Thursday, 12 January 2012

UTABIRI WA SAYARI KATIKA MWAKA 2012 HAPA TANZANIA

Na Dkt N T Jiwaji
  
Utabiri huu unaweza ukachukuliwa kama kwamba ni utabiri wa kinajimu kutabiri matukio ya baadaye.  Lakini si hivyo kamwe! Nyendo za sayari zinafahamika kwa kutumia usahihi wa kihisabati wa maelfu ya miaka ijayo. Kinachoelezwa kwenye makala haya ni matukio ya kufurahisha yanayoweza kutazamwa usiku angani katika mwaka mzima huu.  Yamebainishwa kwa kutumia programu ya kompyuta ya “Stellarium”na kukokotolewa na wataalamu wa astronomia, kwa mfano mtaaalam Fred Espanack wa NASA.
 
Utajiuliza,“Kwa nini unatolewa utabiri wa sayari tu, na siyo wa nyota?” Hofu ilikuwa kwamba ingetolewa kama utabiri wa nyota, ungeweza kuchukuliwa kama utabiri kwa njia ya unajimu au ufalaki, ambao si wa kisayansi. Kusema kweli, kutabiri mwendo wa nyota za kawaida angani si mgumu, kwa vile nafasi za mpagilio ya Makundi ya Nyota angani huwa haubadiliki.  Kinachobadilika ni kusogea kwa Makundi ya Nyota kutoka mashariki kwenda magharibi kama vile Jua linavyosogea wakati wa mchana ambayo inatokana na mzunguko wa Dunia yetu katika mhimili wake.
 
 
Nyota ziko umbali wa matrilioni ya kilomita kutoka kwetu, kwa hiyo nafazi zao zinabaki vile vile kwa maelfu ya miaka.  Ndiyo maana Makudi ya Nyota daima zina mpangilio huo huo na kupewa majina maalum kutokana na maumbo yanayo tokana na mpangilio huo.  Kwa mfano Kundi la Nyota linaloitwa Nge linaonyesha umbo kama la nge angani.  Maumbo ya Makundi ya Nyota hayajabadilika tangu uchunguzi wa kiastronomia ulipoanza maelfu ya miaka iliyopita.
 
Ukishatambua mpangilio wa Makundi ya Nyota, utaelewa upande gani  kuangalia ukitaka kuona Kundi fulani usiku.  Tahadhari kwamba Makundi ya Nyota pia yanasogea polepole kutokana na mzunguko wa Dunia kuiziunguka Jua.  Kuelewla kiasi gani nyota zitasogea kutoka na mzunguko huu huhitaji utaalamu lakini siyo sana .
 
Sayari, kwa upande mwingine, ziko umbali mdogo sana kutoka kwetu ukilinganisha na umbali wa nyota.  Sayari ziko mamilioni ya kilometa wakati nytoa ziko matrilioni ya kilometa.  Pamoja na hiyo sayari huzunguka Jua. Kwa hiyo, sayari huhama angani kwa kiasi kikubwa siku hadi siku. Kuelewa nafasi za sayari angani unahitaji utaalaamu mkubwa.
 
Tukio kubwa na muhimu zaidi la kuangalia mwaka huu ni Mpito wa Zuhura Juani mapema alfajiri tarehe 6 Juni. Hili ni tukio la kipekee katika maisha yetu kwa sababu tukio jingine kama hili halitatokea kwa zaidi ya karne moja, hadi Desemba 2117.  Jiandae kuona tukio hilo kwa kutumia miwani ya kuona kupatwa kwa jua itakyokuwezesha kuona sura ya Jua.  Asubuhi ya tarehe 6 Juni kuanzia mawio, saa 12:33 asubuhi, tutaweza kuona sayari ya Zuhura kama doa, likisogea polepole katika sura ya Jua karibu kabisa na ukingo wake ikiwa ni katika mwisho wa Mpito wa Zuhura Juani.  Katika hatua ya mwisho, itachukua kiasi cha dakika ishirini kuanzia saa 1:36 hadi saa 1:54 asubuhi kwa doa la Zuhura kuvuka ukingo wa Jua.
 
Matukio ya Kupatwa kwa Jua na Kupatwa kwa Mwezi hayatatusisimua sana mwaka huu kwa vile kati ya matukio manne ya kupatwa yatakayotokea duniani mwaka huu, matatu yatatokea upande wa pili wa Dunia kutoka kwetu.  Tukio la kwanza ni la Kupatwa kwa Jua Duara (Annual Solar Eclipse), tarehe 20 Mei litakalotokea kaskazini mwa Bahari ya Pasifiki, la pili ni tukio la Kupatwa kwa Sehemu ya Mwezi (Partial Lunar Eclipse), tarehe 4 Juni ambalo litaonekana katika eneo lote la Bahari ya Pasifiki na Australia na nchi zinazopakana na Bahari ya Pasifiki ambazo ni Asia ya Mashariki na America ya Magharibi.  Tarehe 15 Novemba kutatokea Kupatwa Kamili kwa Jua (Total Solar Eclipse) kwenye Bahari ya Pasifiki ya kusini. Kupatwa kwa mwisho tarehe 28 Novemba kutatokea Tanzania , lakini ni Kupatwa Kwepesi kwa Mwezi (Penumbral Lunar Eclipse) ambapo Dunia litatandaza kivuli chepesi kisichosababisha uweusi kwenye sura ya Mwezi.  Kwa taarifa zaidi kuhusu kupatwa huku, fungua tovuti ya http://eclipse.gsfc.nasa.gov/OH/OH2012.html
 
