Thursday 3 November 2011

Dr.Kimei azungumzia hali ya uchumi wa nchi na mafanikio ya Benki ya CRDB kwa muhula wa mwisho wa mwaka

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB,Dkt. Charles Kimei akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo kuhusu maendeleo na mafanikio ya Benki ya CRDB na hali ya uchumi wa nchi.Kushoto ni katibu wa Benki ya CRDB Bw. John Baptist Rugambo

============  ======  ==============

Utangulizi

Wakati tunakaribia mwishoni mwa mwaka 2011 nimeona ni bora kukutana nanyi ndugu zangu waandishi wa habari ili tupate kuzungumza mawili matatu kuhusu Benki yetu. Hivi Karibuni tumemaliza robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa Benki hivyo nimeona  niwashirikishe kuhusu hali ya CRDB Benki ili nanyi  muweze kuwafikishia habari hizi watanzania wenzetu ambao ni wateja wetu, wanahisa na pia wawekezaji.

Kwanza kabisa ni nianze kwa kusema kwamba kwa ujumla kuwa hali ya kifedha na kibiashara ya CRDB Benki ni nzuri sana. Pamoja na changamoto za kiuchumi zilizoikumba nchi yetu ambazo ni:
  • Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 6.4 mwanzo wa mwaka wa 2011 hadi asilimia 17.4 mwishoni mwa mwezi Septemba 2011.
  • Kushuka kwa thamani ya shillingi ya kitanzania kwa karibu ya asilimia 20 dhidi ya fedha za kigeni hasa hasa dola ya Marekani tokaShilingi 1,512 kwa dola moja January 2011 hadi shilingi 1,830 kwa dola moja mwishoni mwa mwezi Oktoba 2011.
  • Kutotabirika kwa soko la fedha, ambapo riba zimekuwa zikishuka na kupanda kwa kasi katika kipindi kifupi (interest rate volatility).
  • Mgawo wa umeme unaosababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, na kupungua kwa uwezo wa wateja wetu wakopaji kuzalisha na kulipa mikopo yao;
  • Serikali kuchelewesha malipo kwa wakandarasi tunaambiwa TANROADS yenyewe inadaiwa zaidi ya bilioni 400….. hii inamaanisha kuwa sehemu kubwa ya fedha hizi zinadaiwa mabenki.
 
Hali ya biashara ya CRDB Benki - Robo Tatu ya Mwaka
Pamoja na hayo yote ni fahari yangu kuu kusema tena kwamba CRDB Benki imefanya vizuri sana. Hadi mwisho wa mwezi Septemba 2011 Benki ilikuwa na amana toka kwa wateja zifikiazo Trilioni 2.3. Ikumbukwe kuwa wakati tunafunga robo ya pili ya mwaka mwezi Juni; Benki ilikuwa na amana za wateja zipatazo shilingi trilioni 2.1. 

Hapa kuna ongezeko la shillingi bilioni 200. Hili ongezeko linaonyesha kuwa wateja wetu wanaongeza kuwa na imani na CRDB Benki licha ya hali ya uchumi ikiwa tete. 

Pamoja na imani ya wateja wetu waletao fedha zao CRDB Benki kama amana, nasi kama Benki tumeongeza imani kwa wateja wetuwakopaji licha ya changamoto zinazowakabili kutokana na hali ya uchumi. 

Mpaka kufikia mwisho wa robo ya tatu ya mwaka 2011, Benki imeshatoa mikopo ya shilingi za kitanzania TRILLIONI 1.3, ikiwa tumeongeza utoaji wa mikopo kwa shilingi bilioni 80 katika robo ya tatu ya mwaka. Kama mnavyoona imani inazaa imani; mwisho maendeleo kwa jamii yetu wote. 

Baada ya kutoa taarifa kidogo kuhusu hali ya Mizania ya CRDB Benki, sasa nitazungumzia faida ambayo Benki imepata mpaka mwisho wa mwezi Septemba. Benki katika mipango yake ilikuwa imedhamiria kuongeza faida kwa asilimia 5 ikilinganishwa na matokeo ya robo kama hii mwaka jana.

