Saturday 10 December 2011

Vurugu lazuka katika Mahafali ya Tano ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Kishiriki Muhimbili (MUHAS) leo

Wakuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Kishiriki, Muhimbili (MUHAS) wakiingia kwa maandamano kwenye Mahafali ya Tano ya Chuo hicho kabla ya kuzuka kwa vurugu.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo hicho wakiwa tayari kwa kutunukiwa nishani zao kabla ya kuzuka kwa vurugu.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Kishiriki, Muhimbili (MUHAS) wakimsikiliza mwenzao kabla ya kusambalatishwa na kikosi kazi cha Jeshi la Polisi (FFU).
Brass Band ya Jeshi la Magereza ikitumbuiza kabla ya kuzuka kwa vurugu hizo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mh. Ali Hassan Mwinyi (katikati) akiongozana na baadhi ya wakuu wa Chuo hicho mara baada ya kuzuka kwa vurugu za wanafunzi wa chuo hicho waliokiwa wakitaka kurudishwa kwa Serikali ya Wanafunzi ambayo ilivunjwa hapo awali.
Mmoja wa wanafunzi wa Chuo hicho akiwa ametiwa mbaroni na kina Ras Makunja.
Mmoja wa watu walioathirika na vurugu zilizotokea leo akiwa ameanguka katika kiti.
Ras Makunja akiwa na Gitaa lake tayari kwa kuendeleza muziki.
Kina Ras Makunja wamekasirika sasa ni mwendo wa macho mbele.
Ras Makunja akiwa tayari kwa lolote.
Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile akiwasihi wanafunzi kutawanyika.
mabango.
malalamiko.
wazee wakiwa tayari kwa lolote

Na Francis Dande

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Kishiriki, Muhimbili (MUHAS), leo wamesababisha shughuli za Mahafali ya Tano ya Chuo hicho kusimama kwa muda baada ya kuzuka kwa fujo kubwa zilizopelekea Askari wa Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya kishindo ili kuwatawanya.

Wanafunzi hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kuhamasishana huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali kwa lengo la kuushinikiza uongozi wa chuo hicho kurudisha serikali ya wanafunzi (MUHASSO).

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Deogratias Ntukumazina alitoa ahadi kwa wanafunzi hao ya kuirudisha Serikali ya Wanafunzi pindi watakapofuta kesi waliyofungua Mahakama Kuu kauli ambayo ilipingwa vikali na wanafunzi hao na kutishia kuvuruga shughuli za mahafali zilizokuwa zimesimama kwa muda kutokana na wanafunzi hao kufanya mkutano wao uongozi wa Chuo mbele ya Jukwaa ambalo sherehe za kuwatunuku wahitimu zingefanyika kutokana na kugoma kuondoka mahali hapo hata baada ya uongozi wa Chuo kuwataka kufanya hivyo jambo ambalo lilisababisha Jeshi la Polisi kuongeza nguvu ili kuwatawanya.

Hali ilivyokuwa mbaya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alitoa amri kwa Polisi waliokuwa wakilinda Usalama kutumia nguvu jambo ambalo lilisababisha baadhi ya wazazi waliofika katika mahafali hayo kukimbia ovyo na kuanguka na watoto na kusababisha baadhi yao kuumia kutokana na mawe yaliyokuwa yakirushwa na wanafunzi na baadhi ya viti kuvunjwa na wanafunzi hao, katika kurupushani hiyo baadhi ya wanafunzi walikamatwa na Polisi.

Katika Mahafali hayo ambayo baadaye yalifanyika chini ya ulinzi mkali baada ya polisi kuwatawanya wanafunzi hao baada ya njia ya majadiliano kushindikana kutokana na jazba za wanafunzi hao waliokuwa walikuwa wakidai serikali ya wanafunzi ilirudishwe leo.

Hata hivyo Kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi hao aliyetambulika kwa jina la Njechele Boniface alisema kuwa walianza kukusanyika chuoni hapo majira ya saa mbili asubuhi ili kufanya mkutano wao na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Deogratias Ntukumazina ili kuepuka kuingiliana na shughuli za mahafali hayo lakini Mwenyekiti wa Baraza la Chuo alifika chuoni hapo majira ya saa sita mchana na kusababisha kuingiliana kwa mkutano huo na shughuli za mahafali hayo.

No comments:

Post a Comment