Ingawa mwaka huu hatutaweza kuona moja kwa moja matukio ya kupatwa wakati yanapotokea katika sehemu zinigine duniani, kuna tovuti nyingi kwenye mtandao wa Intaneti unazoweza kukufuatilia ambazo zinaonyesha kupatwa huku moja kwa moja wakati kunapotokea.
 
Ukilinganisha tarehe za kupatwa na awamu za Mwezi, utaona kwamba Kupatwa kwa Jua hutokea wakati wa Mwezi Mchanga tu, na Kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati wa Mwezi Mpevu.  Linganisha tarehe za kupatwa za hapo juu na tarehe za Mwezi Mpevu na Mwezi Mchanga zilizotolewa hapa chini.
 
Tarehe za kuandama kwa Mwezi (Mwezi Mchanga) nchini Tanzania kwa mwaka mzima ni: Januari 23, Februari 22, Machi 22, Aprili 21, Mei 21, Juni 19, Julai 19, Agosti 17, Septemba 16, Oktoba 15, Novemba 14 na Desemba 13.
 
Mwezi Mpevu utakuwa Januari 09, Februari 08, Machi 08, Aprili 06, Mei 06, Juni 04, Julai 03, Agosti 02, Agosti 31, Septemba 30, Oktoba 29, Novemba 28 na Desemba 28.
 
Matukio ya kuvutia zaidi angani ni sayari za Zuhura (Venus) na Sumbula (Jupiter) ambazo tayari zinang’ara katika pande mkabala za anga kama nyota kali kama vile ni taa iliyowekwa angani.
 
Zuhura iko juu angani na inaendelea kupanda haraka siku hadi siku.  Wakati huu, Jua linapokuchwa, Zuhura inaonekana iko juu, karibu nusu ya anga, upande wa magharibi.  Sayari hii inakaribia Dunia yetu polepole kwenye mzingo wake ambayo inasababisha ipande juu zaidi angani hadi kufikia nyuzi 35 ifikapo tarehe 1 Februari.  Itabaki takriban juu kiasi hicho hadi katikati ya Aprili.  Baada ya hapo, itakapokaribia zaidi na Dunia, itashuka angani na kufikia upeo wa magharibi mwisho wa Mei.  Wakati wa nyendo hizi, Zuhura inazidi kung’ara kwa kasi kikubwa zaidi hata kuweza kutoa kivuli usiku wa kiza zaidi bila Mwezi.
 
Wakati Zuhura inakaribia zaidi Dunia kwenye mzingo wake wa ndani ya mzingo wa Dunia, na kubadili nafasi yake kwenye anga za usiku, umbo lake linavyoonekana kwenye darubini pia unabadilika na ukubwa wake pia unaongezeka siku hadi siku.  Kuanzia mwanzo wa Oktoba mwaka jana wakati ilipokuwa inaonekana duara ndogo tu, hadi mwanzoni Januari hii, Zuhura imefikia awamu ya upevu na kuwa takriban umbo la yai, na kufikia mwinuko wa juu zaidi.  Ifikapo mwanzoni mwa Machi, itakuwa awamu ya nusu na kipenyo chake maradufu. Kuanzia katikati ya Aprili itakuwa na umbo la hilali nene na kubadilika kuwa hilali nyembamba ya kuvutia kama vile Mwezi Mchanga ifikapo mwisho wa Mei na ukubwa wake utakuwa mara tano.  Unaweza hata kuchanganya kati ya hilali ya Zuhura na ile ya Mwezi unapoiangalia Zuhura katika darubini.
 
Sumbula ni sayari nyingine inayoonekana kama nyota angavu katika mbingu ya mashariki na imekuwa ikipanda kila siku.  Kwa sasa imeshafikia utosini. Itasogea upande wa mbingu ya magharibi na kushuka zaidi mpaka itakapokutana na Zuhura mwanzoni mwa Machi.  Kwa kutumia darubini, utaweza kuona kwa urahisi mikanda sambamba ya mawingu katika ukanda wa ikeweta ya sayari hiyo.  Hata katika darubini ndogo utafurahia kuona miezi yake minne iliyopewa jina la Miezi ya Galileo.  Kila masaa mawili hivi utaona miezi minne hiyo ikibadilisha nafazi yake kama vile inaizunguka sayari ya Submula.  Sumbula ni sayari yenye gesi nzito na ni kubwa zaidi kuliko sayari zote katika Mfumo wetu wa Jua, na inaweza kumeza Dunia elfu moja ndani yake.
 
Mirihi (Mars) ni sayari nyingine itakayojitokeza na kuonekana katika anga za usiku wa kabla ya saa nne. Ifikapo mwishoni mwa Januari, itachomoza upande wa mashariki saa 3:30 usiku na ifikapo Machi itakuwa iking’ara sana kwa uwekundu ikiwa inachomoza wakati wa magharibi baada tu ya Jua kutua upande mkabala. Mwanga waJua huangaza sayari hiyo moja kwa moja usoni mwake nakuing’arisha.  Baada ya hapo, itafikia utosini katikati ya Mei na kushuka polepole upande wa magharibi hadi kufikia upeoni mwisho wa mwaka.
 
Mihiri inaonyesha mwendo wa upande wa mkabala, tofauti na mwendo wa kawaida wa sayari angani ambao ni kutoka magharibi kwenda mashariki katika mtandao mtulivu wa Makundi ya Nyota.  Kuanzia Januari hadi katikati ya Aprili, Mihiri inakwenda upande mkabala, ikitokea kwenye Kundi la Mashuke (Virgo) hadi kwenye Kundi la Simba (Leo). Ifikapo katikati ya Aprili itakaribiana sana na nyota ya mbele ya Simba iitwayo Regulus. Baada ya hapo inasogelea tena Kundi la Mashuke ikiwa katika mwendo wake wa kawaida wa kuelekea mashariki.
 
Zohali (Saturn) ni sayari iliyozungukwa na mfumo bapa wa pete iliyoundwa na mawe madogo madogo. Zohali inachomoza upeo wa mashariki saa 3:30 usiku mwanzoni mwa Machi.  Ifikapo katikati ya Aprili, Zohali itaanza kuchomoza mkabala na Jua linapotua saa ya magharibi, hivyo itakuwa angavu zaidi kwa vile uso wake utawashwa moja moja na mwanga wa Jua.  Baada ya hapo, itapanda polepole na kufikia utosini katikati ya Julai na baadaye kutua upande wa magharibi na kupotea kwenye upeo wa magharibi ifikapo mwisho wa Septemba.  Ukitaka kuitaitambua sayari yoyote anani, linganisha mng’aro wake na mng’aro wa nyota zingine jirani yake.   Sayari hung’ara kwa mwanga wa moja kwa moja, wakati mwanga wa nyota humeremeta.  Inavutia sana kuangalia sayari ya Zohali katika darubini kuona mfumo wake wa pete bapa.
 
Zebaki ni sayari isiyoonekana kwa washabiki wengi duniani kwa vile huizunguka Jua katika mzingo wa karibu mno na Jua hivyo huonekana karibu kabisa na upeo baada tu ya Jua kuchwa au kuchomoza.  Hata hivyo,  sisi hapa Tanzania tuna uwezo wa kuinona Zebaki mara kwa mara kwa vile inapanda juu ya kutosha angani kiasi na kuitoa katika mwanga wa  upeoni mara tu baada ya Jua kuchwa upande wa magharibi jioni au alfajiri kabala ya kuchomoza mashariki.
 
Mwanzoni mwa Januari, Zebaki iko Juu ya kutosha kuonekana upande wa mashariki kabla kupambazuka. Kama wewe ni mwamkaji wa alfajiri sana , tarehe 10 hadi 15 Januari utaona nyota zilizojipanga mbinguni kwenye mstari kutoka mashariki hadi magharibi.  Mwezi utakuwa upande wa magharibi na kufuatiwa na Mirihi anga ya katikati, na Sumbula itakuwa utosini, na mwisho Zebaki upande wa mashariki.  Zebaki pia itakuwa juu zaidi Februari 20, lakini wakati huu itaonekana jioni upande wa magharibi upeoni mara tu baada ya Jua kuchwa.  Siku hiyo pia itaunda mstari wa kukaribiana na Zuhura, Sumbula na Mwezi. Mpangilio huu wa mstari mmoja angani hutokea kwa sababu mizingo ya sayari zote kuizunguka Jua, na Mwezi kuizunguka Dunia, yote ipo katika bapa moja.
 
Machi 7, itaonyesha mpangilio mwingine wa mstari angani mara tu baada ya kuchwa.  Katika mstari huo zitakuwa Zebaki katika upeo wa magharibi, ikifuatiwa na Sumbula karibu yake na halafu Mwezi upande wa mashariki na Mirihi karibu na Mwezi.  Zebaki pia itaonekana juu tarehe 1 Julai na hasa Oktoba 27 ambapo itakuwa juu zaidi kabisa wakati wa magharibi baada tu ya Jua kuchwa.
 
Katika miezi ijayo, angalia makala zangu kwa maelezo zaidi kuhusu sayari na Mwezi na mambo ya kuvutia angani.  Pia utapata habari katika tovuti yangu, https://sites.google.com/site/astronomyintanzania/

No comments:

Post a Comment