Mpaka tunazungumza hapa, matokeo yaliyopo ya kifedha ni kuwa CRDB Benki imeshapata faida ya shillingi bilioni 63 kabla ya kodi.Shilingi bilioni 63 ni zaidi ya bilioni 10.5 ya faida ambayo Benki ilikuwa imepatikana katika kipindi kama cha Januari mpaka Septemba 2010. 

Hizi BILIONI 63 ni zaidi ya ongezeko la asilimia 22 ukifananisha na matokeo ya mwaka jana. Kama nilivyosema hapo awali hali ya kibiashara na kifedha ya CRDB Benki ni ya fanaka. Mimi naamini Mungu yuko na CRDB Benki 

Tunavyozungumza hapa, bado mwaka haujaisha. Sisi kama Benki bado tunaendelea kuweka bidii na kuongeza matumizi ya maarifa ili wateja wetu, wanahisa wetu na watanzania kwa ujumla wafaidike na Benki yao. CRDB Benki iko kwa ajili yao. 
Hali ya usoni ya kibiashara ya Benki

Baada ya kuzungumzia hali ya uchumi wa nchi na hali ya fedha ya CRDB Benki, naona ni sawia sasa tukazungumzia hali ya usoni ya kibiashara ya Benki hii. 

Mpango Mkakati wa Benki

Kwanza kabisa Benki imeendelea na utaratibu wake wa  kuhakikisha kuwa inawapatia wateja wake wote huduma na bidhaa za kivumbuzi (Innovative), za kisasa (Modern) na kwa gharama nafuu. Benki yetu huhakikisha kuwa ni “DAIMA YA KWANZA, KUWAWEKA WATEJA WETU KWANZA”. 

Wote mnafahamu kuwa tumeuletea umma wa watanzania kadi ya TemboCardMasterCard ambayo ni “chip card” (EMV Compliant)tukiwa wa kwanza kuuwezesha umma mkubwa wa watanzania kuweza kunufaika na bidhaa hii maarufu dunia nzima. Kama mnakumbuka tulikuwa wa kwanza kuutambulisha umma wa watanzania chapa ya Visa kwenye  kadi za malipo.

Hivi sasa ukiwa na akaunti na Benki yetu unaweza kupata huduma ulimwenguni kote ukiwa na chapa hizi mbili. Haijalishi akaunti uliyonayo ni ya shilingi au fedha zingine za kigeni. Mpaka tunavyoongea muda huu tumeshafikia na kuzidi lengo ambalo tulikuwa  tumekubaliana na MasterCard International.

CRDB Benki inatambua umuhimu wa wateja wadogo katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. Hivyo mbali ya mikakati mingi ambayo benki imetekeleza katika kuinua sekta hii; sasa imewaletea katika soko akaunti maalum ijulikanayo kama akaunti ya BIDII. Bidii akaunti ni akaunti mahususi kwa wafanya biashara wa kati na wadogo (SME). Itawasaidia sana kupata unafuu wa kuendesha shughuli zao za biashara na pia mikopo ya kuendeshea biashara hizo. 

Ni mahususi sana kwa wale wafanyabiashara wenye biashara mbalimbali ndogo au za kati  na wakati  mwingine wakiwa pia na ajira. Hapa nawazungumzia wenye biashara za maduka, mahoteli, biashara za usafiri (daladala au/na malori), Kilimo biashara (agribusiness) au ufugaji biashara  n.k. Bidii akaunti ni ya kipekee kwa kuwa ni akaunti ya hundi (Current) ambayo wakati huo huo inatoa faida, yaani riba kwa fedha ambazo zinakuwa kwenye akaunti.

 Hii pia ni mara ya kwanza kwa umma wa  watanzania kupata akaunti ya hundi ambayo pia inatoa riba.

Muda mfupi ujao pia CRDB Benki itazindua huduma mpya na ya kipekee kwenye sekta ya Kilimo-biashara (agribusiness) na ufugaji-biashara (livestock business) ambayo itajulikana kama Kilimo na Ajira Loans. 

Hii huduma nawahakikishia itawakosha wengi na kufuta machozi ya vijana wengi hapa nchini. Nadhani wote mnafahamu kuwa CRDB Benki inakopesha zaidi sekta ya kilimo kuliko sekta  nyingine zote. Asilimia 28% ya mikopo yetu yote inaenda kwenye sekta ya kilimo. 

Hili litakuwa na siku yake, hivyo kwa leo mnivumilie kwa kuwa naishia hapa. 
Wakati tunashughulikia hilo pia tuko kwenye hatua za mwisho katika kuboresha huduma yetu ya SimBanking. Kama mnavyofahamu hii ni huduma ambayo inamuwezesha mteja wa benki kupata huduma za Benki kwa njia ya simu ya mkononi. 

Nitawaeleza kwa undani zaidi tutakapokutana tena karibuni. 

Nikiendelea kuzungumzia hali usoni ya biashara, kama mnavyofahamu baada ya sekta ya kilimo, sekta inayofuata kwa ukuaji  ni sekta ya ujenzi. Hii sekta inakua sana, na sisi kama Benki tuliliona hilo na tumekuwa mstari wa mbele kwa miaka mingi kukopesha sekta hii.  

Hivi majuzi kulikuwa na tukio moja jema lililowahusisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na benki kadhaa, kusaini mkataba wa kutoa mikopo kwa wanunuzi wa nyumba za NHC. Benki yetu haikuwa moja kati ya watia saini wale. Kitendo hiki kiliwapatia simanzi watanzania wengi na kuwapa shaka pamoja na maswali mengi kulikoni???. Tumekuwa tukipata simu nyingi, barua na barua pepe watanzania wakiulizia jambo hilo. 

Napenda nilizungumzie hili katika sehemu tatu tofauti:
  • Kwanza, Nitaanza na suala la Benki na biashara  ya kukopesha wateja binafsi (Personal Customers) mikopo ihusuyo nyumba kama vile kujenga, kukarabati, kuongeza  au kununua. Benki imekuwa ikitoa mikopo ihusuyo suala zima la nyumba kwa wateja binafsi kwa miaka takribani kumi hadi sasa. Imekuwa ikitoa mikopo ya kukarabati  au/na kuongeza nyumba , kujenga na kununua nyumba. Biashara hii imekuwa ikikua na kukubalika sana na wateja.
Changamoto kubwa ya mikopo hii imekuwa ni gharama kubwa za viwanja, ujenzi au ununuzi wa nyumba ambazo zimekuwa zikiongezeka sana.

Nadhani hili si geni kwa watanzania wengi. Gharama za viwanja zipo juu zaidi kwa viwanja vilivyopimwa. Si ajabu leo hii kusikia fulani amenunua kiwanja kwa bei ya zaidi ya shilingi milioni 200. Hili limefanya nyumba ziwe na bei ya juu sana na hivyo kuwafanya watanzania hata wenye bidii sana kushindwa kumudu.

Pia CRDB Benki imekuwa ikikopesha wateja wafanyao biashara za kati na kubwa. Hapa  Benki imekuwa ikikopesha katika nyanja zote, ununuzi wa majengo, ujenzi wa majengo, na pia ukarabati wa majengo ya biashara kama hoteli, shule na kadhalika. Haya majengo marefu maarufu kama “skyscappers” ni baadhi tu ya majengo hayo.   
Hali ya usoni ya Uchumi wa nchi

CRDB Benki imefurahishwa na kitendo cha serikali yetu kupitia Benki kuu kuingilia kati kuanguka kwa thamani ya shilingi yetu dhidi ya fedha za kigeni pia juhudi zake za kupunguza mfumuko wa bei. Tumefarijika pia na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme nchini.

Hivi vyote vinaashiria kuwa hali ya uchumi itaendelea kuimarika na biashara ya wateja wetu kwa minajili hiyo, biashara ya benki itaimarika zaidi. 

Nimalize kwa kuwashukuru sana kwa kuja kwenu hapa, kuuitikia mwito wa CRDB Benki. Nimefarijika sana kukutana nanyi tena baada ya kitambo kidogo kupita. 
Nawaona mna siha njema. Kwa wale ambao hatutaonana hivi karibuni, nawatakia Idd njema.

Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment