya Kilimo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima wazawa. Benki hizo mbili hazitatoa mikopo kwa wawekezaji wageni. Aidha, tumeanzisha mpango wa dhamana kwa wauzaji nje na wenye viwanda vidogo na vya kati, yaani Export Credit Gurantee Scheme na Small and Medium Enterprises Guarantee Scheme”. Mifuko hiyo maalum inayosimamiwa na Benki Kuu ipo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wazawa. Mwaka 2011 wananchi wengi walinufaika na Export Credit Guarantee Scheme kupitia vyama vyao vya ushirika 635 vilivyopatiwa jumla ya shilingi bilioni 108.67. Aidha, makampuni mengine yalipata jumla ya shilingi bilioni 24.35. Ni makusudio yetu kuongeza fedha ili makampuni na na watu wengi wanufaike na fursa hizi.

Uwezeshaji Wajasiriamali Wadogo

Ndugu wananchi;

Tunatambua kwamba wapo watu wanaopenda kufanya shughuli zao za kujipatia kipato. Tunatambua pia kwamba si kila mtu atapata nafasi ya kuajiriwa, lakini wapo wanaoweza kujiajiri kwa maana ya kuwa na shughuli zao za kuwapatia riziki. Hata hivyo, ili waweze kufanya hivyo wanahitaji kuwa na mtaji, yaani pesa. Si wengi wanao ndugu au jamaa wa kuwapatia pesa wanazozihitaji. Pesa za namna hiyo ziko benki ambako kuzipata kwake kuna masharti magumu, moja likiwa ni dhamana ya kitu kisichoondosheka. Wengi na hasa vijana hawana dhamana ya namna hiyo.

Ni kwa nia ya kuwaondoshea kikwazo hicho ili waweza kukopesheka, ndipo tulipohimiza uanzishaji wa SACCOS na kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Ndiyo maana pia kuna Mifuko ya Wanawake na Vijana. Kwenye Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila Mkoa kwa upande wa Bara na milioni 100 kwa mikoa ya Zanzibar isipokuwa Mkoa wa Mjini Magharibi uliopata shilingi milioni 200. Pesa hizo zilikopeshwa kupitia Benki za NMB na CRDB kila moja ikipewa shilingi bilioni 5.5 kwa maelewano kuwa wao watachangia mara tatu. Pia asasi ndogo za fedha 12 zilipewa jumla ya shilingi bilioni 10.

Ndugu Wananchi;

Tathmini iliyofanywa na Baraza la Uwezeshaji la Taifa zinaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 37.17 zilikopeshwa na benki za NMB na CRDB na jumla ya shilingi bilioni 12.06 zilikopeshwa na asasi 12 za fedha. Jumla ya wananchi 72,912 wamenufaika na mikopo hiyo. Kati yao 46,299 ni wanaume na 36,613 ni wanawake. Mikopo hiyo pia imenufaisha SACCOS 192 na vikundi vingine 86. Kati ya jumla ya shilingi bilioni 49.23 zilizotolewa kwa mikopo, shilingi bilioni 39.275 zimesharejeshwa ambazo ni sawa na asilimia 79.8 ya mikopo iliyotolewa. Kiwango cha urejeshwaji mikopo kinategemewa kuongezeka kwa vile baadhi ya mikopo iliyotolewa kupitia asasi ndogo za fedha bado haijaiva.

Ndugu Wananchi;

Tathmini iliyofanywa inaonyesha pia kwamba yapo mambo mazuri mengi na upungufu kadhaa. Upungufu uliojitokeza ni pamoja na baadhi ya SACCOS kutoza riba kubwa kuliko kiwango cha juu kilichowekwa na serikali cha asilimia 12. Lingine ni kuwa japokuwa vijana ndiyo wanaohitaji uwezeshaji wa kujiajiri lakini ni asilimia 32.5 tu ya vijana waliokopeshwa. Aidha, wanawake walikuwa ni asilimia 38.4 tu ya waliokopeshwa.

Baadhi ya mazuri yaliyojitokeza ni pamoja na: ongezeko la ajira la asilimia 3.8; kuongezeka kwa watu wenye akaunti benki kwani asilimia 33 ya waliokopeshwa walifungua akaunti kwa mara ya kwanza. Lingine muhimu ni kupanda hadhi kwa baadhi ya SACCOS, vikundi na watu binafsi kulikowafanya waweze kupata sifa na nafasi ya kukopeshwa na mabenki. Urejeshwaji wa mikopo kwa takribani asilimia 80 ni wa kuridhisha japo ingekuwa bora kiasi chote au hata zaidi ya hapo kitarejeshwa. Hivyo basi juhudi ziendelee kufanyika katika kurejesha mikopo iliyosalia.

Ndugu Wananchi;

Kwa ujumla tathmini iliyofanyika inaonesha kuwa mpango huu ni wenye manufaa na kwamba yafaa tuendelee nao. Pia kwamba tuuongezee uwezo ili wananchi wengi zaidi wafaidike nao. Serikali inayaafiki mapendekezo hayo na inayafanyia kazi. Ni makusudio yetu kuwa katika bajeti ijayo tutatenga fedha zaidi katika Mfuko huu. Tutaendelea kutumia mpango wa dhamana kwa mabenki ili kuongeza fedha za uwezeshaji. Aidha, tutauboresha mfuko huu na mingineyo yote ya uwezeshaji kiutendaji na kifedha ili watu wetu wengi waweze kunufaika nayo. Tutatengeneza mfumo maalum utakaowawezesha vijana wengi zaidi kunufaika.

Ndugu Wananchi;

Naelewa kuwa upo utaratibu unaozitaka Halmashauri za Wilaya na Miji kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. Utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa ukisuasua. Napenda kutumia nafasi hii kuzikumbusha Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatekeleza agizo hilo bila kukosa. Wakuu wa Wilaya wafuatilie utekelezaji wa agizo hili na watoe taarifa kwa Wakuu wa Mikoa kila miezi minne ambao nao watatoa taarifa kwa Waziri Mkuu.

Malimbikizo ya Madai ya Watumishi Serikalini

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka 2011 kero ya malimbikizo ya madai ya stahili mbalimbali za watumishi wa umma wakiwemo walimu imejirudia tena. Tatizo hili nililikuta wakati naanza kazi hii na tukafanya jitihada kubwa na kulipa madeni yote. Baada ya kubaini kuwa limekuwa linajirudiarudia kila baada ya kipindi kifupi, nilitoa maelekezo kwa Halmashauri za Wilaya na Miji na Wizara za Serikali kuhakikisha kuwa tatizo hilo linakoma.

Kuhusu uhamisho nilielekeza kwamba kama Halmashauri au taasisi yoyote ya Serikali haina pesa za uhamisho, isiwahamishe watumishi wake. Niliagiza kuwa mtindo wa kuhamisha watumishi bila ya kuwa na fedha za uhamisho ukomeshwe mara moja. Nilitaka kiongozi au mhusika yeyote atakayekiuka agizo hili alipishwe yeye gharama za kumhamisha mtumishi huyo. Kuhusu madai ya likizo nilielekeza kutengwe fedha za kutosha za likizo kwani mapumziko ni haki na muhimu kwa wafanyakazi. Hata hivyo kama fedha hakuna si busara kulimbikiza madeni. Uzuri wa likizo ni kuwa hazipotei. Wakati wa kustaafu siku za likizo ambazo mtumishi hakuchukua hulipwa.

Ndugu Wananchi;

Nilisema pia kwamba suala la kuwapandisha watumishi vyeo bila kuwarekebishia mishahara yao kwa wakati ni upungufu wa kiutendaji ambao ni lazima ukomeshwe mara moja. Kupandishwa watumishi vyeo ni mpango unaoeleweka na siyo jambo la dharura wala ajali. Kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali, mtumishi hupandishwa cheo kwa misingi miwili. Kwanza, kutimiza masharti ya muundo wake wa utumishi, na pili, kuwepo kwa fedha kwenye bajeti ya Wizara au Idara husika kwa madhumuni hayo. Hivyo iweje leo mtu apandishwe madaraja bila kulipwa mshahara stahiki? Hili halieleweki na wala halikubaliki.

Ndugu Wananchi;

Niliagiza viongozi wa Wizara zote na Halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi wote wanapandishwa vyeo wakati wao ukiwadia na wanalipwa stahili zao kwa wakati. Hali kadhalika, madeni ya malimbikizo ya mafunzo hayawezi kuwepo kama utaratibu wa serikali wa mafunzo ungefuatwa. Chini ya utaratibu huo mambo matatu hupaswa kuzingatiwa. Kwanza, mpango wa mafunzo wa Wizara, Idara au Taasisi. Pili, watumishi wanaohitaji mafunzo kuingizwa kwenye mpango wa mafunzo wa taasisi husika. Tatu, kutenga fedha za kugharamia mafunzo hayo. Kama fedha haikutengwa, mtumishi hawezi kwenda kusoma. Mtumishi anayejiendeleza nje ya mpango huo atafanya hivyo kwa gharama zake mwenyewe.

Sasa madeni hayo ya mafunzo yanatoka wapi? Kama wako watendaji wanaowaruhusu watumishi walio chini yao kwenda kusoma bila kutengewa fedha kwenye bajeti wawajibishwe ipasavyo.

Ndugu Wananchi;

Baada ya hotuba yangu ya Februari, 2009 na Serikali kulipa takriban shilingi bilioni 64 kwa madai ya walimu mwaka huo, bado Serikali ililipa tena shilingi bilioni 29.8 kati ya Julai 2010 na Oktoba 2011. Hivi sasa nimeambiwa tena kuna madai mapya yaliyofikia shilingi bilioni 52.7. Sina tatizo na madai yanayostahili kulipwa na najua kwamba shilingi bilioni 22.5 zimetolewa na kati ya hizo shilingi bilioni 19.2 zimekwishapelekwa kwenye Halmashauri husika na shilingi bilioni 3.3 ni kwa ajili ya waajiriwa wa Wizara. Zilizobakia zitalipwa kwenye mishahara yao.

Bado ningependa kujua imekuwaje tena kuwe na malimbikizo makubwa kiasi hiki. Mambo haya tulikwishaelewana kuhusu namna ya kuepuka malimbikizo. Kulikoni? Je lini tabia hii ya kulimbikiza madeni itakoma? Nataka majibu toka kwa wahusika.

Ndugu Wananchi;

Hivi karibuni tumelijadili suala la ajira na huduma kwa walimu. Tumegundua kuwa zipo mamlaka kadhaa zinazohusika na ajira na masuala ya walimu na kwamba huenda inachangia kasoro hizi zinazojitokeza. Tumeelewana kuhusu kulitafutia ufumbuzi wa kudum wa suala hilo mapema iwezekanavyo. Labda itasaidia. Naamini baada ya muda si mrefu tutakuwa tumepata jawabu litakaloturidhisha sote. Serikali na walimu ili tuondokane na misuguano isiyokuwa ya lazima.

Mahusiano ya Kimataifa

Ndugu Wananchi;

Katika medani ya Kimataifa mwaka 2011, Serikali iliendelea kutetea na kuendeleza maslahi ya Tanzania nje ya nchi. Mahusiano yetu na mataifa na mashirika ya kikanda na kimataifa yamezidi kuimarika. Ahadi yetu katika mwaka 2012 ni kuendeleza juhudi hizo maradufu kwani nchi yetu inanufaika sana kwa ajili hiyo.

Washirika wetu wa maendeleo wameendelea kutuunga mkono, kututia moyo na kutusaidia katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mzuri na misaada yao na tunawaahidi kuitumia vizuri misaada hiyo.



Sensa

Ndugu Wananchi;

Katika kumalizia hotuba yangu nataka kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Jumapili ya tarehe 26 Agosti, 2012. Hapa nchini tumekuwa na utaratibu wa kufanya sensa kila baada ya miaka 10, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2002.

Kufanya Sensa ya Watu na Makazi ni jambo lenye umuhimu wa kipekee kwa taifa. Takwimu na taarifa zitakazokusanywa husaidia taifa katika kupanga mikakati na mipango yake ya maendeleo. Aidha, husaidia Serikali kupima mafanikio ya programu zake mbalimbali za Maendeleo. Husaidia pia kujipanga vizuri katika kufanya mambo yake.

Ndugu Wananchi;

Maandalizi ya kufanyika kwa sensa hiyo yanaendelea vizuri. Maelekezo yanatolewa na yataendelea kutolewa kuhusu namna itakavyofanyika na wajibu wa kila mmoja wetu. Ninawaomba Watanzania wenzangu msikilize maelezo na maelekezo hayo. Pia naomba nyote muhifadhi na kuikumbuka tarehe hiyo ili siku hiyo mtu asikose kuhesabiwa. Mwisho, naomba kila mmoja wetu awepo kuhesabiwa siku hiyo.

Vitambulisho vya UTaifa

Ndugu Wananchi,

Jambo la pili ni vitambulisho vya uraia. Hatimaye azma ya tangu Uhuru ya kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha uraia tumeweza kuanza kuitimiza. Mwezi Desemba mwaka 2011, mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya uraia umeanza. Mchakato huu ambao ni wa miaka mitatu umegawanyika katika awamu nne kila moja ikihusisha makundi mbalimbali.

Awamu ya kwanza imeanza na watumishi wa Dar-es-Salaam na Zanzibar na vitambulisho vyao vitatolewa wakati wa sherehe za Muungano mwezi Aprili 2012. Baada ya hapo zitafuta awamu nyingine. Nawasihi wananchi wenzangu mjiandae kwa kutayarisha nyaraka muhimu zitakazohitajika kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo. Aidha, naomba kutoa tahadhari kwamba watumishi watakaohusika na zoezi hili wawe waadilifu. Sitapenda kuona au kusikia vitambulisho vinatolewa kwa watu ambao hawastahili kuvipata. Ni wajibu wao kujiridhisha na nyaraka zinazowasilishwa na wananchi na kama watakuwa na mashaka ni vyema kuwasiliana na taasisi husika kwa uthibitisho zaidi.

Hitimisho

Ndugu Wananchi; Watanzania Wenzangu;

Wakati tunapojiandaa kuanza mwaka mpya hapo kesho, napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tumedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa moyo wetu wote na kwa nguvu zetu zote. Tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na vipaji alivyotujaalia Mwenyezi Mungu kushirikiana nanyi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazolikabili taifa letu na watu wake. Naamini kwa pamoja na ushirikiano tutaweza, kila mtu atimize wajibu wake.

Baada ya kusema hayo, nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya 2012. Sote tusherehekee kwa amani na utulivu.

Mungu Ibariki Afrika;

Mungu Ibariki Tanzania.

Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment